Mataifa Afrika yakutana Zanzibar kuweka mikakati wa magonjwa ya mlipuko

Unguja. Wataalamu wa afya na watunga sera kutoka mataifa ya Afrika wamekutana Zanzibar kujadili mbinu na kuweka utayari wa kukabiliana na dharura za kiafya kwa kuzingatia maendeleo ya miji na vijiji.

Katika mkutano huo wa siku mbili uliofungwa jana Jumamosi Juni 15, 2024, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Andamicheal Ghirmay amesema wakati mataifa yakizingatia ukuaji wa miji, ni vyema kuzingatia miundombinu salama pale yatakapotokea maafa ya kiafya, husuani ya mlipuko.

Alisema katika kipindi cha miaka 15 ijayo, zaidi ya nusu ya wakazi wa Afrika, inatarajiwa kuishi maeneo ya mijini, hivyo kukosena kwa utayari wa kukabiliana na dharura za kiafya kutasababisha mamilioni ya watu kuwa hatarini.

Dk Ghirmay amesema magonjwa ya mlipuko yanakuwa kasi kuliko inavyotarajiwa na kwa sasa ukanda wa Afrika unashughulika na magonjwa ya mlipuko 85 na majanga 35 ya kibinadamu.

“Kadri tunavyoendelea tunatakiwa kuwa na mipango ya dharura katika mipangomiji yetu, kuhakikisha uhusishaji wa jamii na bajeti vinajitosheleza, kukabiliana na majanga haya,” amesema 

Amesema WHO inajizatiti kuzisaidia nchi za Afrika kuimarisha huduma zao za afya za dharura na kuzijengea uwezo wa kiutendaji. 

Alisema kwa Tanzania na Zanzibar wamefanikiwa kusaidia utaalamu na kuongeza uwezo katika kushughulikia magonjwa ya mlipuko.

Ametolea mfano wa magonjwa wa Marburg, kipindupindu, surua na Uviko-19 ambapo walishirikiana, hivyo wakajua umuhimu wa kujiweka tayari kwa kuwa na vikosi kazi vya kushughulikia magonjwa hayo.

Amesema kujitokeza kwa janga la Covid-19 katika miaka ya karibuni imeonyesha udhaifu na umuhimu wa kuwa na mifumo imara ya afya, yenye uwezo wa kukabiliana na dharura hizo hasa katika maeneo ya mjini.

“WHO itaendelea kutoa msaada wa rasilimali na utaalamu ili kuhakikisha mazingira ya mijini nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla yanakuwa na uwezo wa kukabiliana na dharura za kiafya mara zinapotokezea,” amesema   

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Dk Islam Seif Salum amesema upangaji holela wa mipango miji nao unasababisha kutokea kwa majanga ya kiafya nchini.

Amesema Serikali itaendelea kuchukua jitihada za kukabiliana na dharura za kiafya ili kuwanusuru wananchi kutokana na maafa. 

Amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau imeamua kuweka mipango miji yenye miundombinu rafiki ili kuiweka nchi salama wakati maafa yanapotokea.

 “Uratibu na ufuatiliaji bora, umeweza kuongeza uwezo wetu wa kukabiliana na maafa ya kiafya wa haraka endapo yatatokezea, kutokana na ushirikiano wetu na washirika wengine wa maendeleo ikiwemo wenzetu WHO,” amesema.

Amesema kasi ya ukuaji wa miji barani Afrika, ikiwemo Zanzibar, imeongezeka na kuleta changamoto kubwa za kiafya hasa maeneo ya mjini kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya watu na kukua kiuchumi. 

Hata hivyo, amewataka wananchi kuendelea kufuata miongozo inayotolewa na Serikali kupitia wataalamu wa afya, ili kujikinga na majanga.

“Zanzibar imeweza kupambana na maradhi na kuna historia ya kuondoa kipindupindu kwa kuwa kuna mifumo ambayo inasaidia na ndio maana mkutano huu umekuja hapa ili waweze kujifunza,” amesema

Amewataka wnanchi kuzingatia miongozo inayotolewa na wataalamu kujikinga na magonjwa yanayoepukika.

Baadhi ya washiriki wa mkutano huo wamesema wamepata utaalamu na maarifa ya kuandaa mikakati madhubuti ya kujiandaa kwa dharura za kiafya sambamba kuwa na uwezo wa kulinda afya kwa ajili ya ustawi wa jamii.

“Hizi mbinu za kuweka miji zitatusaidia kujua nini cha kufanya kwa hiyo ni jambo muhimu,” amesema mtaalamu wa mipango miji, Oscar Jabir kutoka Ghana.

Washiriki wa mkutano huo wametoka Tanzania, Nigeria Thailand, Botswana, Ghana na China.

Related Posts