‘Watoto wa mitaani’ wafunguka wanavyotumikishwa kingono

Arusha. Watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani wamefichua jinsi jamii inavyowatumikisha kingono na kihalifu, hasa kwenye dawa ya kulevya bila kujali umri wao.

Wamesema jamii inayowazunguka imekuwa ikiwachukulia kama wahalifu au vyombo vya starehe na kutimiza haja zao, hivyo wameiomba Serikali kuwaokoa na janga hilo.

Watoto wamesema hayo leo Juni 17, 2024 jijini Arusha kwenye hafla ya makabidhiano ya nyumba maalumu kwa ajili ya uanzishaji wa kituo cha kuokoa watoto wanaoishi mitaaani kinachoendeshwa na Shirika la Amani Center for Street Children kwa ufadhili wa klabu ya Rotary ya Mjini Moshi.

Godfrey Solomon (16), amesema ameishi mitaani kwa zaidi ya miaka mitatu sasa na amekuwa akishuhudia changamoto lukuki, ikiwemo baadhi ya watoto wenzao waliowazidi umri kuwatumikisha wadogo kingono, jambo linalowaathiri kisaikolojia.

“Sio wenzetu tu wanaofanya, hata baadhi ya watu wazima wanakuja usiku tumelala, wanachukua wenzetu na kwenda kufanya nao hayo mambo na kuwarudisha, kitendo ambacho kimetuathiri sana kisaikolojia watoto tunaoishi mitaani,” amesema mtoto huyo.

Amesema katika kukabiliana na hayo, wengi wamekuwa watumiaji wa bidhaa zinazoweza kulevya kuondoa msongo wa mawazo kama bangi na dawa za kulevya.

“Wengine hutumia hata gundi na mafuta ya petroli ambayo hununua kwa fedha wanazopata kupitia ujira kidogo kwenye ubebaji wa mizigo mitaani au hata kuosha magari,” amesema mtoto huyo.

Kwa upande wake, Elia Mbise amesema changamoto nyingine inayowakabili ni kubebeshwa dawa za kulevya, hasa bangi na mirungi.

“Sisi tunaofanya kazi ya kubeba mizigo hasa kutoka stendi kuu huwa tunabebeshwa hadi dawa za kulevya bila kujua, kwani mtu anakushikisha mzigo umpelekee eneo atakalokuelekeza huku akikufuata nyuma, baadaye kwenye ukaguzi kama uko salama ndio unajua kumbe ulibeba dawa,” amesema Mbise.

Mtoto mwingine, Daniel Massawe (16) ameomba Serikali kuvisaidia vituo vinavyojitokeza kuwasaidia, ili kuwaokoa na majanga mbalimbali, ikiwemo vipigo vya mara kwa mara.

Kutokana na changamoto hizo, Mratibu wa Shirika la Amani Center, Naomi Kimaro amesema wameanzisha kituo cha kuokoa watoto hao wapate mahala pa kusemea shida zao na matamanio yao ya kimaisha, ili kupata msaada.

“Nyumba hii tuliofadhiliwa na klabu ya Rotary itakuwa kituo cha watoto hao kufikia muda wanaotaka kwa ajili kufua, kuoga, kula na tutatumia muda huo kuwasikiliza matatizo na changamoto wanazokumbana nazo na kuwapa ushauri wa kubadili fikra zao za kuishi mitaani,” amesema Naomi.

Amesema lengo la kufanya hivyo ni kuwashawishi watoto hao kurudi majumbani kwao kwa wale wenye wazazi au walezi lakini pia wasio na waangalizi wakubali kuishi kwenye vituo vya kuaalelewa.

Kwa upande wake, Mratibu wa Klabu ya Rotary, Aloyce Kimario amesema lengo la kufadhili nyumba hiyo ni kwa ajili ya kupunguza wimbi la watoto wanaoishi mitaani kwa mkoa wa Kilimanjaro na Arusha, ili kuwa na hatma ya Taifa salama la Tanzania baadaye.

Related Posts