Kunani Ikulu kwa mabadiliko haya?

Moshi/Dar. Kuna nini Ikulu? Ndilo swali linaloonekana kuwasumbua Watanzania wengi kwa sasa, baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kufanya mabadiliko mengi mfululizo ya wasaidizi wake katika kipindi kifupi, kati ya Mei na Juni mwaka huu.

Katika kipindi hicho, mkuu huyo wa nchi amefanya mabadiliko ya wasaidizi wake 10, wanane kwa Juni pekee na wawili Mei, mwaka huu.

Mabadiliko hayo yanahusisha kuwaondoa baadhi ya wasaidizi wake katika Ofisi ya Rais Ikulu na kuwateua katika mamlaka, idara na taasisi nyingine mbalimbali za Serikali.

Wakati wengi wakihoji kunani nyuma ya mabadiliko hayo, wanazuoni wa siasa na uongozi, wanahusisha mabadiliko yanayofanywa ama na harakati za kuelekea uchaguzi, kuziba ombwe la wasiowajibika au kuongeza ufanisi.

Wanataaluma wengine wamekwenda mbali zaidi na kuyafananisha mabadiliko hayo na kile walichokiita usafishaji wa nyumba iliyochafuka kitambo.

Ingawa ni mamlaka ya Rais kuanzisha na kufuta nafasi za madaraka mbalimbali katika utumishi, kwa mujibu wa Ibara ya 36(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bado uamuzi wake unaibua mijadala.

Mijadala zaidi katika mitandao ya kijamii iliibuka katika mabadiliko aliyofanya Juni 6, 2024 alipomhamisha Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus kwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu.

Katika maoni yake kuhusu mabadiliko hayo, mchambuzi wa masuala ya siasa, Bubwerwa Kaiza ametaja mambo mawili ikiwemo changamoto ya taarifa katika ziara ya Rais Samia nchini Korea, iliyolazimu Serikali kutoa ufafanuzi.

“Nadhani kutakuwa na shida. Kwa hali ya kawaida kusingekuwa na haraka haraka kama hivi hadi wengine wanapangiwa vyeo ambavyo havina upungufu katika taasisi. Lakini nafasi zinatengenezwa ili kupata nafasi ya kuhamisha maofisa hawa,” amesema alipozungumza na Mwananchi.

Mchambuzi huyo kwa upande mwingine amehusisha mabadiliko yanayofanywa na Rais Samia na maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwakani.

“Sina ushahidi lakini nazungumza kwa uchambuzi kulingana na yanayojitokeza. Nafikiri suala la uchaguzi mwaka huu na mwaka wa kesho linaweza kuwa sababu mojawapo kwa kinachotokea, haya ni maandalizi ya watu wanaotakiwa kuwepo hapo (ofisini),” amesema Kaiza.

Mchambuzi huyo amesema katika hamishahamisha hiyo, anadhani pengine Rais Samia anataka kuweka watendaji watakaomsaidia katika chaguzi zijazo, inawezekana watu watakaopatikana ndio watakuwa msaada katika jukumu hilo.

Mbali na mtazamo wa kaiza, mwanahabari na mchambuzi wa masuala ya siasa na uongozi, Absalom Kibanda anaona uamuzi wa Rais Samia juu ya maofisa hao waandamizi Ikulu, unalenga kusafisha nyumba.

“Nyumba imechafuka lazima isafishwe na hili halina maana ya sijui matakwa ya kiuchaguzi au matakwa ya nini. Wakati wowote katika maisha ya uongozi, nyumba inapaswa kuwa safi,” amesema.

Kwa mujibu wa Kibanda, aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) anachokifanya mkuu huyo wa nchi ni kupanga safu ya wasaidizi wake kwa kile alichoeleza kuwa mambo hayakuwa sawa.

Akifafanua hoja ya mambo kutokuwa sawa, amesema kulikithiri usambaaji wa taarifa za upotoshaji na hakukuwa na hatua madhubuti zilizokuwa zinachukuliwa.

“Huo ni wajibu ambao baadhi ya wasaidizi wa Rais walipaswa kufanya na kuna watu pengine wameshindwa kutimiza wajibu wao huo, kwa sababu huwezi kutegemea kila wakati Rais mwenyewe ndiye atoe majibu wakati ana wasaidizi wengi,” amesema.

Kibanda amekwenda mbali zaidi na kueleza kuwa mabadiliko yanayoshuhudiwa yanapaswa kuwa angalizo kwa watendaji waliopo serikalini hadi sasa.

Amewataka wajiweke sawa na kutambua wajibu wao kwani wakati wowote wanaweza kukumbwa na hatua kama hizo.

“Upo ushahidi wa kihistoria na kimazingira, kwamba katika miaka mitatu ya Rais Samia hana hiyana katika kufanya mabadiliko, hata kwa nafasi moja katika miaka kadhaa wakabadilika watu watatu au wanne, haimpi shida,” amesema.

Hata hivyo, mwanahabari huyo amesema pengine aliyekuwa Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi ndiye anayetarajiwa kuziba baadhi ya nafasi zilizoonekana kuwa na mapengo.

“Mobhare anakwenda kupata nafasi kubwa zaidi, yenye majukumu makubwa zaidi na inawezekana ikawa ni eneo ambalo anaonekana ana nguvu na uwezo zaidi, hilo wala huhitaji kuambiwa, ukisoma taarifa ya Rais inasema amepangiwa majukumu mengine,” amesema.

Amesema hiyo inamaanisha  kwamba kuondolewa kwake (Matinyi) katika wadhifa aliokuwa nao sasa ni kwa sababu tayari kuna majukumu mahususi aliyopangiwa.

Hata Dk Aviti Mushi anaungana na Kibanda katika hoja kuwa, mzizi wa mabadiliko hayo, licha ya kushtua, lengo kuu ni kuisafisha Ikulu.

“Nadhani (Rais) ameona hawawezi kuendana na kasi yake, sio viongozi wabaya, lakini labda anataka kuwepo na wengine kuimarisha ofisi ya Ikulu,” amedai Dk Mushi.

Hata hivyo, Dk Mushi naye amegusia suala la maandalizi ya uchaguzi kama sababu nyingine ya mabadiliko hayo, akisisitiza kuwa, “uchaguzi si lelemama.”

Kwa mtazamo wa Kiama Mwaimu uamuzi wa mabadiliko ya wasaidizi hao, unaweza kusababishwa na baadhi yao kushindwa kumsaidia katika anachokitarajia.

“Inawezekana pia hawa watumishi kwa mtazamo wa Rais hawawezi kumpa ushindi katika chaguzi zijazo au katika utawala bora kwenye Serikali yake,” amesema Mwaimu ambaye ni mmoja wa wachambuzi wa masuala ya siasa.

Akizungumzia maadili ya viongozi, Paul Kimiti aliyewahi kuwa waziri na mkuu wa mikoa mbalimbali nchini, amesema huenda kuna tatizo kwa wasaidizi wa Rais wanaomsaidia kuteua viongozi.

“Tatizo sisi watendaji hatumsaidii Rais, yeye hawajui wote hawa, anapelekewa na wengine anapelekewa kwa sababu ni marafiki wa mtu fulani. Zamani kulikuwa na ‘vetting’ sio mtu mmoja anaweza kupeleka majina yote,” amesema Kimiti alikijibu swali la waandishi wa habari aliozungumza nao nyumbani kwake, Dar es Salaam jana.

Amesema katika uteuzi huo, watu wenye sifa mbalimbali wanapaswa kuchunguzwa na kupimwa uwezo wao kabla ya kuteuliwa kwenye nafasi husika.

“Nitacheki na watu wengine, nitaangalia marafiki zake, tabia nijue, halafu familia niijue. Ndio maana zamani ukiteuliwa kwa sababu vetting imefanyika unakaa miaka mingi. Siku hizi ndio hao unaona wanafanya madudu ya ajabu, miezi miwili mitatu umetenguliwa, mwaka mmoja miwili umetenguliwa. Ujue kuna makosa yanafanyika, wanamwingiza Rais wetu kwenye matatizo,” amesema Kimiti.

Ametoa mfano wa nchi nyingine bila kuzitaja, akisema wanashindanisha nafasi kwa kuangalia uwezo wa watu.

“Kuna nafasi ya mkuu wa mkoa mahali fulani, sio kuteua tu, kwanza unaangalia mkoa ule wa namna gani? Hali yake, nani anafaa? Watu wawili watatu unawaangalia. Sio kusema tu, Kimiti mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

“Dar es Salaam inataka aina ya watu, tofauti na mtu utakayempeleka Rukwa, Lindi na Mtwara. Wakorofi wote wako hapa (Dar es Salaam).”

Panga pangua Ikulu ilianza siku chache tu baada ya Rais Samia kuapishwa kushika wadhifa huo, Machi 19, 2021 kuchukua nafasi ya Rais John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17 mwaka huo.

Baada ya kuapishwa alimwondoa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Bashiru Ally na kumteua kuwa mbunge huku nafasi yake ikichukuliwa na Balozi Hussein Kattanga Machi 31, 2021.

Aprili 4, 2021 alimuondoa Gerson Msigwa katika wadhifa wa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, baada ya kuhudumu kwa miaka sita tangu Agosti mwaka 2016 wakati wa utawala wa Magufuli na kumteua kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali.

Nafasi aliyokuwa nayo Msigwa ndani ya ofisi hiyo nyeti ilirithiwa na Jaffar Haniu aliyeteuliwa Juni mwaka 2021 lakini naye hakudumu, Februari ya mwaka uliofuata aliondolewa na kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya Rungwe, akimpisha Zuhura Yunus.

Katika panga pangua hiyo, Moses Kusiluka aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu Ikulu na Januari 2023 Diwani Athumani aliteuliwa kumrithi. Diwani alidumu kwa siku mbili tu, baadaye nafasi hiyo ilirithiwa na Mululi Mahendeka anayeongoza hadi sasa.

Ingawa haionekani kama ni ofisi ya moja kwa moja Ikulu, lakini Agosti 28, 2023 Rais alifanya mabadiliko ya mkurugenzi mkuu wa usalama wa Taifa na kumteua Ali Idi Siwa akichukua nafasi ya Said Hussein Massoro aliyehudumu kwa miezi minane.

Tangu mabadiliko hayo, umma haukushuhudia mabadiliko ya mara kwa mara kwa wasaidizi wa Rais hadi Mei na Juni 2024, miezi inayoonekana kuvunja rekodi ya hamishahamisha hadi baadhi ya watu kuanza kuhoji kuna nini Ikulu?

Januari 2024, Rais Samia alimhamisha ofisa mwandamizi Ofisi ya Rais Ikulu, Doris Kalasa na kumteua kuwa Katibu Tawala (RAS) mkoa wa Iringa.

Mei 29,2024, Rais akamhamisha Dk Linda Ezekiel aliyekuwa Kaimu ofisa mtendaji mkuu wa President’s Delivery Bureau (PDB) kwenda kuwa naibu katibu mkuu mtendaji, Tume ya Mipango nchini, anayeshughulikia ubunifu wa biashara.

Juni 6, Rais akamhamisha Felister Mdemu aliyekuwa msaidizi wa Rais (Maendeleo ya Jamii) kwenda kuwa naibu katibu mkuu Maendeleo ya Jamii na Zuhura Yuhus kutoka mkurugenzi wa mawasiliano Ikulu kwenda kuwa naibu katibu mkuu.

Pia tarehe hiyohiyo, akamuondoa Petro Magoti aliyekuwa msaidizi wa Rais (siasa) kwenda kuwa mkuu wa Wilaya Kisarawe na akamhamisha pia Nehemia Mandia aliyekuwa Msaidizi wa Rais (sheria) na kumteua kuwa jaji wa Mahakama Kuu.

Halikadhalika, Juni 11, 2024 akamwondoa msaidizi mwingine Elias Mwandobo kwenda kuwa mkuu wa Wilaya ya Momba.

Juni 15,2024, akamhamisha Balozi John Simbachawene aliyekuwa ofisa mwandamizi Ofisi ya Rais, Ikulu kwenda kuwa naibu katibu mkuu wizara ya Viwanda na Biashara na pia Dk Habib Kambanga mwenye wadhifa kama huo kuwa balozi.

Pia akamhamisha Ofisa Mwandamizi wa Ofisi ya Rais Ikulu, Mkoba Mabula, kwenda kuwa Naibu Katibu mkuu katika wizara ya Maliasili na Utalii, wizara ambayo huwa mawaziri wake pia huwa hawadumu muda mrefu.

Imeandikwa na Daniel Mjema (Moshi), Juma Issihaka, Bakari Kiango na Elias Msuya (Dar

Related Posts