Wawakilishi waonyesha udhaifu, uimara wa bajeti

Unguja. Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wameanza mjadala wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/25 wakionyesha udhaifu na uimara wake, huku  wakitaka isiishie kwenye makaratasi.

Wakichangia bajeti hiyo ya Sh5.182 trilioni iliyowasilishwa barazani Juni 13, 2024 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya, baadhi ya wawakilishi wamesema bajeti hiyo ni ya mfano, na iwapo itatekelezwa italateta mabadiliko kwa Zanzibar na wananchi wake. 

Mwakilishi wa Wawi, Bakar Hamad Bakar leo Juni 18, 2024 amesema licha ya bajeti kuandaliwa vizuri na kuwasilishwa kwa weledi, haitakuwa na tija kama hakutakuwa na utekelezaji, hivyo mambo hayo yaende sambamba.

Ameitaka Serikali kuimarisha mifumo ya manunuzi itakayoweka uwazi zaidi na nidhamu katika matumizi ya fedha za umma.

“Tatizo si miradi kufanyika, tatizo liangalie je kilichofanyika ndicho kilichotakiwa? Kwa hiyo mambo haya lazima yasimamiwe kwa umakini. Tuombe Serikali isimamie na kuendeleza mifumo imara kwenye usimamzi wa fedha za umma, hizi ni fedha za walipa kodi,” amesema.

Pia amezungumzia ujenzi wa uwanja wa ndege wa Pemba, akisema mpango ulikuwapo muda mrefu na wananchi walisimamishwa kuendeleza nyumba na mashamba tangu mwaka 2017.

Amesema licha ya dhamira nzuri ya Serikali kujenga uwanja huo, bado kuna changamoto kwa baadhi ya wananchi kutopewa fidia, hivyo kuendelea kuwa na wasiwasi.

“Hatua ambayo imeshaanza niwapongeze, lakini bado kuna malalamiko katika fidia, licha ya baadhi yao wameshaanza kulipwa, wale ambao hawajalipwa wanaendelea kuwa na wasiwasi kama watalipwa au vipi,” amesema.

Amesema Serikali itafute namna ya kuwalipa wananchi wawekeze katika maeneo mengine, kwani kushindwa kufanya hivyo inazidi kuwaumiza.

Akizungumza ajira, amesema ikiwa wanataka kuajiri vijana wengim lazima Serikali ijikite katika sekta ya uvuvi, hususani wa bahari kuu.

Amesema Serikali imeonyesha jitihada za kutoa vifaa kwa wavuvi wadogo, lakini imesahau uvuvi wa bahari kuu ambao utasaidia kutoa ajira nyingi na kuongeza mapato ya Serikali.

Mbali na hilo, amekumbushia ahadi ya Serikali iliyowahi kutoa kuhusu ununuzi wa meli kubwa ya uvuvi wa maji marefu.

“Kama imeshindikana basi Serikali ifanye kutenga fedha za ndani inunue meli kubwa kufanya uvuvi maeneo ya bahari kuu, kwani nchi yetu ni ndogo kama tukiwekeza vizuri huko itapunguza tatizo la ajira,” amesema.

Kuhusu deni la Taifa la Sh1.1 trilioni, amesema licha ya kuwa ni himilivu, lakini Serikali iwe makini na taasisi inazokopa kwa kuzingatia masharti nafuu yanayotolewa na taasisi husika.

“Ukikopesheka maana yake anayekukopesha anaona una uwezo huo, kwa hiyo nchi yetu inakopa kujenga miundombinu haina budi ikakopa kwa sasa ili miradi hiyo isisubiri kesho ifanyike leo. Hapa serikali inatakiwa kuangalia masharti ya taasisi zinazokepesha,” amesema.

Mwakilishi wa Mfenesini, Machano Othman Said akizungumzia ajira amesema ukosefu wake kwa vijana ni tatizo kubwa.

“Kwa hiyo lazima Serikali ije na jibu la suala hili na matumizi ya dawa za kulevya inaweza kufifisha juhudi za kuleta maendeleo,” amesema.

Machano amesema pamoja na mipango mizuri ya ujenzi wa viwanja vya ndege, lazima kuwe na barabara nzuri, na za kisasa kwa sababu mtalii au mgeni akishuka uwanja wa ndege lazima apate usafiri wa haraka kufika anapotaka kwenda.

Amesema bado kuna wawekezaji wanapata changamoto, hawapati maji ya uhakika na umeme kwa wakati wote kwa hiyo ni jukumu la Serikali kuhakikisha huduma hizo zinapatikana bila kuyumba ili kukuza uwekezaji.

Amesema uchumi wa Zanzibar unaweza kuendeshwa na utalii pekee iwapo Serikali ikiendelea kuweka mikakati imara na kufungua maeneo mengine ya uwekezaji, hususani katika visiwa.

Amesema Serikali ina wajibu wa kuendelea kutoa huduma za afya, na kuhakikisha shule zinakuwa na mkondo mmoja na wanafunzi 45 kwa darasa moja.

Akizungumzia bajeti kwa ujumla amesema, “Hii ni bajeti bora kuwahi kutokea, kinachotakiwa fedha hizi zitoke iweze kutekelezwa.”

Mwakilishi wa Mahonda, Asha Abdalla Mussa amesema Rais ana nia safi kuhakikisha mfumuko wa bei unashuka lakini mwaka uliopita 2023 umeongezeka kufikia asilimia 6.9 kutoka asilimia 5.1.

“Jitihada zinafanyika, Serikali ilitumia zaidi ya Sh3 bilioni kusamehe kodi za baadhi ya vyakula na mafuta vinginevyo ingeongezeka mara dufu, kwa hiyo hili eneo linahitaji mkakaati maalumu, kwani bidhaa zinapoongezeka bei wanaoumia ni wananchi wa hali ya chini,” amesema.

Ameishauri Serikali kuendeleza maeneo ambayo hayajapata wawekezaji, ili kuongeza idadi ya watalii wanaoingia kisiwani humo.

Hata hivyo, amesema iwapo bajeti itatekelezwa ipasavyo nchi itaimarika kwa kuwa imezingatia jinsia.

Mwakilishi wa kuteuliwa, Juma Ali Khatib ameipongeza Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) kwa kuimarisha mifumo, akisema imepunguza wafanyabiashara kupanga foleni kwenda kuwasilisha mapato ya Serikali.

Ameishauri Serikali kuongeza jitihada za ujenzi wa barabara za vijijini katika maeneo ya uchumi wa buluu, na kuimarisha miundombinu iwe rafiki kuchochea uwekezaji.

“Matumaini yetu msimu ujao utakuwa na karafuu nyingi kwa hiyo tunahitaji kuimarisha miundombinu wakulima wapate kusafirisha mazao, na itapunguza magendo,” amesema.

Amezungumzia pia tatizo la wafanyabiashara kusumbuliwa bandarini akiishauri Serikali kuliangalia jambo hilo akieleza wapo watu wamechukua mikopo wanapopata usumbufu wa kusafirisha bidhaa, hivyo watashindwa kulipa.

Kuhusu kilimo cha umwagiliaji amesema: “Kila mwaka tumekuwa na mipango mizuri ya kilimo cha umwagiliaji lakini haitekelezeki kwa hiyo tunataka kujua wapi tunakwa?”

“Nguvu kazi tunayo, ardhi tunayo kwa hiyo ni vyema tukafika mahali Zanzibar ikajitosheleze kwa chakula hususani mchele, kitu gani kinakwamisha mpaka leo hatujajitosheleza,” amehoji.

Amesema Zanzibar ina wataalamu wengi wa kilimo, hivyo umefika wakati kuwashirikisha kuinua kilimo hususani cha umwagiliaji.

Mwakilishi wa Mtoni, Hussein Ibrahim Makungu amesema ni lazima kuimarisha sekta ya fedha, miundombinu na huduma za utalii bila kubweteka kutokana na sekta hiyo kuendelea kukua.

Makungu amesema kuna mapato mengi yanapotea, kwani wageni wengi wakifika Zanzibar hawajulikani wanakwenda wapi, akashauri ZRA, Uhamiaji na Kamisheni ya Utalii kushirikiana kuwa na mtandao mmoja kufahamu wageni wanaoingia na sehemu wanapokwenda.

“Hakuna mgeni anatoka Ulaya anakuja Zanzibar hajui wapi anakwenda kulala, hili jambo kuna fiche (siri) kubwa kwa hiyo linachangia kupoteza mapato mengi ya Serikali, inawezekana kinachokusanywa ni robo tu,” amesema.

Amezungumzia kero ya usafirishaji mizigo bandarini kutoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara, licha ya kuwa ni nchi moja.

“Waziri (Dk Saada) wewe umekuwa waziri hata Bara unayajua haya matatizo, mtu ana sukari kilo moja anatakiwa alipe, haya si mambo mema kila siku wasikia kero lakini tuwe wamoja kuondosha kero hizi. Muungano ni mzuri lakini hili linatuchafua,” amesema.

Amesema biashara zinazotoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara zinafikia zaidi ya Sh150 bilioni.

“Hatuwezi kuajiri wote, sasa watu wanajiajiri lakini wanakutana na vikwazo,” amesema.

Bajeti itajadiliwa kwa siku tatu.

Related Posts