Serikali ya Ruto yalegeza msimamo, mswada wa fedha 2024 – DW – 18.06.2024

Hata hivyo mswada huo umetengewa siku ya Alhamisi kujadiliwa na kupata ridhaa bungeni.Wakati huohuo, purukushani zimeshuhudiwa kutwa nzima katikati ya jiji kuu kuupinga mswada wa fedha wa 2024.

Mchana huu wa siku ya Jumanne, umeshuhudia hali ya mshike mshike katikati ya jiji la Nairobi pale waandamanaji walipokusanyika na kuvurugana na maafisa wa usalama. 

Dhamira ya waandamanaji hao ni kuwashinikiza wabunge waliokuwa kikaoni kujadili mswada wa fedha wa 2024 kuutulipilia mbali kwani unamkaba koo mwananchi wa kawaida.

Soma pia: Wanaharakati nchini Kenya wapinga ongezeko jipya la kodi

Muda mfupi kabla ya bunge kuanza kikao, viongozi wa chama tawala wakiongozwa na rais William Ruto walifanya mkutano wao ikulu na kutangaza kuwa wamelegeza kamba na baadhi ya mapendekezo ya kodi mpya yametatuliwa mbali.

Akihutubia waandishi wa habari, mbunge wa Molo Kuria Kimani, ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya bunge ya fedha, akiandamana na rais Ruto na viongozi wa Kenya Kwanza alibainisha kuwa wamekisikiliza kilio cha wakenya na kufanya mabadiliko kwenye orodha ya mapendekezo ya kodi mpya zinazozonuwia kufadhili bajeti ya mwaka 2024/25.

Kodi hizo mpya zilizoangaziwa kuondolewa ni pamoja na ile ya mkate, usafirishaji wa sukari, huduma za fedha na kuhamisha hela, kodi ya kutumia magari, bidhaa zinazotengezwa nchini mfano sodo, vibinda, matairi, simu na pikipiki kadhalika bima ya afya na mchango wa hazina ya ujenzi wa nyumba.

Soma pia: Bunge la Kenya lapitisha muswada tata wa fedha

Kwa mujibu wa kiongozi wa chama tawala bungeni Kimani Ichungwah, mswada huo unawasilishwa bungeni leo na mjadala kuanza kesho kabla ya kupigiwa kura ya idhini siku ya Alhamisi. Jee, tamko la leo lina uzito gani? 

Tamko la Jumanne limezua hisia mseto. Reuben Kiborek ni mbunge wa Mogotio na ameisifia serikali ya Kenya Kwanza kwa kusikiliza kilio cha mwananchi.

Polisi walitumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji mjini Nairobi. (Picha ya maktaba)
Polisi walitumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji mjini Nairobi. (Picha ya maktaba)Picha: Thomas Mukoya/REUTERS

Yote hayo yakiendelea, mamlaka ya kukusanya ushuru na kodi nchini Kenya, KRA, ina kibarua kigumu mbele yake kukusanya shilingi bilioni 567 kwa mwezi huu wa Juni ili kutimiza malengo yake ya mwaka wa fedha.

Ijapokuwa kiwango cha pato la kodi kimeongezeka kwa asilimia 9.5 kwa mwezi wa Mei mwaka 2024, mamlaka ya KRA haijawahi kukusanya shilingi bilioni 567 katika kipindi cha mwezi.

Ifahamike kuwa katika kipindi cha miezi 8 ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2023/4 mamlaka ya KRA ilikusanya shilingi bilioni 171.7 pekee kwa mwezi.

Related Posts