Akufukuzae hakuambii toka. Ndiyo msemo unaoweza kuutumia kwa mshambuliaji wa Simba, Pa Omar Jobe, ambaye mashabiki wa klabu hiyo wameonyesha kiu kubwa ya kutamani kuona anaachwa.
Simba wiki hii, imeanza kuwaaga wachezaji wake ambao hawatawahitaji msimu ujao, ikiwa tayari imeshawaaga wawili, aliyekuwa nahodha wake mshambuliaji John Bocco, Jumatatu Juni 17 na leo ikimuaga kiungo mshambuliaji mkongwe Said Ntibazonkiza ‘Saido’, wakipewa ‘Thank you’, yaani ahsante kwa kuitumikia klabu hiyo lakini ndani yake akatajwa Jobe.
Kila habari za wachezaji hao walipotajwa kwenye ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Instagram ya klabu hiyo, mashabiki wengi wameonyesha kiu ya kusubiri ‘thank you’ ya mshambuliaji huyo raia wa Gambia.
Tangu atue ndani ya klabu hiyo, akiingia kupitia dirisha dogo la usajili, Jobe amefunga bao moja pekee hatua ambayo haikuwafurahisha mashabiki wa Simba licha ya kupewa muda wa kutosha kucheza ndani ya timu hiyo.
Hata hivyo, Simba italazimika kukaa mezani na Jobe kukubaliana vizuri kama inataka kukata kiu ya mashabiki wake wanaotamani aondoke, kwani mshambuliaji huyo bado ana mkataba wa mwaka mmoja na nusu wa kuitumikia klabu hiyo.