Kigoma. Wananchi wa Kijiji cha Basanza Wilayani Uvinza, Kigoma wameiomba Serikali kuwaondoa kazini madaktari na wahudumu wa afya wasio na huruma na utu kwa wagonjwa.
Hayo yamesemwa leo Jumapili Juni 16, 2024 na wakazi wa kijiji hicho mbele ya mkuu wa mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye aliyetembelea zahanati ya Basanza na kuzungumza na watumishi na wananchi baada ya video iliyokuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonyesha Prisca Makenzi (17), anayedaiwa kujifungua bila msaada wa mtoa huduma.
Wananchi hao wamesema ni vema Serikali ikafanya mabadiliko ya utumishi katika zahanati hiyo.
Mkazi wa Basanza, Pelesi Leonard amesema mara zote wagonjwa wanaofika kwenye zahanati kutibiwa, wanalalamikia huduma mbaya hasa wajawazito, hali inayohatarisha maisha yao na watoto wanaotarajia kujifungua.
Amedai imekuwa kawaida kwa wajawazito kujifungulia sakafuni au mlangoni kwa sababu hakuna anayewajali.
“Daktari naye akifika na kukukuta mjamzito umejifungulia chini bila usaidizi anakufokea huku akisema kwa nini usisubiri hadi yeye afike ndio ujifungue, jamani uchungu huwa unamsubiri mtu? Mimi mwanamke nawezaje kuuzuia uchungu?,” amehoji Leonard.
Amemuomba mkuu wa mkoa wafanye uchunguzi wa haraka kwenye zahanati hiyo, ili watakobainika kutokuwa na utu kwa wagonjwa wafukuzwe kazi.
“Tunakuomba mkuu wa mkoa mtuondolee madakta hawa, mtuletee wengine,” amesema Leonard.
Naye Agnes Maduhu, amesema imefikia hatua kwa wajawazito kijijini hapo kutoona umuhimu wa kwenda kujifungulia kwenye zahanati hiyo, ili kukwepa unyanyasaji na huduma mbovu.
“Kama mjamzito hawezi kupokelewa vizuri zahanati na kupewa huduma muhimu, ni bora tukajifungulia nyumbani kuna usalama zaidi kuliko kwenda hospitali na kukosa huduma na kujifungua bila usaidizi wa mtoa huduma hatua ambayo ni hatari zaidi, wanaweza wakafa mama na mtoto kwa uzembe wa mtu mmoja,” amesema Maduhu.
Baada ya kusikiliza kero za wananchi, Andengenye ametoa maagizo kwa Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma, kuunda kamati itakayochunguza tuhuma hizo.
“Hii haiwezi kukubalika, katibu tawala unda kamati, tufuatilie tuhuma za watumishi wa idara ya afya wanaotuhumiwa kukiuka maadili ya kiutendaji wakati wa kutoa huduma kwa wagonjwa,” amesema Andengenye.
Amesema Serikali haiwezi kuwavumilia watumishi wanaokwamisha jitihada zake za kuwafikishia huduma bora za afya wananchi. “Na yeyote atakayebainika, hatua kali za kisheria zitachukuliwa, ikiwamo kufukuzwa kazi, watumishi wa aina hii hatuwahitaji,” amesema mkuu huyo wa mkoa.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Hassan Rugwa amewasisitiza watumishi wa idara ya afya kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia taaluma.
Amesema Serikali imewekeza fedha nyingi katika sekta ya afya kwa lengo la kuwapunguzia mzigo wananchi wa kufuata huduma mbali na maeneo wanayoishi.