Mahakama Kuu ilivyowanusuru wavuvi waliofungwa kwa kukutwa hifadhini Rubondo

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Geita imewaondolea hatia wavuvi watatu ya adhabu ya kifungo gerezani baada ya kukiri makosa ya kuingia kijinai na kukutwa na nyavu haramu ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Rubondo.

Mahakama hiyo katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Griffin Mwakapeje Juni 14, 2024, imefikia uamuzi huo baada ya kukubaliana na hoja za rufaa waliyoikata wavuvi hao—Juma Magoma, Salmin Ramadhani na Mathias Thobias wakipinga hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Chato iliyowatia hatiani kwa kukiri kwao na kuwahukumu.

Wavuvi hao walishtakiwa kwa makosa mawili, kuingia kijinia katika Hifadhi ya Taifa ya Rubondo, kinyume cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Shtaka la pili lilikuwa ni kukutwa na nyavu zisizoruhusiwa aina ya timba (monofilament) ndani ya hifadhi hiyo, kinyume cha kanuni za uvuvi.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, wote walikiri, Mahakama iliwatia hatiani na kuwahukumu adhabu ya kifungo cha miezi minne na faini ya Sh2 milioni kwa kila mmoja au kifungo cha miaka mitatu jela wakishindwa kulipa faini hiyo kwa kila kosa.

Hata hivyo, walikata rufaa Mahakama Kuu kupinga hatia na adhabu hiyo, huku wakiwasilisha jumla ya sababu nne za rufaa.

Katika sababu hizo, pamoja na hoja nyingine waliibua madai ya kasoro za kisheria za hati ya mashtaka na za mwenendo wa kesi, hoja kubwa katika sababu ya kwanza kuwa Mahakama ya Wilaya ilikosea kuwatia hatiani kwa kuzingatia kukiri kwao ambako hakukuwa dhahiri.

Mahakama Kuu baada ya kusikiliza hoja za sababu hizo za rufaa na kutoka kwa wakili wa warufani hao, Charles Kiteja na za upande wa mjibu rufaa, Jamhuri iliyowakilishwa na Wakili wa Serikali, Godfrey Odupoy, Mahakama hiyo imekubaliana na hoja rufaa hiyo.

Pia Jaji Mwakapeje amesema kuwa maelezo ya shtaka hilo hayabainishi viini vya kosa la kuingia kijinai.

Hivyo, amesema kukiri kwa washtakiwa kwa kosa kama hilo hakuwezi kuwa kukiri kuliko dhahiri, kwa kuwa hakukukidhi vigezo vya kukiri kosa kuliko dhahiri vilivyowekwa na Mahakama Kuu katika uamuzi wa kesi mbalimbali na kuthitibishwa na Mahakama ya Rufani.

Vilevile Jaji Mwakapeje amesema ushahidi katika kesi za washtakiwa kukiri kosa, sharti uonyeshe mipaka kisheria ya maeneo yaliyohifadhiwa walimokuwa warufani isivyo halali na kwamba hilo lingethibitisha kuwa walikuwa ndani ya mipaka ya hifadhi hiyo, lakini katika kesi hiyo ushahidi huo haupo.

“Zaidi kwa kuzingatia kukiri kosa kwa warufani yaani ‘ni kweli sikuwa na kibali hifadhini” hakuhusiani na kukiri kosa la kuingia kijinai ambalo walishtakiwa nalo, badala yake kunahusiana na kukutwa ndani ya hifadhi bila kuwa na kibali cha Kamishna wa Uhifadhi chini ya Sheria ya Hifadhi za Taifa,” amesema Jaji Mwakapeje na kuongeza:

“Ni bahati mbaya kwamba sheria hiyo (ya Hifadhi za Taifa) ambayo ni maalumu kwa uhifadhi, haina kosa hilo.”

Amesema kwa kuwa upande wa mashtaka uliamua kutumia Sheria ya Kanuni ya Adhabu, basi mashtaka na maelezo ya kosa la kuingia kijinai katika hifadhi hiyo yangewawezesha warufani kujua asili ya makosa waliyoshtakiwa nayo kwa mujibu wa kifungu cha 132 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai.

Kuhusu kukiri kwa washtakiwa/warufani hao katika shtaka la pili, Jaji Mwakapeje amesema kuwa kile walichokikiri washtakiwa kilikuwa ni tofauti na maelezo waliyosomewa washtakiwa ambayo ni tofauti na shtaka.

“Kutokana na sababu hizo na kwa kuwa kukiri kosa kwa warufani (washtakiwa) katika rufaa hii hakukukidhi masharti yaliyowekwa katika kesi ya Michael (Michael Adrian Chaki dhidi ya Jamhuri, rufaa ya jinai namba 399/2019), ninaona mashiko katika rufaa hii”, amesema Jaji Mwakapeje na kuhitimisha:

“Ninaikubali (rufaa) na ninatengua hatia na kufuta adhabu iliyotolewa dhidi ya warufani. Zaidi ninaamuru kuachiliwa haraka kwa warufani hawa kutoka gerezani isipokuwa kama wataendelea kushikiliwa kwa sababu nyingine halali.”

Related Posts