Geita. Upande wa utetezi katika kesi ya mauaji ya aliyekuwa mfanyakazi wa Kampuni ya Uchimbaji Dhahabu ya Geita (GGML), Milembe Suleman umeiomba Mahakama Kuu Kanda ya Geita kutopokea kielelezo cha shahidi wa 13 ambacho ni maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa pili, Safari Lubingo.
Pingamizi limetolewa na wakili wa utetezi, Laurent Bugoti anayemtetea Lubingo akidai mteja wake alitoa maelezo bila ridhaa kwa kuwa alipigwa kinyume cha kifungu cha 27(3) cha Sheria ya Ushahidi.
Kesi hiyo namba 39 ya mwaka 2023 inasikilizwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Kelvin Mhina. Ilitajwa jana kwa ajili ya upande wa mashitaka kuendelea na ushahidi.
Milembe (43), aliyekuwa mfanyakazi wa kitengo cha ugavi cha GGML aliuawa usiku wa kuamkia Aprili 26, 2023 kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali mwilini, ikiwemo kichwani, usoni na mikononi.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Dayfath Maunga (30), Safari Lubingo (54), Genja Deus Pastoy, Musa Lubingo (33) na Ceslia Macheni (55). Wanakabiliwa na shitaka moja la kumuua Milembe Seleman.
Akitoa ushahidi leo Juni 18, 2024 shahidi wa 13 wa upande wa mashitaka, Said ambaye ni askari polisi kitengo cha upelelezi wa makosa ya jinai amedai Mei 5, 2023 ndiye aliyeandika maelezo ya onyo ya mshtakiwa Safari Lubingo.
Akiongozwa na mwendesha mashitaka, Wakili wa Serikali, Merito Ukongoji amedai wakati wa mahojiano mshtakiwa alikiri kushiriki mauaji ya Milembe, pia alikiri kushirikiana na mshtakiwa wa kwanza Dayfath.
Kutokana na ushahidi huo, ameiomba Mahakama kupokea maelezo ya onyo kama kielelezo ndipo upande wa utetezi ulipinga kupokewa kielelezo hicho kwa hoja tatu.
Hoja hizo ni mshtakiwa kutoa maelezo bila ridhaa yake kwa kuwa alipigwa, maelezo ya onyo kuchukuliwa nje ya muda wa kisheria wa saa nne, na kwamba mshtakiwa hakusaini baadhi ya maelezo ikielezwa saini inayoonekana ni ya askari aliyeandika maelezo hayo.
Mahakama ilisikiliza kesi ndogo ndani ya kesi kubwa, ambayo upande wa mashitaka ulikuwa na shahidi mmoja aliyedai mshtakiwa alisaini maelezo, na kuhusu kupigwa alidai alimuhoji akiwa kwenye hali nzuri.
Shahidi wa utetezi, mshtakiwa wa pili, Safari Lubingo akiongozwa na wakili Bugoti amedai alikamatwa Mei 3, 2023 na kufikishwa kituo cha polisi Geita alikohusishwa na mauaji ya Milembe ambaye hakuwa akimfahamu.
Amedai akiwa chini ya polisi aliamriwa kuvua nguo zote na kulala chali kisha kupigwa na askari ili akubali tuhuma alizopewa na baada ya kipigo alipelekwa Kituo cha Polisi Nyarugusu.
Amedai alipigwa kwa siku tatu na Mei 5, 2023 ndipo yalipoandikwa maelezo na kutokana na kipigo Mei 9, 2023 alipelekwa Hospitali ya Mkoa wa Geita.
Aliiomba mahakama kupokea kielelezo ambacho ni PF3 aliyopewa kwenda hospitali. Ilipokewa na mahakama kama kielelezo ID1. Amedai maelezo ya onyo siyo yake bali ni ya polisi.
Upande wa utetezi umeiomba mahakama kutoa wito wa kufika mahakamani mashahidi wawili ambao ni askari wa upelelezi Sajenti Pascal anayedaiwa kutoa PF3 na Christopher Matola daktari anayedaiwa kumtibu mshtakiwa.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 19, 2024 kwa upande wa utetezi kuleta mashahidi.