Kliniki inayotembea inavyowasaidia wenye VVU Uvinza

Uvinza. Upatikanaji wa huduma za kinga, tiba na matunzo kwa watu wanaoishi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) katika kitongoji cha Tandala, kata ya Uvinza, wilayani Uvinza na maeneo irani, kumetajwa kusaidia kupunguza gharama na muda waliokuwa wakitumia kufuata huduma hiyo awali.

Wakizungumza leo Jumatatu Juni 17, 2024 baadhi ya wapokea huduma hiyo wakati wa kliniki inayotembea inayoitwa ‘M-koba’ ambayo iko ndani ya mradi wa Afya Hatua, wamesema awali afya zao zilikuwa mbaya kutokana na kushindwa kupata dawa.

Mradi huo unatekelezwa na Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS) kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Ukimwi (PEPFAR) kupitia kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (CDC).

Mkazi wa kitongoji cha Tandala, Joshua Nzengo amesema awali walikuwa wanapata changamoto kusafiri umbali mrefu takribani kilomita 50 na kutumia gharama kubwa hadi makao makuu ya wilaya kufuata hospitali na kuchukua dawa pamoja na ushauri.

“Nauli kutoka hapa kwenda wilayani ni Sh10,000 kwa basi kwenda na kurudi, kwa wananchi kama sisi wa hali ya chini na tunaotegemea kilimo, ni ngumu kila wiki kwenda kufuata dawa.

“Kuna wakati unakaa nyumbani hadi mwezi mzima bila dawa na inasababisha afya inakuwa dhaifu, hivyo hatua hii ya kutusogezea huduma karibu imetusaidia sana,” amesema Nzengo.

Naye Joseph Kulwa, amesema mbali na gharama kuwa kubwa kufuata huduma hizo, walikuwa wakitumia takribani siku mzima kufuata huduma hizo.

“Tulikuwa tukitumia siku nzima kwenda mjini kufuata huduma na tukirudi tayari ni jioni, hatuwezi tena kufanya shughuli za kimaendeleo, hivyo kutusogezea huduma hiyo inaturahisishia kuchukua dawa na kwenda kuendelea na shughuli zetu za kila siku,” amesema Kulwa.

Muuguzi wa kitengo cha tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na maambukizi ya VVU kutoka kituo cha afya cha Uvinza, Said Hamis amesema kliniki hiyo inayotembea inatolewa mara mbili kwa mwezi na kwamba hadi sasa wana zaidi ya wapokea huduma 280 katika kituo hicho cha Tandala.

Amesema huduma hiyo ya Mkoba ilianza mwaka 2019 na tangu kuanzishwa imewarahisishia wapokea huduma kufika kwa wakati na kuchukua dawa bila kukosa kila tarehe ya kliniki, hatua iliyosaidia kuboresha afya zao na huku wakiendelea na majukumu yao ya kila siku bila kikwazo.

Meneja Mradi wa Afya Hatua kwa wilaya ya Uvinza, Dk Gabriel Max, amesema katika halmashauri hiyo wana vituo 16 vinavyotoa huduma ambazo ni pamoja na  tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na maambukizi ya VVU, upimaji, uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi, huduma ya kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, kinga na tohara.

Amesema wananchi wapo mbali na maeneo ya kupokelea huduma zao, kwa kutambua hilo kwa kushirikiana na Serikali walisogeza huduma hizo.

“Huduma hizi za  Mkoba zinatolewa kwa maeneo 36 kwa Uvinza na hazina tofauti na huduma zinazotolewa katika kituo cha afya, kwani wahudumu wanakuwa wale wale, dawa, vipimo na huduma ya ushauri, lengo ni kuwapunguzia umbali na gharama wapokea huduma,” amesema Max.

Related Posts