SIO ZENGWE: VAR si kipaumbele cha nchi kwa sasa

KLABU 20 zinazoshiriki Ligi Kuu ya England (EPL) zimekubaliana kuendelea na matumizi ya teknolojia ya mwamuzi msaidizi wa video (V.A.R) baada ya kupiga kura katika Mkutano Mkuu wa mwaka kuamua kuhusu hoja ya Wolves iliyotaka teknolojia hiyo iondolewe msimu ujao wa 2024/25.

Wolves iliwasilisha takriban hoja tisa ambazo ilisema zinaharibu mtiririko wa mchezo, kuvuruga furaha ya bao, kuchelewesha na matumizi kupita malengo ya teknolojia hiyo. Iliwasilisha hoja hiyo mwishoni mwa msimu uliokuwa na matukio mengi yaliyovuruga mwenendo wa klabu kadhaa katika kuelekea ubingwa, zikiwemo Manchester United ambayo ilibatilishiwa mabao manne, ikanufaika na mabao mawili huku ikifungwa mabao matatu yaliyotokana na teknolojia hiyo.

Karibu kila timu kwenye Ligi Kuu iliathirika na kunufaika na matumizi ya teknolojia hiyo, kiasi kwamba kulikuwa na wasiwasi kuwa huenda hoja ya Wolves ya kutaka V.A.R iondolewe ingepita kirahisi.

Hata hivyo, baada ya majadiliano marefu klabu zilikubaliana kuendelea na matumizi ya teknolojia hiyo, lakini zikakubaliana kuwa mambo muhimu yaboreshwe na kuwepo na uwazi na ushirikiano wa hali ya juu wa wadau wa mechi za soka, yaani klabu, waamuzi na waendeshaji wa Ligi Kuu.

Hapa Tanzania, Shirikisho la Soka (TFF) limetangaza kuwa mechi za msimu ujao zitakazochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa zitatumia teknolojia hiyo na tangazo hilo likapokelewa na habari njema kutoka serikalini baada ya Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba kuwasilisha kwenye bajeti kuu pendekezo la kuondoa kodi kwenye vifaa vya V.A.R vitakavyoingizwa nchini ili kufanikisha mpango wa kuhakikisha uamuzi katika mechi unakuwa sahihi zaidi.

Ni miezi isiyozidi minne iliyosalia kabla ya msimu mpya kuanza huku nchi ikiwa imetoka katika msimu wa soka uliotawaliwa na maamuzi mabovu ambayo yamechangia kupoteza ladha ya ushindi ingawa kwa kiwango ambacho hakionekani kirahisi.

Kipindi kilichosalia ni kifupi kiasi kwamba ni ngumu kwa mamlaka za soka nchini kutimiza utashi wa protokali za kuomba na hatimaye kuruhusiwa kutumia teknolojia hiyo. Majaribio yanatakiwa yafanyike katika viwanja tofauti kabla yale ya mwisho kufanyika kwenye uwanja mmoja na baadaye kuidhinishwa na Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa).

Hadi ufanye hayo majaribio, maana yake shirikisho limekuwa limeshajiandaa kivifaa na rasilimali watu wa kuweza kuitumia teknolojia hiyo na kutengeneza kanuni zake vizuri kujenga mazingira mazuri ya matumizi, mambo ambayo hayawezi kufanyika katika muda huu mfupi labda tu tuamue kufanya bora liende kama tunavyoendesha mambo yetu mengi. Ushirikishaji wa mtoaji wa mfumo wa teknolojia hiyo (STP) hautegemewi kuwa wa haraka kiasi cha kufikia kuanza kutumia teknolojia hiyo msimu ujao.

Hata ile kauli tu kwamba mitambo ya V.A.R itawekwa kwenye uwanja mmoja wa Benjamin Mkapa inaonyesha ni kwa kiasi gani nchi haiko tayari kuikumbatia teknolojia hiyo kama ilivyokuwa kwa matumizi ya waamuzi waamuzi watano ambao hadi sasa wameonekana katika mechi za Simba na Yanga tu, huku nyingine zikiendelea kuwa na uamuzi mbovu.

Maana yake, kama tukitumia V.A.R uwanja mmoja tu, tunaweza kujikuta miaka inaenda bila ya teknolojia hiyo kusambaa viwanja vingine. Ilifanyika hivyo kwa waamuzi watano na hadi leo hatuoni matumizi yao kwenye mechi zisizokutanisha wawili hao.

Kitu cha muhimu ilikuwa ni kuangalia vipaumbele vya nchi katika suala la uamuzi. Kwamba nini kiboreshwe ili kuimarisha usahihi katika uamuzi. Kama yule refa wa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) ya 2022, Papa Gassama alichezesha mechi baina ya wenyeji Cameroon na Misri kwa dakika 120 bila ya kuitwa kwenda kuangalia marudio ya tukio alilofanyia uamuzi, tunashindwaje kutengeneza kwanza waamuzi wa aina hiyo?

Maana yake inawezekana kabisa mechi zikachezeshwa kwa usahihi bila ya kutegemea teknolojia hiyo. Na hilo litakapowezekana, V.A.R itaingizwa kuongeza ufanisi katika usahihi wa uamuzi na si kuitegemea teknolojia hiyo ituletee ufanisi.

Kilicho dhahiri ni kwamba si teknolojia inayofanya maamuzi bali ni binadamu. Teknolojia inasaidia tu kutoa taarifa muhimu zitakazomuwezesha mwamuzi kufanya uamuzi kwa usahihi zaidi ya alivyoona kwa jicho la kwanza. Mwamuzi anaweza kuamua kuendelea na alichoamua kwanza au kubadilisha uamuzi wake baada ya kuangalia marudio au kumsikiliza mwamuzi msaidizi wa video.

Kwa hiyo badala ya TFF na Bodi ya Ligi (TPLB) kukuna vichwa kutafakari jinsi ya kuingiza teknolojia ya V.A.R, ni muhimu waangalie suala la ubora wa waamuzi wetu ambao sina shaka kwamba uko chini na ndio maana hawapati nafasi ya kwenda kuchezesha mashindano makubwa ya barani Afrika wala duniani na wanaachwa hata kwenye orodha za awali ambazo hutumika kupata waamuzi kama wa Afcon au hatua za juu za mashindano ya klabu Afrika au hata Kombe la Dunia.

Kipaumbele chetu kiwe kwanza ubora wa waamuzi, kwa kuboresha usahihi wao katika kutafsiri sheria dhidi ya matukio na mazingira, kasi yao uwanjani, uzoefu ambao hutokana na kuwa na muda mwingi kwenye kazi na mambo mengine muhimu.

Waingereza walikumbana na tatizo la uhaba wa rasilimali watu katika eneo la matumizi ya V.A.R wakati walipolazimika kutumia waamuzi walewale wa video kwa siku tatu mfululizo—Ijumaa, Jumamosi na Jumapili—na kuonyesha uchovu ulioathiri kazi zao na ndipo walipotangaza nafasi za uamuzi wa V.A.R kwa mwamuzi yeyote aliyepitia mafunzo ya urefa ili aongezewe stadi za teknolojia hiyo. Huku tuna rasilimali watu ya aina hiyo watakaoweza kusambaa kanda zote?

Kwa hiyo kipaumbele cha Tanzania kwa sasa si V.A.R bali rasilimali watu inayoweza kuendana na matumizi ya teknolojia hiyo, kwa kuwa mwishoni mwa siku binadamu ndiye anayefanya maamuzi ya mwisho na si kompyuta au runinga.

Related Posts