Samia: Taasisi, idara zilipe madeni ya vyombo kabla ya Desemba 24

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa miezi sita kwa wizara na taasisi zote za umma zinazodaiwa na vyombo mbalimbali vya habari kuhakiki madeni na kukubaliana namna ya kuyalipa.

Agizo hilo limetokana na kilio cha muda mrefu cha vyombo vya habari kwa Serikali cha kutaka madeni yalipwe ili kuvifanya vitekeleze wajibu wake ipasavyo, ikiwemo kulipa stahiki za wafanyakazi na gharama za uendeshaji.

Rais Samia ametoa agizo hilo jijini Dar es Salaam, wakati akifungua Kongamano la Pili la Maendeleo ya Sekta ya Habari lililoanza leo Juni 18, 2024 na kuhitimishwa kesho. Limeshirikisha wadau mbalimbali na taasisi za habari.

Amesema hayo baada Kamati ya Kutathmini Hali ya Uchumi katika vyombo vya habari na Umoja wa Haki ya Kupata Taarifa (CoRI) kumwomba Rais Samia kusema jambo juu ya madeni ambayo Serikali inadaiwa, yanavyochangia kudhoofisha tasnia ya habari nchini.

Ombi kama hilo limewahi kutolewa mara kadhaa na Jukwa la Wahariri Tanzania (TEF) kwenye mikutano yake mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ambao kwa nyakati tofauti walizitaka taasisi zinazodaiwa kuyalipa.

Leo kwenye kongamano hilo, Rais Samia ametumia sehemu ya hotuba yake kutoa agizo juu ya madeni hayo.

Hata hivyo, amesema yapo yanayolipika na yeye atasimamia ulipaji wake na mengine hayalipiki kutokana na kutokuwa na vielelezo mahsusi vinavyoyadhibitisha.

“Hili la madeni ni suala la muda mrefu, nimelisikia siku nyingi, tumekwisha kuanza kufanya uhakiki, kuna madeni yanalipika na mengine hayalipiki na ni mengi, si madogo,” amesema Rais Samia.

“Wizara na taasisi zote za umma zinazodaiwa ndani ya Serikali yangu zihakiki madeni hayo na kuhakikisha zinakubaliana na taratibu za kulipana na jambo hili lifanyike si zaidi ya Desemba 24,” amesema huku akishangiliwa na washiriki wa kongamano hilo.

Katika kusisitiza hilo amesema: “Tukivuka Desemba 25 madeni mengi ya vyombo vya habari yanayolipika yawe yamelipwa, mimi nitasimamia ndani ya Serikali yangu, nanyi hakikisheni madeni yenu yamekaa vizuri.”

Alisema ataisikuma Wizara ya Fedha kuhakikisha kama wamekusanya madeni yote ya Serikali na uhakiki wa madeni ya vyombo vya habari na yale yanayolipika yaweze kulipwa.

Vilevile, Rais Samia ametoa wito kwa vyombo hivyo vya habari pindi madeni hayo yatakapolipwa navyo viwalipe wafanyakazi wake.

Mbali na hilo, mkuu huyo wa nchi huku akisisitiza vyombo vya habari si mshindani wa Serikali, bali ni mdau mshiriki wa masuala ya sekta ya umma, amevitaka viandike mambo yanayojenga Taifa na si kubomoa.

Amesema siku za nyuma vyombo vya habari vilikuwa katika mvutano na Serikali na hawakufika popote lakini uamuzi wa kukaa pamoja na kuzungumza na kushirikiana navyo umeondoa mivutano.

“Vyombo vya habari vikiwa huru vinagusa kila pembe ya eneo na vinahamasisha kupokea ujuzi mpya, taarifa za maendeleo, vinafichua maovu vinavyofanywa na watendaji wa umma, vinatoa hisia za wananchi dhidi ya Serikali yao na vinafanya kazi ya kukuza demokrasia.”

“Vyombo vya habari si mshindani wa Serikali, huko nyuma tulikuwa…hawa wanavuta na wale wanavuta, lakini kipindi hicho sijui ni lini. Lakini tulipoamua kukaa kitako na kuzungumza angalau tunaona,” amesema Rais Samia.

“Hapa nayakumbuka sana maneno ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa India, Jawaharlal Nehru akiambiwa kuchagua, alisema nina hiyari ya kuchagua uhuru wa vyombo vya habari pamoja na changamoto zake, kuliko kuufinya hivyo na mimi naungana naye asilimia 100,” amesema.

Rais Samia amewasisitiza waandishi kutumia kalamu zao vizuri wanapoandika masuala mbalimbali kwa kutanguliza mbele masilahi ya Taifa

“Tuepuke kujivua nguo sisi wenyewe,” ameonya.

Hata hivyo, kiongozi huyo amesema hapingi kukosolewa: “Mimi naamini mawazo kinzani,” akieleza yanamsaidia kuboresha lakini yanayozingatia staha, si lugha zisizofaa hususan mitandoni.

“Uhuru wa kutoa mawazo kinzani si uhuru wa kutukana, kukebei mambi…Uhuru wa kujieleza una mipaka yake,” amesema.

Aidha, Rais Samia amewataka maofisa habari wa umma kuelewa sera za sekta wanazofanyia kazi na wasiogope kuandika changamoto zinazowakabili.

“Watu hawajui sera za sekta wanazofanyia kazi matokeo yake wanakuwa wanawafuata viongozi nyuma tu na kamera zao, unakwenda kuandika, hapana huu si uandishi wa habari, ijue wizara yako,” amesema.

Mbali na hilo, Rais Samia amemwagiza Waziri Nape kuangalia ama kuunda kamati au vinginevyo, kuandaa Mkakati wa Mawasiliano Tanzania, akisema unahitajika sana kuwapo unaoendana na mahitaji ya sasa.

“Kama hatuna tunafanyaje, kama upo unatumikaje, Waziri kama utaunda timu nyingine bwana Tido aiongoze,” alisema.

Awali, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema ingawa Tanzania haijafika katika uhuru wa habari inaoutarajia, angalau ipo katika hatua tofauti na iliyokuwanayo siku za nyuma.

“Hayo yamefanyika kutokana na mageuzi ya usimamizi katika sekta ya utangazaji na mapitio ya sera na kanuni ambayo msingi wake ni maelekezo yako (Rais Samia),” alisema.

Mafanikio hayo, alisema yamechagizwa na kuongezeka kwa uzalendo kwa wanahabari na mabadiliko ya sera na sheria, akirejea maporomoko ya tope wilayani Hanang, Mkoa wa Manyara akisema wanahabari wengi walieleza uhalisia wa tatizo.

Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya kutathmini hali ya uchumi katika vyombo vya habari, Tido Mhando amewasilisha ripoti ya kamati hiyo ikitaja maeneo sita yanayolithibitisha hilo.

Miongoni mwa maeneo hayo amesema ni madeni ya vyombo vya habari kwa taasisi na wakala za Serikali, akidokeza yanazorotesha ustawi wa vyombo hivyo huku akimwomba Rais Samia kulitolea maelekezo jambo hilo.

Kuhusu takwa la la kisheria linalozuia asiye Mtanzania kuzuiwa kumiliki zaidi ya asilimia 49 ya hisa iwapo anataka kuwekeza, Tido amesema kamati imependekeza asilimia ziongezwe hadi 75. Kwa sasa mzawa ni asilimia 51 na asiye Mtanzania asilimia 49, ambalo Rais Samia amesema watakwenda kuliangalia.

Jambo lingine alilolieleza, ni vitisho ambavyo vimesababisha vyombo vya habari kujidhibiti katika uchapishaji wa maudhui, kwamba vimeacha masuala yenye masilahi ya umma na kuhabari viti vidogo vidogo.

Katika hilo, Tido ambaye ni nguli katika tasnia, aliitaka Serikali kupunguza ubabe ambao umekuwa mwingi na hakuna chombo ambacho hakijakutana nao.

Suala la hisa katika umiliki wa vyombo vya habari, lilizungumzwa pia na Mwenyekiti wa (CoRI), Ernest Sungura aliyeomba kuondoa wasiokuwa waruhusiwe kuwekeza kwa zaidi ya asilimia 49.

Ajibu hilo, Rais Samia alisema kwa kuwa suala hilo ni takwa la kisheria watakwenda kuliangalia.

“Ni kweli vyombo vingi vilivyokuwa na watu wa nje wamerudi nyuma na kwa hiyo vyombo vile vimerudi nyuma, kwa hiyo tutakwenda kuliangalia,” amesema.

Sambamba na hilo, Sungura ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), ametaka sheria ya ajira na mahusiano kazini itekelezwe hata katika taaluma ya habari, ili kuhakikisha wanahabari wanalipwa na wanakuwa na mikataba, akirejea takwimu za Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari (UTPC), zinazosema asilimia 80 hawana mikataba hiyo.

Katika mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema wamepokea na wamelifanyia kazi agizo la Rais Samia kuhusu wakuu wa mikoa na wilaya kuacha ubabe.

“Dar es Salaam ni salama na hii inatokana na maelekezo yako mazuri, namna ambavyo umetuasa sisi wakuu wa mikoa na wilaya kuongoza vizuri, tuepukane na masuala ya kibabe, ingawa mimi nilishaacha,”amesema Chalamila.

Related Posts