Rombo. Kijana, Erasmi Johnbosco (23), Mkazi wa kitongoji cha Moru, Kijiji cha Lessoroma, Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro anadaiwa kuuawa kwa kuchomwa na kisu sehemu ya kifuani na kijana mwenzake baada ya kumhoji ni kwanini amemwaga bia ya Sh1,800 wakati wenzake wana kiu ya kinywaji hicho.
Tukio hilo, lilitokea jana Juni 17, 2024 ,muda wa jioni katika moja ya duka la vinywaji lililopo kitongoji hicho na kuzua taharuki kwa wananchi.
Hata hivyo, baada ya kutokea mauaji hayo, kundi la vijana waliokuwa wamebeba mawe walivamia makazi ya watu ikiwemo nyumbani kwa familia ya kijana anayetuhumia kwa mauaji.
Imeelezwa kundi hilo walianza na kurusha mawe juu ya bati na kusababisha baadhi ya watu kupata usumbufu.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema tukio hilo limetokea jana na mtuhumiwa wa mauaji hayo alikimbilia nchi jirani ya Kenya.
Kamanda Maigwa amesema jeshi hilo kwa kushirikiana na maofisa wa nchi hiyo, wanaendelea kumtafuta mtuhumiwa ili hatua za kisheria zichukuliwe.
“Huyu kijana alichomwa sehemu ya kifuani na kitu chenye ncha kali na kijana mwenzake waliokuwa wote na alikimbizwa hospitali kwa haraka kwenye matibabu na wakati anaendelea na matibabu alifariki dunia,” amesema.
“Mtuhumiwa amekimbilia nchi jirani ya Kenya lakini Maofisa wetu kwa kushirikiana na upande mwingine, tunaendelea kumtafuta mtuhumiwa na tutakapomkamata tutamfikisha kwenye vyombo vya sheria,” amesema Kamanda Maigwa.
Akizungumza mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Evord Bernadi amesema wakati mtuhumiwa akiwa na huyo kijana aliyefariki dunia kwenye moja ya duka lililopo kwenye kitongoji hicho, Erasmi (marehemu) alipoona mwenzake amemwaga bia ya mwenzake aliyekuwa amekaa naye alimuuliza kwanini anamwaga pombe wakati wenzake wana kiu na ndipo ugomvi ulipoanza.
“Huyu aliyemchoma kisu Erasmi, alikuwa na mwenzake dukani wamekaa wanakunywa pombe, wakati wamekaa mtuhumiwa alimwaga bia ya mwenzake, marehemu akamuuliza mbona unamwaga pombe wakati wenzako wanakiu? Na sisi hatujanywa pombe? Ndipo alipochukua kisu alichokuwa nacho na kumchoma nacho kifuani, akawa ameanguka chini,” amefafanua.
Amesema walipomchukua na kumkimbiza katika Kituo cha Afya cha Karume kilichopo kijijini hapo walikuta tayari ameshafariki dunia na hivyo mwili wake umehifadhiwa hospitalini hapo kwa ajili ya taratibu za maziko.
Mtendaji wa Kijiji hicho, Emma Moshi amesema tukio hilo limewahusisha vijana hao wakiwa eneo la kitongoji hicho na kwamba awali kuliibuka ugomvi ambao ulisababisha mauaji hayo.
“Tukio hili lilitokea saa 11 jioni na inavyosemekana ni kwamba huyu mtuhumiwa baada ya kufanya mauaji hayo, alikuwa anatembea na kisu barabarani akisema ameua na kutishia watu amani kwenye eneo hilo,” amesema.
Amesema baada ya kutokea tukio hilo kundi la watu wenye hasira kali wakiwa wamebeba mawe walikwenda kwenye nyumba aliyokuwa akiishi mtuhumiwa huyo na kufanya uharibifu pamoja kupiga mawe kwenye baadhi ya nyumba zilizopo maeneo ya jirani.
“Watu walikwenda nyumbani kwa huyu mtuhumiwa kumtafuta, walipomkosa walivunja nyumba yake vyoo pamoja na kupiga mawe kwenye baadhi ya nyumba jirani na familia hiyo,” amesema mtendaji huyo.
Pamoja na mambo mengine, mtendaji huyo amesema changamoto kubwa ambayo ipo kijijini hapo ni kwamba vijana wamejiingiza kwenye ulevi wa kupindukia pamoja na uvutaji wa bangi na mirungi na kwamba imekuwa ni tushio kubwa kwenye maeneo hayo