Mkurugenzi Mtendaji wa Bank Of Africa Tanzania, Esther Cecil Maruma (kushoto) akisaini kitabu cha wageni wakati alipofanya ziara ya kikazi kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mh.Rosemary Senyamule mwishoni mwa wiki, (Kulia) ni Meneja wa Fedha wa benki hiyo, Derick Lugemala.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bank Of Africa Tanzania, Esther Cecil Maruma (katikati kulia) akieleza mikakati ya benki hiyo kuwezesha wananchi kujikwamua kiuchumi kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Mh.Rosemary Senyamule wa kwanza mstari wa kushoto wakati alipomtembelea ofisini kwake akiongoza ujumbe wa maofisa waandamizi wa benki hiyo pichani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bank of Africa Tanzania, Esther Cecil Maruma (katikati) akiongozana na Maofisa waandamizi wa Benki hiyo Mkuu wa Masoko na Mawasiliano,Nandy Mwiyombela (kulia) na Meneja wa Fedha wa benki hiyo, Derick Lugemala (kushoto) wakiwa eneo la ofisi za Bunge jijini Dodoma walipoenda kusikiliza bajeti kuu ya serikali .
BANK of Africa Tanzania imeipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuja na bajeti yenye mwelekeo wa kuchochea ukuaji wa biashara sambamba na maendeleo ya kiuchumi nchini.
Pia imeeleza dhamira yake ya kuendelea kuboresha huduma zake katika kuhudumia makundi yote ya wateja kuanzia wateja binafsi, Wafanyabiashara na makampuni katika kufanikisha ajenda za Serikali za kukuza ushirikishwaji wa kifedha nchini Tanzania.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bank of Africa Tanzania, Esther Cecil Maruma amebainishwa hayo hivi karibuni wakati akitoa maoni kuhusiana na bajeti ya Serikali ya kipindi cha mwaka 2023/2024 iliyosomwa bungeni na Waziri wa Fedha, Mh.Mwigulu Nchemba ambapo pia alihudhuria kikao cha bajeti akiwa ameongoza ujumbe wa maafisa wengine waandamizi wa benki hiyo.
Amesema bajeti hii imelenga zaidi kuchochea maendeleo ya wananchi kupitia ukuzaji wa shughuli za kuwaletea maendeleo na kukuza uchumi wa nchi ambavyo kama zilivyo nchi nyingi duniani uchumi katika miaka ya hivi karibuni uliporomoka kutokana na changamoto mbalimbali za kidunia za janga la Covid 19 na vita.
Pia amesema serikali imekuwa na mwelekeo wa kuendelea kutekeleza Sera za Bajeti na fedha zinazolenga kuwezesha sekta binafsi na makampuni makubwa ambapo hatua hizo ni kuendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara , kulinda thamani ya shilingi sambamba na kuongeza wigo wa ukusanyaji wa kodi.
Maruma amesema Benki hiyo inaendelea kuwa na nafasi nzuri kimtaji na kuendesha shughuli zake kwa kuzingatia kanuni za Mamlaka za usimamiaji wa shughuli za kifedha nchini na inayo mtaji wa kutosha kuendesha biashara kama inavyotakiwa na uwezo wa kutoa huduma kwa njia ya kidijitali na benki inaendelea kubadilika na kuwa bora zaidi, kuvutia wateja wengi wapya na wateja waliopo.
Wakati huohuo Mkurugenzi Mtendaji wa Bank of Africa Tanzania, Esther Cecil Maruma , alipata fursa ya kutembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ,Tawi la benki hiyo la Dodoma na wadau mbalimbali wa benki hiyo.
Katika mkutano na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma alimweleza mikakati mbalimbali ya benki na jinsi ilivyojipanga kushirikiana na Serikali katika kuchangia kukuza uchumi wa taifa na kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanzania.