Yanga yamficha winga mpya Avic

YANGA bado inapiga hesabu za kusajili winga wa maana na mezani kwao kuna mawinga wawili akiwemo Philipe Kunzumbi na Basiala Agee, lakini mmoja kati ya hao wawili akawahishwa kambi ya klabu hiyo ya Jangwani iliyopo Avic Town fasta akiwekewa mtego wa maana.

Yanga ilimfungia safari Agee baada ya Rais wa klabu hiyo, Injinia Hersi Said kumsoma winga huyo kwa macho wakati timu anayoichezea ya  AS Union Maniema ikicheza dhidi ya FC Lupopo.

Mbali na Agee, pia Hersi alikuwa akimsoma beki mpya wa kushoto Chadrack Boka ambaye dili lake limeshakwisha na kubaki winga huyo wa Maniema.

Hata hivyo, katika mchezo huo Maniema ikawapiga chenga Yanga ikimchezesha winga huyo kama kiungo mshambuliaji wa juu, yaani namba 10 badala ya ile ya kushambulia akitokea pembeni jambo lililowavuruga na kushindwa kuuona ubora waliojulishwa mapema akicheza eneo la pembeni.

Fasta mabosi wa Yanga wakakuna vichwa na sasa imepanga kutumia akili kubwa kumsoma winga huyo hapa hapa nchini kimafia baada ya kuipa mualiko AS Maniema kuja kufanya maandalizi ya msimu kwa kambi yao kuwekwa pale kambini Avic, Kigamboni.

Mabingwa hao wa Tanzania uhakika ni kwamba kambi yao ya maandalizi ya kuelekea msimu mpya hawataiweka Avic na itakuwa nje ya nchi, nafasi kubwa ikiwa inataka kutimkia Urusi au kama Afrika itakuwa Afrika Kusini au Kenya.

Kuondoka huko kukaipa nafasi Yanga kuialika Maniema, huku mabosi wa Yanga wakitaka kumsoma zaidi Agee ambaye ni fundi wa mipira ya adhabu ndogo kama ambavyo Stephanie Aziz KI anachokifanya.

“Tunataka tumuangalia zaidi, kilichotuishtua ni uwezo aliouonyesha katika mechi ya Ligi dhidi ya TP Mazembe na Maniema ikishinda kwa mabao 2-0, alicheza kwa kiwango kikubwa sana kama winga,” alisema bosi mmoja wa juu wa Yanga na kuongeza;

“Ukiacha hayo yote lile bao alilowafunga Mazembe la adhabu ndogo, likatushtua zaidi kuwa kama tukimpata Agee, huku akiwa anapiga adhabu kwa mguu wa kulia na kule akiwa Aziz tuitakuwa  na nguvu zaidi. Timu yao itakuja hapa tutamuangalia na kama ataturidhisha tutafanya maamuzi hata kama timu yetu itakuwa haipo kwa kuwa kocha anajua kwamba tulikuwa tunamfuatilia.”

Jana bosi mmoja wa juu wa Maniemna, Guy Kapia amelithibitishia Mwanaspoti kuwa Maniema itakuja Tanzania wiki ya kwanza ya Julai kwa kambi hiyo maalum ya maandalizi ya msimu mpya.

“Tutakuja Tanzania, kuanzia mapema Julai na tutacheza mechi za kirafiki hapo, tunawashukuru wenzetu Yanga kwa kutupa mualiko huu,” alisema Kapia na kuongeza; “Kocha wetu Papy (Kimoto) ameridhia kambi yetu iwe Tanzania, kikubwa alikuwa anataka eneo zuri lililotulia ili timu ifanye maandalizi vizuri, mimi nilikluja hapo Tanzania na nilifika pale kambi ya Yanga ni eneo sahihi kwetu.”

Related Posts