Celtics bingwa, rekodi tamu NBA

Boston Celtics ya Ukanda wa Mashariki imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya NBA, baada ya ushindi wa vikapu 106-88 dhidi ya Dallas Mavericks ya Magharibi, juzi Jumanne.

Ushindi huo umefanya matokeo ya jumla kuwa 4-1 baada ya mechi tano za katika fainali hiyo, tofauti na wengi walioamini itafikisha mechi saba kupata bingwa.

Awali Jayson Tatum baada ya kufunga na Dallas mchezo wa nne ugenini alisema ni bora zaidi kucheza mchezo wa kuamua nyumbani kwenye Uwanja wa TD Garden na alionyesha alichokisema kwa kuiongoza Celtics kushinda mchezo huo wa tano kwa kufunga pointi 31, asisti 11 na ribaundi nane, huku nyota mwenzake Jaylen Brown akifunga pointi 21, ribaundi nane na asisti sita.

Upande wa Dallas, ilishindwa tena kufua dafu mbele ya Celtics kwenye ulinzi kutokana na ubora mkubwa wa wapinzani wao hao na kuonekana wazi wameelemewa na mchezo huo.

Luka Doncic alifunga pointi 28, ribaundi 12 na asisti tano wakati nyota mwenzake Kyrie Irving akifunga pointi 15 pekee.

Kutokana na ubora wa nyota wawili, Tatum na Jaylen Brown, mashabiki wamejikuta wakigawanyika kuhusu tuzo ya mchezaji bora wa mchezo wa fainali (MVP, kabla ya mwishowe kuamuliwa.

Ni Brown aliyebeba tuzo hiyo licha ya mchezo mzuri alioonyesha Tatum kwenye mchezo huo wa tano na kusababisha mashabiki kuimba jina lake.

Hata hivyo, ubora wa Brown kwenye mechi tatu za awali walizoshinda ikiwamo ile ya tatu ya ugenini uliowavuruga Dallas ndiyo iliyombeba na kunyakua tuzo hiyo ikiwa ni ya pili kwenye fainali baada ya kushinda ya Ukanda wa Mashariki walipoichapa Indiana Pacers 4-0.

Ushindi wa Celtic umeifanya kuweka rekodi ya kufikisha mataji 18 ya Ligi ya NBA na kuwa kinara ikiiacha Los Angeles Lakers ikiwa na 17.

Mara ya mwisho Celtics kushinda taji hilo ni mwaka 2008 na ilisubiri kwa miaka 16, huku mwaka 2022 ikijaribu kufanya hivyo lakini ikaangukia pua mbele ya Golden State Warriors.

Joe Mazula, kocha aliyepewa timu hiyo miaka miwili iliyopita akichukua mikoba ya Ime Udoka, ameifanya Celtics kuwa tishio kwa misimu yote miwili na kubeba taji hili, ikichagizwa na ubora kuanzia kwenye ligi ndefu.

Related Posts