BAADA ya kumalizana na winga Joshua Mutale (22), mabosi wa Simba wamedaiwa hawajamaliza kazi huko Zambia baada ya kuhamia kwa kiungo mkabaji wa Zesco United, Kelivin Kapumbu (28) kwa nia ya kumvuta Msimbazi kukiwasha kwa msimu ujao wa mashindano ya ndani na yale ya kimataifa.
Hata hivyo, taarifa hizo kutoka ndani ya Simba zinasema kuwa mabosi wa klabu hiyo hasa wanaosimamia usajili wamegawanyika juu ya umri wa chezaji huyo, japo walio wengi wanapendekeza aletwe hata kwa mkataba wa muda mfupi kwani ana kitu kitakachoibeba timu hiyo katika Kombe la Shirikisho Afrika.
Hii sio mara ya kwanza kwa Simba kuhitaji huduma ya Kapumbu, kwani walishawahi kumfuata miaka miwili nyuma, kipindi hicho akiichezea Zanaco na mchezaji huyo akiwa katika kiwango cha juu, lakini dili lilibuma kutokana na mabosi wa Msimbazi kushindwa kuvunja mkataba aliokuwa nao na Wauza umeme wa Zambia.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, mmoja wa vigogo wa Simba alienda Zambia kukamilisha dili za nyota wawili wanaohitajiwa Msimbazi, akiwamo Mutale ambaye inaelezwa kila kitu kimekamilika, ndipo ikamgeukia Kapumbu, lakini ghafla jina hilo lilipotua kwa viongozi wengine wakaanzisha mjadala juu ya umri alionao.
Wapo wanaokubaliana na mazungumzo hayo yaendelea ili jamaa atue Msimbazi, lakini wengine wakiona anakwenda kumaliza soka, hivyo ni bora wakaendelea kuwaamini waliopo ndani ya kikosi hicho. ambao kiumri hawatofauti nao sana.
Msimu uliomalizika, Simba ilikuwa na viungo wakabaji wanne akiwamo Mzamiru Yassin, Sadio Kanoute, Fabrice Ngoma na Babacar Sarr, ambao baadhi ya viongozi wanaona bora waendelee kusalia hao, japo jina la Sarr likiwekewa mstari mwekundu na kama akitoka basi ndipo Kapumbu aingie kuzina nafasi yake.
Mwanaspoti limepata taarifa kwa mmoja wa viongozi wa klabu ya Simba, kwamba ukuachana na winga Joshua Mutale (22), aliyesainisha miaka miwili na sasa wapo katika mchakato wa kumalizana na klabu ya Power Dynamos anayoitumikia.
Anayesimamia usajili huo ni Crescentius Magori ambaye ni mshauri wa Rais wa Heshima wa Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’ ambaye imelezwa bado yupo Zambia kukamilisha dili hilo la Kapumbu ambaye anamaliza mkataba wa Zesco mwishoni mwa mwezi huu.
Ukiachana na wachezaji hao kutoka Zambia, usajili mwingine ambao Simba, imefanya ni wa beki Lameck Lawi kutoka Coastal Union.
Kapumbu aliyeanza kucheza soka la ushindani tangu mwaka 2016 anatumia mguu wa kulia na aliwahi kupita katika timu za Zanaco na Lumwana Radiants, akisifiwa pia kwa uwezo wa kutuliza timu na kupiga pasi zenye macho ma mtibuaji mipango ya timu pinzani mbali na utulivu mkubwa alionao.
Beki wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Amir Maftah alisema; “Umri wa Kapumbu sio mbaya, ingawa nasisitiza Simba inahitaji kusajili vijana zaidi ambao wataongeza nguvu wengine waliopo, tena wanapaswa kuongeza wachezaji wa maana kuanzia wanne hadi watano.”
Aliyekuwa kocha wa makipa wa timu hiyo, Idd Pazi kwa upande wake, alisema; “Simba inahitaji utulivu kusajili wachezaji wenye tija,ambao watakuja kuongeza kitu kipya ndani ya kikosi msimu ujao, ili kuirejesha furaha ya mashabiki wao, baada ya kukosa ubingwa ndani ya misimu mitatu mfululizo.”
Huu ni msimu wa tatu kwa Simba ikiwa haijatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara wala Kombe la Shirikisho na imekuwa ikihaha kusaka kiungo mkabaji wa uhakika tangu ilipoachana na Taddeo Lwanga kutoka Uganda na Mbrazili Gérson Fraga Vieira, kwani wachezaji waliosajiliwa kuziba nafasi hiyo walichemsha kutokana na kucheza juu zaidi kuliko chini, japo Babacar Saar na Ismael Sawadogo walionekana kufiti ila walikosa kasi.