Rais Samia kwenda Afrika Kusini kushiriki uapisho wa Ramaphosa

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anatarajia kuondoka nchini jioni ya leo Jumanne Juni 18, 2024 kwenda Afrika Kusini kwa ziara ya kikazi ya siku moja kwa ajili ya kushiriki hafla ya uapisho wa Rais Mteule, Cyril Ramaphosa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Ofisi ya Rais Ikulu, Rais Samia atashiriki hafla hiyo itakayofanyika kesho Jumatano Juni 19, 2024 baada ya Ramaphosa kuchaguliwa tena kuwa Rais wa nchi hiyo.

Ramaphosa alichaguliwa tena kuwa Rais wa Afrika Kusini na Bunge la nchi hiyo Ijumaa ya Juni 14, 2024 kufuatia makubaliano kati ya chama tawala cha African National Congress (ANC) na vyama vya upinzani.

ANC ililazimika kuingia makubaliano na vyama hivyo kikiwamo Chama cha Democratic Alliance (DA) na vyama vidogo kama  Inkhata Freedom Party, baada ya kushindwa kufikisha asilimia 50 ya kura.

Katika uchaguzi wa Mei 29, 2024 ANC ilipoteza idadi ya viti katika Bunge la nchi hiyo baada ya miaka 30 ya uongozi wake katika taifa hilo.

Ramaphosa ataendelea kuwa Rais katika muungano huo, huku nafasi nyingine zikiendelea kujadiliwa.

Katika uchaguzi huo, ANC ilipata asilimia 40.2 ya kura, wakati DA ikishika nafasi ya pili kwa asilimia 22, huku vyama vingine kama Umkhonto weSizwe kikipata asilimia 15 na Economic Freedom Fighters asilimia 9.5.

Related Posts