Arusha. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 50 ya kuanzishwa kwa Jumuiya ya Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika inayoshughulikia Sayansi ya Afya (ECSA-HC) yatakayofanyika Juni 19, 2024 jijini Arusha.
Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Arusha, Frank Mbando amebainisha hayo leo Juni 18, 2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kongamano hilo la sayansi ya afya linaloendelea jijini hapa.
Amesema katika maadhimisho hayo, wananchi zaidi ya 500 watanufaika na huduma ya kupima na kuchunguza afya zao bure ikiwa ni sehemu ya maadhimisho hayo, kuchunguza magonjwa yasiyoambukiza na kupatiwa tiba.
Amesema taasisi hiyo yenye muunganiko wa nchi wanachama zipatazo tisa na makao makuu yake yapo jijini Arusha, inaadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake na kilele kitafungwa Juni 19, 2024 na Dk Mpango.
Mbando amesema pamoja na mijadala ya kisayansi inayoendelea kuhusu tafiti za afya, ECSA-HC iangalie namna ya kujikomboa na kujitegemea zaidi katika sekta ya afya, katika mazingira ya uwezeshaji wa dawa na vifaa tiba ukizingatia kwamba bado nchi za Afrika zinategemea zaidi kuagiza vifaatiba na dawa ambavyo ni gharama kubwa kutoka nje ya nchi zao.
“Juni 19, 2024 ndiyo kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya ECSA-HC, tunatarajia Dk Mpango kuwa mgeni rasmi na kabla ya hapo tutashuhudia kambi ya uchunguzi wa matibabu bure. Ni vizuri wananchi wakatumia fursa hiyo kuangalia afya zao na huduma hiyo inatolewa bure bila malipo,” amesema Mbando.
Mkurugenzi mtendaji wa taasisi hiyo, Profesa Yoswa Dambisya amesema kabla ya kilele cha maadhimisho hayo wataalamu wa afya wapatao 250 wamekutana kutoka mataifa mbalimbali kwa lengo kubadilishana uzoefu na kuwasilisha mafanikio ya tafiti za afya.
Dk Godfrey Sama ambaye ni mmoja ya waandaaji wa kongamano hilo, amesema kilele cha maadhimisho hayo kitakwenda sambamba na uchangiaji damu na wanatarajia kutoa huduma ya uchunguzi wa afya kwa watu zaidi ya 500 katika kambi iliyopo General Tyre Arusha.
Mshirikiwa wa kongamani hilo, Dk Mpoki Ulisubisya amesema kumekuwepo na changamoto ya idadi kubwa ya wananchi kutumia dawa kiholela bila kufanya vipimo hatua ambayo amesema inachangia ugonjwa kuendelea kuwa sugu, hivyo amewataka wataalamu wa afya kujenga utaratibu wa kutoa elimu kwa wananchi na kufanya vipimo kabla ya kutumia dawa.
Dk Ulisubisya amesema changamoto iliyopo ni utafiti unaofanywa wa kuzalisha dawa za kutibu ambao hauendani na kasi ya uhitaji uliopo na amewataka wananchi kujijengea utaratibu wa kutumia dawa za hospitali kwa kuwa ndizo dawa sahihi.
Profesa Tigan Moyo kutoka Zimbabwe amesema Wizara za Afya kutoka nchi mbalimbali zimekuwa zikifanya jitihada kuhakikisha sekta ya afya inaimarika hususani kwa usalama wa wananchi, hivyo mkutano huo unaangazia mchango wa wataalamu hao katika sekta nzima ya afya.