Dar es Salaam. “Kwa hali ilivyo, barabara ilivyojaa vumbi, huwa natembea na nguo nyingine katika begi, nikifika ofisini nabadilisha ili niwe huru kazini.”
Ndivyo anavyoelezea Alfred Zacharia, mkazi wa Kitunda, jijini hapa na mtumiaji wa barabara ya Gongolamboto hadi Posta yenye urefu wa kilometa 23.33 inayoendelea kujengwa njia ya magari yaendayo haraka.
Ujenzi huo unaoendelea umekuwa ukisababisha vumbi kwa watumiaji, wakati wa jua kali na matope mengi kipindi cha mvua, jambo linalowaathiri watumiaji.
Uwepo wa vumbi hilo, umesababisha baadhi yao kuwa watumiaji kupata vikohozi visivyopona, huku wale wanaosumbuliwa na pumu na mzio ikiwa ni mateso zaidi.
Mbali na magonjwa, baadhi wamekuwa wakilazimika kutembea na nguo mbili katika mabegi yao kama ilivyo kwa Zacharia, ili wawe nadhifu kazini hasa wanaowahi na kutumia usafiri wa bodaboda.
“Mpaka nifike kazini, vumbi limejaa mwili mzima, nywele kama mvi, suruali viatu huwezi kuniangalia mara mbili. Nikifika ofisini lazima uanzie chooni kubadilisha nguo na kuondoa vumbi kichwani, kabla ya kuendelea na ratiba za kila siku,” amesema Zacharia.
Wakati Zacharia akisema hayo, Dickson Masela amesema kwa mwaka mzima sasa amekuwa akitumia dawa za kikohozi bila mafanikio, hali ambayo hakuwahi kuipata zamani.
“Kwa hali ilivyo huwa inanilazimu kupanda pikipiki kila siku asubuhi, ili niwahi kikao kinachoanza saa 2:00 asubuhi kila siku, vinginevyo ningekuwa nafika saa 4 au 3 asubuhi,” alisema.
Katika kukabiliana na hali hiyo, sasa analazimika kuvaa barakoa kila anapokuwa barabarani nyakati za asubuhi na jioni.
Mbali na Masela, Winfrida James amesema hali ya vumbi hilo la barabarani imefanya awe mtumiaji wa dawa za mzio kila wakati, hali inayomnyima uhuru.
“Nikipigwa na vumbi, nitakuna macho, nitapiga chafya, kifua kitabana nitakosa raha siku nzima, sasa hali hii nimekuwa nikiipata siku za hivi karibuni, nikiwaza kwenda kazini naanza kupata mawazo,” amesema Winfrida.
Licha ya kuvaa barakoa, bado amekuwa akipata mafua yasiyopona, hali inayomnyima uhuru wa kutoka eneo moja kwenda lingine.
Akizungumza na Mwananchi Digital, Daktari bingwa wa mfumo wa upumuaji, Dk Elisha Osati amesema vumbi kali huathiri mfumo wa upumuaji wa binadamu pamoja na macho.
Dk Osati amesema vumbi linapoingia katika njia ya hewa mtu huweza kukohoa au kupiga chafya, ikiwa ni moja ya hatua ya mwili kujilinda baada ya kitu kisichokuwa cha kaiwaida kinapoingia katika njia ya hewa.
Amesema vumbi hilo pia linaweza kuingia katika mapafu na kuathiri ukuta wa juu ambao unaweza kuanza kuumuka, jambo ambalo litafanya mwili kukabiliana nalo.
“Pia mirija ya hewa inaanza kupata kama vivimbe ndani yake, uvimbe wa ukuta huo huweza kuvuta seli nyingi, ili ziweze kukinga mapafu.
“Hali hiyo inaweza kuathiri sehemu ya mapafu au kuharibu ukuta laini kwenye mapafu na njia ya hewa ambayo huweza kufanya maambukizi kuingia kirahisi au virusi au kufanya mtu kupata pumu au ugonjwa wa mapafu mkali wa Copd,” amesema Dk Osati.
Dk Osati amesema hali hiyo pia huweza kumfanya mtu kupata maambukizi ya mara kwa mara na uvimbe ukiendelea kwa muda mrefu unaweza kuwa chanzo cha seli za mwili kubadilika katika mapafu ambayo inaweza kutengeneza aina moja wapo ya saratani katika mapafu na njia ya hewa.
Katika macho, amesema vumbi huambatana na chembechembe ndogondogo ambazo zinapoingia machoni hujishika katika ukuta laini wa nje ya macho na kuufanya kuumuka.
Hali hiyo inatajwa kuwa sababu ya baadhi ya watu kuwashwa macho na baadhi kupata ugonjwa wa macho mekundu ‘red eyes’.
Katika hilo, Dk Osati ameshauri kuwa ipo haja ya kumwaga maji barabarani wakati ujenzi ukiendelea, ili vumbi isiwepo kwa kile alichokieleza kuwa bahati mbaya barabara nyingi zinajengwa huku watu wanatumia.
“Watu wanaopita au waishio jirani, pia wachukue tahadhari kwa kuvaa barakoa, ili kuepuka vumbi linaloingia katika mdomo na pua na macho ukajikinga kwa kitambaa kinachoonyesha kama hauwezi kuvaa miwani,” amesema.
Kauli ya msimamzo wa mradi
Msimamizi wa mradi huo kutoka Wakala ya Barabara (Tanroads), Frank Mbilinyi amesema ni wajibu wa mkandarasi kuhakikisha barabara hiyo haiwi na vumbi, huku akiahidi kuwasiliana na mhandisi mshauri ili amkumbushe.
“Unajua tatizo linaweza kuwa ni kukauka, huenda maji yalimwagiwa saa 12 asubuhi hadi saa nne barabara inakuwa imekauka na vumbi linatoka. Pia wanaolalamika wangesema hali imekuwa hivyo kwa kipindi gani kwa sababu tumetoka kwenye mvua nyingi,” amesema Mbilinyi.
Mbilinyi amesema wajibu wa kumwagia maji ni sawa na ule wa kuhakikisha barabara mbadala zinapitika wakati wa mvua kubwa kwa mkandarasi kuhakikisha anazikwangua kuondoa mashimo, ili magari yapite kirahisi wakati ujenzi ukiendelea.