* Serikali yapongeza jitihada hizo zitakazotengeneza ajira kwa vijana
SERIKALI Imepongeza jitihada za Benki ya Standard Chartered ambayo imezindua rasmi mradi wa ‘Futuremakers Initiative-Ready for Inclusive Suistainable Employment and Enterpreneurship (RISE/E) wenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni mbili wenye lengo la kukuza matarajio ya ajira kwa vijana wenye ulemavu pamoja na kusaidia biashara ndogo ndogo kwa vijana wenye na wasio na walemavu hususani wanawake.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa mradi huo Kaimu Katibu Tawala anayeshughulikia uchumi na uzalishaji Mkoa wa Dar es Salaam Dk. Elizabeth Mchote ambaye alimwakilisha Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu; Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Patrobas Katambi amesema, mradi huo wa shilingi Bilioni mbili, milioni mia mbili hamsini na nne elfu laki sita na tisini na tisa elfu na mia sita ishirini (2,254,699,620) wa miaka mitatu umelenga kusaidia vijana 270 wenye ulemavu huku wanawake wakiwa 50%.
Amesema, mradi huo umefika kwa wakati na ni fursa kwa vijana kuingia katika soko la ajira.
“Kulingana na matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, Tanzania ina idadi kubwa ya vijana walio chini ya miaka 25 na tunafahamu changamoto za zinazowakabili ikiwemo ufinyu wa ajira na fursa za ujasiriamali kupitia mradi huu tunaamini vijana wengi watanufaika kwa kupata mafunzo ya uwezo na kuwa na biashara zenye mafanikio.” Amesema.
Aidha amesema, Katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili vijana kuna umuhimu wa ushirikiano baina ya sekta binafsi na Serikali ili kutengeneza fursa nyingi za ajira na ujasiriamali kwa vijana na kukuza uchumi wa Tanzania.
Kuhusiana na mradi huo ameeleza kuwa, vijana hususani wanawake wenye ulemavu ambao huathirika katika masuala ya ajira watanufaika ambapo vijana 270 wenye ulemavu watapata ujuzi juu ya maandalizi ya kupata ajira ikiwa na mwendelezo wa kuwawezesha vijana 108 wenye ulemavu kupata ajira endelevu katika ujasiriamali.
“Serikali inaipongeza sana Taasisi ya Standard Chartered kwa kwa kuwekeza zaidi ya shilingi Bilioni 2.2 katika mradi huu ambao utasaidia kupunguza changamoto za ajira na ujasiriamali kwa vijana….Wizara ipo pamoja katika kuunga mkono hili katika kutengeneza na kuboresha sera, programu na mipango kwa ajili ya vijana, ajira, kazi na ustawi wa watu wenye ulemavu…Na Wizara itaendelea kutengeneza sera na programu shirikishi zaidi zinazokukuza ushirikishwaji kwa watu wenye ulemavu kwa kuhakikisha wanapata fursa sawa za ajira, elimu na masuala ya kijami.”Amesema.
Akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Standard Chartered Tanzania, Mkuu wa Biashara Wateja Wakubwa, wa Kati na Taasisi za Fedha Jerry Boateng amesema kuwa; mradi huo umelenga kunufaisha vijana hasa wanawake na wenye ulemavu.
Jerry amesema, vijana wapatao 270 wenye ulemavu watapata ujuzi kwenye maandalizi ya kupata ajira ikiwa na mpango wa kuwawezesha vijana 108 wenye ulemavu kupata ajira endelevu katika ujasiriamali huku biashara ndogondogo 90 zikitarajiwa kunufaika ikiwa pamoja na kupata ushauri wa kitaalamu wa kibiashara ili kukuza biashara zao na kuongeza kuwa kupitia mradi huo ajira 144 zitatengenezwa.
Pia ameeleza kuwa licha ya vijana wajasiriamali kuleta matokeo chanya katika jamii bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mitaji, taarifa sahihi za masoko ya uhakika na kukosa miongozo na hamasa ya biashara na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine katika kuziba ombwe katika masuala ya ajira na ujasiriamali kwa vijana.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE,) Suzanne Ndomba amesema, Mpango huo unaojumuisha vijana wenye ulemavu na wasio na ulemavu ni muhimu katika kuleta usawa na maendeleo katika kundi hilo la vijana na kuipongeza Benki hiyo kwa kuonesha kwa vitendo kupitia mradi huo wenye tija kwa jamii.
“ATE Tumefurahishwa na mradi huu ambao umelenga kuimarisha fursa na matokeo kwa vijana wenye na wasio na ulemavu kupata ajira zinazostahili pamoja na kujiajiri kupitia ujasiriamali….Vijana watumie nafasi hii kukua kimawazo, kujitambua na kuwa na digital skills ambayo haiepukiki.” Amefafanua.
Amesema, ATE imekuwa ikishirikiana na Ofisi ya TAMISEMI katika kuhakikisha maslahi ya watumishi wenye ulemavu yanazingatiwa mahala pa kazi pamoja na kuhamasisha waajiri kuzingatia sheria ya mwaka 2010 ya kundi hilo ambayo inawataka kuwaajiri kwa asilimia 3.
Mradi huo utatekelezwa na mashirika ya SightSavers na Challengers Worldwide kwa kushirikiana na Tanzania Gender Nertworking Programme (TGNP,) na Youth With Disabilities Organization (YoWDO.)
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam Dk. Elizabeth Mchote (wa pili kulia,) akiwa pamoja na menejimenti ya Standard Chartered wakizindua mradi huo. Leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE,) Suzanne Ndomba akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo na kuipongeza Standard Chartered Bank kwa uthubutu huo na kuwataka vijana kutumia fursa hiyo. Leo jijini Dar es Salaam.
Matukio mbalimbali wakati wa uzinduzi huo uliofanyika katika Hoteli ya Serena, Jijini Dar es Salaam.