JKU yatemeshwa ubingwa FA Zenji, Chipukizi kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika

Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) limeipa ubingwa wa FA Chipukizi baada ya mchezo wa fainali dhidi ya JKU kuvunjika dakika ya 103, kutokana na vurugu zilizotokea kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Mchezo huo uliokuwa umechezwa kwa dakika 90 na timu hizo kutoka sare ya bao 1-1, ulilazimika kuongezwa dakika  30 kuwa 120, lakini ulivunjika dakika hiyo ya 103 baada ya JKU kuanzisha vurugu kwa kumvamia mwamuzi baada ya kukataa bao walilofunga, akidai ni ‘off side’.

Mwamuzi huyo alidai mchezaji wa JKU aliotea ndipo viongozi na wachezaji kumvamia mwamuzi na kusababisha kuvunjika kwa mchezo huo timu hiyo imetozwa faini ya Sh2 milioni na ubingwa kupewa timu pinzani (Chipukizi)

Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa kanuni ya mashindano ya ZFF 2023/24 sura ya 20(6), huku Chipikuzi nao licha ya kubeba ubingwa huo, imepigwa faini ya Sh1 milioni kwa kosa la mashabiki wake kurusha chupa na makopo uwanjani, adhabu hiyo ni kwa mujibu wa kanuni ya mashindano ya ZFF 2023/24 sura ya 19(3) II.
Pia mwamuzi wa mchezo huo, Mohamed Amour Ngwali amesimamishwa kuchezesha michezo yote inayosimamiwa na ZFF kwa muda wa miezi mitatu pamoja na kutozwa faini ya Sh500000 (laki tano)
Kulingana na kanuni na taratibu za Shirikisho la soka Zanzibar, Chipukizi itawakilisha visiwa hivyo kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Related Posts