Mbowe awataka Chadema Manyara kujipanga uchaguzi wa Serikali za mitaa

Babati. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Freeman Mbowe amewataka viongozi na wanachama wa chama hicho kujipanga ipasavyo kushiriki kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa ili kuongoza vijiji, vitongoji na mitaa nchini.

Akizungumza mjini Babati, leo Juni 18, 2024 Mbowe amesema viongozi wa Chadema na wanachama wanapaswa kujiandaa ili washiriki na kushinda nafasi za uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka 2024.

Mbowe amesema ushindi wa nafasi hizo kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa utakuwa mwanga na dira ya ushindi wa Uchaguzi Mkuu wa nafasi ya urais na wabunge unaotarajiwa kufanyika mwaka 2025.

Amesema kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa kuhakikisha anashiriki kutafuta ushindi wa wagombea wa Chadema kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa pindi utakapowadia.

Hata hivyo, amesema bila kuwa na msimamo na kujiandaa vema hawawezi kupata ushindi, hivyo viongozi na wanachama wote wajiweke tayari na kufanya maandalizi mapema.

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) Mkoa wa Manyara, James Nzige amesema wamejipanga kuhakikisha wanashiriki na kushinda nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa.

Nzige amesema miaka mitano iliyopita Chadema ilikuwa inaongoza Babati mjini na kuwa na madiwani wengi, hivyo wanajipanga ili kurudisha hali ilivyokuwa awali.

“Tumejipanga kwa kufanya chaguzi na kupata viongozi wa ngazi ya msingi na hivi sasa uchaguzi wa majimbo unafanyika ili kupanga safu zetu vyema na kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa,” amesema Nzige.

Amesema anatarajia wananchi wa Manyara ambao ni wana demokrasia na wenye msimamo, watawaunga mkono kwa kuwachagua viongozi wa kupitia chama hicho pindi muda wa uchaguzi utakapofika.

Mkazi wa Nangara mjini Babati, Solomon John amesema hatua hiyo ya Chadema kujipanga kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa itakuwa vema kwa kuwa  hawakushiriki chaguzi hivi karibuni.

John amesema walizoea kuwaona Chadema wakisusa chaguzi mbalimbali hivi sasa ila baada ya Mbowe kutoa tamko kuwa watashiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa wamefarijika.

Related Posts