Majadiliano Jatu, DPP bado yaendelea

Dar es Salaam. Serikali imesema bado haijafikia tamati katika majadiliano ya kuimaliza kesi baina yake na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Jatu PLC, Peter Gasaya.

Gasaya (33), anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi akishtakiwa kwa mashitaka mawili, likiwamo la kujipatia Sh5.1 bilioni kwa njia ya udanganyifu.

Wakili wa Serikali, Eric Davies ameieleza  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Juni 18, 2024 kesi ilipoitwa kwa ajili ya kujua hatua iliyofikiwa katika vikao vya majadiliano baina ya DPP na mshtakiwa.

Gasaya anadaiwa kujipatia fedha hizo kutoka Saccos ya Jatu kwa madai ya kuzipanda kwenye kilimo cha mazao ili kuzalisha faida zaidi, wakati akijua ni uongo.

Wakili Davies ametoa maelezo hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mhini anayesikiliza shauri hilo.

“Upande wa mashitaka bado tunaendelea na vikao vya majadiliano na mshtakiwa, hatujafikia tamati, hivyo tunaomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea na vikao,” amedai mahakamani hapo.

Baada ya maelezo hayo, wakili wa mshtakiwa, Nafikile Mwamboma amekubaliana na upande wa mashitaka, hata hivyo akaomba mahakama itoe hati mteja wake afikishwe mahakama waweze kuendelea na vikao.

“Sina pingamizi juu ya maelezo ya upande wa mashitaka, lakini naomba mahakama itoe removal order (hati ya kumtoa mshtakiwa mahabusu na kumpeleka mahakamani) ili tuje tuendelee na vikao vya majadiliano kuimaliza kesi hii,” ameomba wakili Mwamboma.

Hakimu Mhini amekubali ombi la mshtakiwa akisema atatoa hati hiyo mshtakiwa aweze kuletwa mahakamani. Aliahirisha kesi hadi Julai Mosi, 2024 itakapotajwa.

Kesi hiyo imeendeshwa kwa njia ya video mshtakiwa akiwa rumande.

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anakabiliwa na mashitaka mawili ambayo ni kujipatia Sh5.1 bilioni na kutakatisha kiasi hicho cha fedha katika kesi ya uhujumu uchumi namba 8/2023.

Katika shitaka la kwanza, anadaiwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika Jiji la Dar es Salaam, akiwa Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, kwa njia ya udanganyifu alijipatia Sh5.139 bilioni kutoka Saccos ya Jatu

 kwa maelezo fedha hiyo atazipanda kwenye kilimo cha mazao, jambo ambalo alijua kuwa siyo kweli.

Shitaka la pili anadaiwa kutakatisha kiasi hicho cha fedha tukio analodaiwa kulitenda kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika Jiji la Dar es Salaam.

Anadaiwa akiwa Mtendaji Mkuu na mwanzilishi wa Jatu Saccos alijihusisha na muamala wa Sh5.139 bilioni  kutoka akaunti ya Jatu Saccos iliyopo benki ya MNB tawi la Temeke kwenda akaunti ya Jatu PLC iliyopo benki ya NMB tawi la Temeke, wakati akijua fedha hizo zinatokana na kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Related Posts