MISIMU mitatu ya kiraka, Farid Mussa ndani ya Yanga ameitaja kuwa ni ya mafanikio kwake baada ya kutwaa mataji matatu ya Ligi Kuu Bara, na mataji mawili ya ngao ya jamii huku akicheza hatua ya fainali Kombe la Shirikisho Afrika.
Kiraka huyo amefunguka mambo mbalimbali akizungumza na Mwanaspoti, huku akitaja mchezo wa fainali Kombe la Shirikisho Afrika; “Hakuna tukio baya nimekutana nalo kama la msimu uliopita tukicheza mchezo wa fainali na kushindwa kutwaa taji kwa changamoto ya bao la nyumbani na ugenini mchezo wa kwanza tukiwa nyumbani dhidi ya USM Alger tulifungwa mabao 2-1 kwenye mchezo wa kwanza, kwani pamoja na sare ya jumla ya 2-2, lakini wamefaidika na mabao ya ugenini.”
“Hakuna kitu kiliniuma kama hicho kwani ugenini na sisi tulipata ushindi wa bao 1-0 na ndio ulikuwa mchezo wa kuamua lakini haikuwa siku njema kwetu kwani ubingwa walipewa USM Alger hiki kitu sitakaa nikakisahau maisha yangu yote japo nimebakiwa na kumbukumbu ya medali.”
“Sio kwamba Yanga walinipa fedha kubwa nilivyoamua kusajiliwa hapo hapana niliangalia nafasi yangu na malengo yangu ya kutwaa mataji ambayo yatanijengea historia na heshima miaka ijayo hata ukimuangalia Cristiano Ronaldo anavyohama hama timu sio kwamba anaangalia fedha tu hapana hata mataji pia,” anasema na kuongeza;
“Nimecheza Yanga kwa mafanikio nimevaa medali za mataji ya ndani pia nimevaa medali ya Kombe la Shirikisho la Afrika ambayo hata nikizeeka nina kitu cha kumuonyesha mwanangu kwa ushahidi sio kumsimulia tu kuwa nimecheza timu fulani na fulani bila ya ushahidi wa medali.” Amesema.
Hakushtukizwa hiyo ni kauli ya Farid aklisimulia namna alivyopata nafasi ya kucheza kikosi cha wakubwa akiwa Azam FC mchezo dhidi ya Yanga ‘’Ulikuwa usiku bosi Yusuf alikuwa na kocha Kali Ongala walikuja kambini wiki moja kabla ya mchezo kutuambia kuwa tutacheza mechi inayofuata.
“Mechi yangu ya kwanza nikicheza kutoka timu ya vijana nilicheza dhidi ya Yanga nakumbuka nilitumika kwa dakika 80 nilitoka aliingia Kimwaga alifunga bao la tatu,” amesema na kuongeza;
“Tulishinda tukaitwa kusainishwa mkataba nakumbuka nilipewa mkataba wa Milioni saba na mshahara Sh. 600000 niliona hiyo ni kubwa kwani nilikuwa sijawahi kushika hiyo fedha ndefu kama hiyo tangu nimeasha kucheza soka.” anasema.
CHAMA. LUIS WALIVYOZUIA DILI LAKE SIMBA
Baada ya kucheza kwa misimu minne nchini Hispania, Farid alirudi nchini na wengi wakiwa na matarajio ya kumuona akirudi huko kwenda kupambana kama ilivyo kwa Himid Mao ambaye tangu ametoka Azam FC amekuwa akipambana nje ya nchi mwenyewe anafunguka sababu.
“Sikurudi nje kwasababu ya janga la Covid-19 kwani nilikuwa na ofa nyingi nje ya nchi lakini niliona nikisubiri changomoto hiyo iishe ndio nicheze mpira ningerudi nyuma kiushindani na ndipo nilipoamua kufanya uamuzi wa kurudi Tanzania. Nilipofanya uamuzi wa kurudi na kucheza Ligi Kuu Bara 2020 nilipokea ofa nyingi kutoka timu mbalimbali wakiwemo Azam FC, Simba na Yanga ndipo niliamua kuomba ushauri kwa nahodha Mbwana Sammata ambaye alinipeleka Yanga.”
Farid anasema alishauriwa na Samata kutua Yanga baada ya kuambiwa kuwa timu hiyo ndio inatengenezwa licha ya kupitia mambo magumu kwa kupitisha mabakuli kwa wanachama ndio kwanza wanajitafuta tofauti na Simba.
“Nakumbuka kipindi hicho Simba ni ya moto ipo kwenye ubora ina Luis Miquisone, Clatous Chama akaniambia hapo sitaweza kupata nafasi ya kucheza kwani wawili hao tayari walikuwa wamejitengenezea ufalme huku akiniambia Azam FC nitapokelewa kwa mazoea kwasababu ni timu ambayo nimewahi kuicheza.
“Ndipo nilipoamua kucheza Yanga ambayo kulikuwa na Ditram Nchimbi eneo langu hivyo nikaona bora nijitafute huko hadi sasa naendelea kuitumikia timu hii ambayo ni moja ya timu ambayo nitacheza misimu mingi kwani Hispania nilitumika misimu minne tu,”anaongeza.
KUTOKA POSHO BUKU HADI MAMILIONI
Anakiri kuwa ametoka kupokea posho buku au kukosa kabisa hadi kulipwa laki sita au Milioni kadhaa
“Saizi maisha yamebadilika Farid ambaye alikuwa anapewa posho elfu moja sasa anazungumza fedha ndefu kuanzia mshahara hadi posho za mechi hivyo maisha yanabadilika pia na umri unakwenda sambamba na vipaji kukua.”
TSHABALALA, MSUVA KUIGOMEA AZAM
Farid anasema amecheza sambamba na Mohammed Husein ‘Tshabalala’ Saimon Msuva ambao ameweka wazi kuwa ni mastaa ambao walishindwa kubaki baada ya kupewa nafasi ya kuchagua kuendelea kucheza timu ya vijana au kutoka ndani ya timu hiyo.
“Unajua tulifikia wakati tulikuwa tunaona tayari tuna uwezo wa kucheza timu ya wakubwa lakini nafasi ya kupandishwa ilichelewa hivyo nafasi ya kuchagua kubaki au kuondoka ni Msuva, Tshabalala tu kati ya wachezaji waliotoka Azam FC ndio wana mafanikio,” anasema na kuongeza;
“Kocha Stewart Hall alikuwa hana mpango wa kutumia vijana ndipo Tshabalala akaamua kwenda Kagera Sugar huku Msuva akikimbilia Moro United hao ndio wameweza kuwa bora lakini wengine wamepotea kwenye ramani ya mpira sio vizuri kuwaweka wazi lakini ni wengi walichagua kuondoka.”
SURE BOY ALIVYOMPA NAMBA AZAM
Baada ya kupewa mkataba wa timu kubwa alipata majeraha yaliyomuweka nje kwa miezi sita na timu hiyo ilifanya usajili wa Ramadhan Singano ‘Messi’ ambaye kipindi hicho alikuwa kwenye ubora.
“Baada ya usajili huo nakumbuka niliona mambo yangu yanakuwa magumu kwasababu nimetoka majeraha na kaletewa mshindani bora, ilifikia mahali walitaka kunipeleka kwa mkopo Coastal Union,” anasema na kuongeza;
“Lakini mambo yalibadilika baada ya kurudi Azam FC kwaajili ya maandalizi ya msimu mpya, michuano ya Kagame Cup ambayo tulitwaa taji bila kufungwa kikosi kikiwa ni Pascal Wawa, Agrey Moris, Said Mweda, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Gadiel Michael kocha Stewart hii ni Azam ambayo imetoka kutwaa ubingwa, ulifanyika usajili wa Ibrahim Majwega, Singano, Brian Omony’s, Ame Ally, John Bocco, Kipre Tcheche, Frank Domayo, Himid Mao timu ilikuwa imekamilika kati ya wachezaji 30 kama sijakosea au 28 walikuwa wanatakiwa 20 tu.”
Farid anasema kwenye nafasi ya yake huku kocha wake akitumia mfumo wa 3-5-2 waliokuwa wanatumia mguu wa kushoto kulikuwa na yeye mwenyewe, Singano, Gadiel, Majwega wakati mwingine Nyoni alikuwa anacheza nafasi hiyo kama Mwantika hatacheza nafasi ya mabeki watatu nyumba.
“Niliweka malengo kuwa nitatoka kwa mkopo nikawa nimewekeza nguvu za kujiweka fiti ili hata nikitua Coastal Union niwe bora lakini sikujua Mungu kaniandikia nini nikawa najituma sana mazoezini wakati mwingine kwakua nilikuwa naishi hapohapo Chamazi nikawa najihimu kuamka mapema kujiweka fiti,” anasema na kuongeza;
“Kipindi hicho Messi hakuanza kucheza moja kwa moja kutokana na kesi yake na Simba kuhusu usajili hivyo nafasi yangu nilibaki mimi, Erasto na Gadiel hivyo kwenye kucheza walitakiwa wavae wachezaji 18 kati ya 20, 11 wanacheza saba benchi mechi ya kwanza nilikaa juu mimi na kipa mechi ilikuwa dhidi ya KCCA tulishinda bao 1-0.”
“Kwenye mchezo huo aliumia Sure Boy na aliibuka kuwa mchezaji bora wa mechi hivyo kuumia kwake ikabidi yeye akae jukwaani mimi nishuke kucheza mchezo wa pili huo alianzishwa Gadiel mimi nilianzia benchi kocha hakumuelewa kipindi cha pili niliingia mimi nilicheza vizuri tulishinda mechi ya tatu nilianza na kupewa mchezaji bora wa mchezo nilipewa king’amuzi na hiyo ndio ikawa safari ya kwenda Coastal ikafa.”
Anasema kwenye hayo mashindano robo fainali waliwatoa Yanga kwa penati kwenye mechi ya nusu walicheza na KCCA akafunga bao na kuipeleka Azam FC fainali na kwenda kucheza na Gor Mahia.
Farid anasema kama sio soka angekuwa bodaboda. “Kwa namna nilivyopambana hadi nimefika hapa nimekwepa mishale mingi sana nimepambana nimevuka mito na mabonde maana nimetoka Mkoa hadi nikachaguliwa Copa Cocacola (2011), timu ya taifa ya vijana, Azam B nilitwaa nayo ubingwa wa Uhai Cup (2012) hadi kupandishwa na kutwaa taji la Ligi Kuu.”
“Ningekata tamaa kama baadhi ya wachezaji ambao siwezi kuwaweka wazi kwa majina basi naamini ningekuwa bodaboda kwani shule sikuizingatia kabisa zaidi ya kuwekeza muda mwingi kwenye soka.”
“Baada ya kusainishwa zile Milioni saba za kwanza za usajili nilinunua simu kipindi hicho Huawei ndio zipo sokoni nikanunua aina ya P Seven ilikuwa inapiga picha nzuri na fedha nyingine nilinunua eneo kijijini kwetu Kibosho na kumjengea mama yangu nyumba,”
“Najua mimi nakua mzazi lazima awe na sehemu ya kukaa mimi bado nakua naweza nikapanga hivyo nilianza ujenzi ambao sikuukamilisha moja kwa moja kila mwisho wa mwezi mshahara wangu nilikuwa nahakikisha nawekeza kumalizia nyumba.”
ESPERANCE ILIVYOMPELEKA HISPANIA
‘’Nakumbuka mechi iliyonika nafasi ya kwenda kucheza nje ni dhidi ya Esperance hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho Afrika hii timu ilikuwa inanifuatilia lakini mchezo huo walikuja Chamazi kuniangalia,” anasema na kuongeza;
“Nakumbuka nilifunga bao la kwanza na kuseti la pili lililofungwa na Ramadhani Singano ‘Messi’ katika mchezo wa kwanza Dar es Salaam Azam FC tulikuwa nyuma kwa bao 1-0 na kushinda 2-1 hapo ndio safari yangu ilianza.” Anasema.
Anasema changamoto ya yeye kuondoka ilikuwa kubwa baada ya waajiri wake wa zamani Azam FC wakimtaka kumaliza msimu hadi hapo viongozi wa Serikali kuingilia kati na kumruhusu yeye kuondoka.
“Katika siku ambayo nilitamani kuacha mpira ni siku ambayo ngao ya jamii mechi kati ya Simba na Yanga nilikuwa mimi na kipa nilipokea pasi kutoka kwa Michael Sarpong nilikosa lakini nilichukua kama sehemu ya mpira tu kwasababu hata Ulaya mastaa wanakosa,” anasema na kuongeza;
“Hilo lilipita nafikiri matukio yalifuatana tulikuwa na mechi dhidi ya Coastal Union Tanga, pia ilitokea changamoto kama hiyo mimi na kipa nilikosa siku hiyo niliingia chumbani moja kwa moja hadi hamu ya kula ilikata nakumbuka sikutaka kuongea na mtu yeyote, Rais Hersi Said alinitafuta na kunifuata nilipo akaniambia ni sehemu ya maisha ya mpira sitakiwi kukata tamaa huyo ndio akanirudisha mchezoni lakini nilikuwa tayari nimekata tamaa kutokana na maeno ya mashabiki.”
Anasema baada ya kukosa bao dhidi ya Coastal Union licha ya kutulizwa na Hersi alimfuata Kocha Kaze na kumuambia hataki kupangwa mechi inayofuata akikiri kuwa akili yake haikuwa sawa kutokana na presha ya mashabiki.
“Mpira ni akili na kama kichwa hakipo sawa huwezi kuwa bora kiwanjani nakumbuka mchezo niliomba kukaa jukwaani sijui ilikuwa dhidi ya Polisi Tanzania tulitoka sare ya bao 1-1 mashabiki wakaanza kupiga mawe hiyo ndio ilikuwa safari ya kutimuliwa Kaze.”
“Nabi alikuwa ananipanga mazoezini nafasi mbalimbali na kunisifu kuwa nina uwezo wa kucheza nafasi nyingi uwanjani akaanza kunitumia kiungo mshambuliaji, beki zote mbili kulia na kushoto muda mwingine winga wa kulia na kushoto msimu ambao ndio alikuwa anamalizia akikabidhiwa mikoba ya Kaze.”
“Msimu uliofuata sasa niliingia kwenye mfumo wake nikipata nafasi ya kucheza mara kwa mara akinipanga kwenye nafasi anayojisikia yeye kuna mechi nakumbuka nilicheza namba sita kipindi hicho Khalid Aucho alikuwa bado hajapata kibari cha kucheza ulikuwa mchezo dhidi ya Geita Gold kwa Mkapa na nilitumika kwa dakika 75.” Anasema.
Farid anasema maisha ndani ya kikosi cha Nabi yalikuwa bora kwake kwani alikuwa na nafasi ya kujijenga kisoka kwa kucheza nafasi nyingi uwanjani kitu ambacho kwake kimemjenga kuwa mchezaji wa kutumainiwa kwenye nafasi nyingi.
AFICHUA SIRI ZA PIERRE YANGA
Wakati kiraka Farid akiwachambua makocha Naseddine Nabi na Miguel Gamondi aina ya ufundishaji wao na upangaji wa kikosi kuwa ni tofauti ameibua mpya kutoka kwa kocha Raoul Pierre.
“Nabi kikosi chake kilikuwa kinatambulika siku tatu kabla ya mchezo kutokana na kuandaa mchezaji kwa kumuambia mechi ijayo utachea lakini kwa upande wa Gamondi ni sapraizi kwani anatufanyisha mazoezi pamoja na siku ya mchezo ukipewa nafasi utatakiwa kucheza lakini kuna yule kocha alikuwa anaitwa Pierre yule kiboko,” anasema na kuongeza;
“Timu ina wachezaji 28 alikuwa anafanya mazoezi na wachezaji 14 pekee hao ndio ambao anatarajia kuwatumia mechi iliyo mbele yake huyo kocha nakumbuka alikuwa ni mkuu baada ya kutimliwa ndio alikuza Cedrick Kaze.”
Anasema chini ya Pierre ambao walikuwa hawapo kwenye mpango walikuwa wanafanya mazoezi wao wenyewe na wakitambua hawapo kwenye mpango basi walikuwa wanatimka kwenda majumbani mwao.
“Kocha huyo alikuwa anapenda mfumo wake ambao Carlos Fernandes ‘Carlinhos’ anachonga kona wengine wanaruka vichwa kati ili kufunga, huyo kocha alikuwa anapenda sana wachezaji wenye miili mikubwa kama Lamine Moro.” Anasema.
“Kwa wachezaji wote waliopita Yanga msimu wa 2022/23 walikuwa bora sana bila kuchagua nani na nani nafurahia kufanya kazi na wachezaji ambao walikuwa na uchu wa mafanikio, Mayele alikuwa mchezaji ambaye alikuwa ni mcheshi na mtu wa masihala sana,” anasema na kuongeza;
“Pia Jesus Moloko, Yanick Bangala, Djuma Shaban ni wachezaji wote ambao walikuwa wapambanaji utofauti ni aina ya maisha waliyokuwa wanaishi kama Bangala hakuwa mtu wa masihara yeye alikuwa makini kwenye majukumu ya kazi muda mwingine anakuwa bize na mambo yake.”
“Aucho ni mchezaji mzuri na sio mchezaji wa mambo mengi yeye yupo makini na kazi yake kuliko kitu kingine chochote sio mtu wa masihara ni mchezaji kiongozi na muhimili wa timu anakila sifa za kuwa koingozi.” Amesema Farid ambaye amebainisha kuwa kwenye masuala la kupika yupo vizuri akiweza kugonga ugali na kupika aina mbalimbali za mboga kama samaki, makange ya kuku.
Djigui Diarra hakuna ubishi ni kipa ambaye amefanya kazi kubwa msimu huu akiisaidia timu kutwaa taji, Yao, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Dickson Job, Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Khalid Aucho, Maxi Nzengeli, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Wazir Junior, Stephane Aziz Ki na Feisal Salum ‘Fei Toto’.