Chama cha National Rally mguu sawa kuchukua hatamu – DW – 17.06.2024

Uchunguzi wa maoni tayari unaonesha chama hicho kinaweza kushinda lakini bila ya wingi wa kutosha wa kuunda serikali peke yake.

Siku ya Alhamisi mbunge mmoja wa chama hicho cha National Rally aliliambisha shirika la habari la Reuters kwamba kazi kubwa iliyofanywa  na Marine Le Pen katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita imekifanya chama hicho kuwa hivi kilivyo sasa na kuwa chama ambacho kinaweza kuwa serikalini.

 Laurent Jacobelli ameiambia Reuters kwamba wamekuwa kwa miezi sasa wakikifanyia kazi kile walichokiita,mpango wa kuingia Uongozini.

Hivi sasa chama hicho kinafanya majadiliano na wale wanaoweza kuwa washirika wao endapo wapiga kura wa Ufaransa wataamuwa kuwakabidhi nafasi ya kuliongoza taifa hilo baada ya uchaguzi wa mapema ulioitishwa na rais Emmanuel Macron.

Utafiti wa kura za maoni unaonesha chama hicho cha RN huenda kwa mara ya kwanza kikanyakuwa ushindi katika uchaguzi wa Juni 30 na ule wa Julai 7,ingawa  hakitoweza kupata ushindi wa moja kwa moja kuunda serikali peke yao.

Soma pia:Sarkozy asema kuvunjwa kwa bunge na kuitishwa uchaguzi wa mapema huenda kukazua vurugu Ufaransa

Uchaguzi mkuu wa Ufaransa wa mapema uliitishwa na rais Macron baada ya muungano wake wa mrengo wa kati  kushindwa vibaya na chama hicho cha MarineLe Pen,cha RN katika uchaguzi wa bunge la Umoja wa Ulaya.

Hatuwa ya Macron imeupinduwa juu chini mwelekeo wa kisiasa nchini Ufaransa huku vyama vikionesha kuhangaika kutafuta majina ya  wagombea watakaosimama kwenye uchaguzi pamoja na maandalizi.

Kwa chama hicho cha siasa kali za mrengo wa kulia kinachopinga wageni na chenye mashaka na Umoja wa Ulaya,changamoto yake kuwa ni kuubadili umaarufu wake huo kilichoupata katika uchaguzi wa Umoja wa Ulaya, kujipatia ushindi nyumbani na kuwashawishi wapiga kura kwamba kinaweza kuaminika kuiongoza Ufaransa baada ya miongo kadhaa ya kuwekwa pembeni.

Mpango wa kutwaa madaraka

Mbunge Jacobelli, ambaye pia ni msemaji wa chama hicho amesema sehemu ya mpango wao wa kutwaa madaraka waliokuwa muda wote wakiufanyia kazi unajumuisha hatua ya kujaza wagombea katika maeneo yote 577 ya uchaguzi.

Ufaransa | Siasa | National Rally
Viongozi na wafuasi wa chama cha mrengo mkali wa kulia cha nchini Ufaransa cha National Rally wakiwa katika mkutano wa hadharaPicha: Michel Euler/AP Photo/picture alliance

Na katika mkakati huu kuna chungunzima watakaotoka ngazi mbali mbali za chama cha kihafidhina cha Republican  ambacho kiko katika mkondo wa kuporomoka baada ya  kiongozi wake Eric Ciotti kutowa mwito wa  kuungana na RN. Sehemu ya Uongozi wa chama hicho ilikataa pendekezo hilo na kuamuwa kumtimua Ciotti.

Soma pia:Macron ataka wanasiasa kuungana dhidi ya misimamo mikali

Vyanzo kutoka chama hicho cha Le Republic vinatilia mashaka ikiwa Ciotii kweli anauwezo wa kuwavuta wagombea wengi wa chama hicho upande wake.

Jacobelli msemaji wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha RN anasema wanelenga kuwa na serikali ya Umoja wa Kitaifa  lakini ambayo itajumuisha tu vyama vya misimamo mikali  ya kihafidhina na wagombea wasiofungamana na vyama.

Imani ya Wafaransa kwa chama hicho

Ikumbukwe kwamba chama hicho kimekuwa nje ya Uongozi kwa miongo nchini Ufaransa na wapiga kura nchini humo wamekuwa wakikinyima nafasi hiyo kutokana na kutokuwa na imani na sera na misimamo ya chama hicho.

Lakini pia kutokana na mtindo uliokuwepo kwa miaka wa vyama vikubwa nchini humo wa kufikia maelewano na kuunganisha nguvu zao dhidi ya chama hicho.

Lakini chini ya juhudi za Le Pen na kiongozi mpya Jordan Bardella wameshirikiana kuifuta sura mbaya iliyokuwa ikikiandama chama chao na kuwavutia wapiga kura wengi kutoka matabaka mbali mbali ya taifa hilo.

Soma pia:Macron aitisha uchaguzi wa bunge baada ya kushindwa katika uchaguzi wa Umoja wa Ulaya

Chama cha RN kinataka kutanguliza sera za kuulinda uchumi wa Ufaransa na kupunguza kwa kiwango kikubwa uhamiaji. Kinataka malipo ya fedha za kusadia huduma ya watoto zitolewe kwa raia tu wa Ufaransa lakini pia kinataka kuondowa kibali cha ukaazi kwa wahamiaji ambao hawajawahi kufanya kazi kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Fahamu kuhusu uchaguzi wa Bunge la Ulaya

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Kundi jingine la vyama vilioko mbioni kujitafuta kuelekea uchaguzi wa Juni 30 ni vile vya mrengo wa kushoto ambavyo kwa muda mrefu vimegawika.

Viko kwenye mazungumzo ambayo baadhi yao wamesema ni mazungumzo makali ya kujaribu kukubaliana juu ya kuwa na jukwaa la pamoja na mpango wa kugawana maeneo ya kusimama kwenye  uchaguzi,zote zikiwa ni juhudi za kujaribu kuepuka kupoteza nafasi nyingi.

 

Related Posts