‘Jitokezeni kwa wingi kushiriki chaguzi zijazo’

Dar es Salaam. Waumini wa Kiislam na Watanzania kwa ujumla wametakiwa kujitokeza kwa wingi kushiriki chaguzi zijazo za serikali za mitaa vijiji, vitongoji pamoja na Uchaguzi Mkuu 2025, ili kuwachagua viongozi watakaoletea maendeleo.

Wito huo umetolewa leo Jumatatu Juni 17, 2024 na mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Ally Mubarak alipotoa hotuba muda mfupi baada ya kumalizika kwa ibada la swala la Eid Al Adha iliyofanyika katika msikiti wa Mohamed Vi, Kinondoni jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwamo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mawaziri waandamizi wa Serikali.

Sheikh Mubarak amesema kumekuwa na tabia ya uvivu wa baadhi ya Watanzania kushiriki chaguzi, hasa kupiga kura licha ya kuwa na kitambulisho kinachowawesha kutumia haki hiyo ya msingi na kikatiba.

“Wanabaki kusema oooh…mimi siendi, hilo halipo katika uislamu, lakini nataka niwaambie upigaji wa kura ni thawabu hata Mtume Muhammad alipiga kura. Wewe ni nani hadi ukatae?

“Mkiacha kupiga kura watachaguliwa viongozi wasiostahiki kushika madaraka, nchi yetu ipo vizuri, uchumi unakua na haki za watu zinapatikana kwa wakati na Rais Samia Suluhu Hassan anafanya mambo mazuri, licha ya baadhi ya watu kuyakejeli,” amesema Sheikh Mubarak.

Amewasisitizia Watanzania na Waislamu kujitokeza kupiga kura, ili wapatikane viongozi sahihi watakaoendeleza mambo mazuri yanayofanywa na Serikali.

Amesema kuna watu wanajiita wazalendo, lakini uchaguzi ukifika wanakaa kando sio sahihi.

Katika hatua nyingine, Sheikh Mubarak amekemea vitendo vya vurugu vinavyotokea katika misikiti mbalimbali, hasa ugomvi baina ya maimamu na viongozi wa nyumba hiyo ya ibada.

“Hatua hii inasababisha waumini kuhama misikiti na wengine kufikia uamuzi wa kuacha kuswali na hoja yao kubwa ni viongozi wa dini wanafanya mambo ambayo sio.

“Ndugu zangu Waislamu, misikiti ina vurugu hadi inafika hatua Serikali kuingilia kati.Tuache kugombana ndani ya msikiti athari zake ni kubwa,” amesema Sheikh Mubarak.

Katibu Mkuu wa Bakwata, Alhaji Mruma ametoa wito kwa Waislamu wote kujitokeza kwa wingi katika kila hatua itakayoanza ya mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa, ikiwemo uboreshaji wa daftari la wapigakura.

“Wito wetu kwa Waislamu wanaoona wana sifa za kuongoza wasiache fursa hii adhimu, kwani ni haki yao ya kikatiba inayotekelezwa kupitia vyama vyao vya siasa,” amesema Mruma.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji Jacobs Mwambegele, mchakato wa uboreshaji wa daftari la wapigakura utazinduliwa Julai mosi, 2024 mkoani Kigoma, kisha kwenda mikoa ya Tabora na Katavi kwa awamu ya kwanza.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kudumisha amani, upendo, umoja, mshikamano, kuhurumiana sambamba na kujiepusha na vitendo vinavyoashiria vurugu, uonevu na uvunjifu wa amani.

Pia amewasihi waimarishe malezi kuanzia ngazi ya familia, ili kuepuka athari za mmomonyoko wa maadili nchini na kuhakikisha mienendo ya vijana na wanajamii wote inazingatia mila, desturi na tamaduni zetu.

“Ninawashukuru nyinyi na madhehebu yote ya dini kwa kuendelea kuiombea nchi yetu amani, mshikamano na utulivu. Amani tuliyo nayo, ndiyo chachu kubwa ya kufikia mafanikio ya maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi,” amesema.

 Waziri Mkuu ametumia nafasi hiyo kuipongeza Bakwata kwa mipango na  uratibu mzuri wa shughuli za ibada ya Hijja kwa  mahujaji wa Tanzania kwa mafanikio makubwa na Serikali itaendelea kutoa ushirikiano wa dhati, ili kuwezesha Waislamu kutekeleza nguzo hiyo muhimu.

Pia ametoa wito kwa Bakwata kusimamia weledi wa taasisi zote zinazowapeleka Waislamu Hijja kama wanavyoratibu wao.

Related Posts