Geita. Mamia ya wananchi wameshiriki maziko ya aliyekuwa Diwani wa Kamena Halmashauri ya mji wa Geita, Peter Kulwa (67) aliyefariki dunia Juni 13, 2024 na kuacha watoto 34, wajukuu 129 na vitukuu 10.
Kwa mujibu wa risala iliyosomwa na mjukuu wake, Makutano Sadick, diwani huyo alianza kuugua kisukari Mei 2002 na kupatiwa matibabu katika hospitali mbalimbali nchini na Juni, 2024 akiwa anaendelea na matibabu Hospitali ya Kamanga iliyopo Jijini Mwanza, mauti yalimfika.
Alisema babu yake ameacha watoto 34, wajukuu 129 na vitukuu 10.
“Alianza kuugua Mei 2002 na alitibiwa hospitali mbalimbali za hapa Geita, Singida na Mwanza, alikuwa akipata nafuu na kuendelea na majukumu yake, lakini ilipofika Aprili 10, 2024 hali yake ilizidi kuwa mbaya tukampeleka Hospitali ya Kamanga alikoendelea na matibabu hadi Juni 13,2024 saa tisa alasiri alifariki dunia,” amesema Sadick.
Akizungumzia maisha ya babu yake, Sadick amesema alikua mtu mwenye upendo aliyewafundisha kujitegemea, kufanya kazi kwa bidii.
“Tutamkumbuka kwa upendo wake lakini zaidi ni mtu aliyeamini kwenye kufanya kazi na kazi yake kubwa ilikua kilimo na ameacha alama ambayo haitafutika kwetu, alilima mazao ya chakula na ya biashara hatukuwahi kupungukiwa,” amesema Sadick.
Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Geita, Hadija Said amesema wataendelea kuenzi mema yote yaliyofanywa na diwani huyo ambaye alikuwa mshauri wa wengi, mwenye hekima na busara.
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba akitoa salamu za pole amesema licha ya kutoonana naye, lakini alikuwa akiwasiliana naye mara kwa mara kwa simu kumjulia hali akiwa hospitali.
Hata hivyo, amewataka wananchi kuyaenzi mema yote yaliyofanywa na diwani huyo wakati wa uhai wake.
Shida Elias mkazi wa Kamena akimzungumzia diwani huyo amesema alikuwa na upendo na alijali sana masilahi ya wananchi, ndiyo sababu aliweza kuongoza kwa muda mrefu kwenye kata hiyo.
“Tunamkumbuka kwa mengi pamoja na kuwa diwani, lakini hata kabla ya kuwa kiongozi, alikuwa mtu aliyependa maendeleo, wengi hatujasoma lakini alikua akisema elimu yetu ni jembe hivyo tulime sio ili tupate chakula tu, alitaka kilimo biashara ndio maana aliwekeza kwenye viazi vitamu na hadi sasa kata yetu ndio inaongoza kwa uzalishaji wa viazi vitamu vinavyopelekwa mikoani, hii ni alama aliyoiacha kwetu,” amesema Elias.