Jamhuri ya Czech ilionekana kutumia mbinu za kujilinda zaidi na kutegemea mashambulizi ya kushtukiza karibia mchezo wote na mbinu zao zilizaa matunda baada ya Lukas Provod kufunga bao kunako dakika ya 62 ya mchezo.
Hata hivyo bahati haikuwa upande wao baada ya beki Robin Hranac kujifunga mwenyewe kabla ya Conceicao kuwakata maini kwa kufunga bao la dakika za lala salama.
Timu ya taifa ya Ureno, inayotiwa makali na kocha Roberto Martinez ni mojawapo ya timu zinazopigiwa upatu kushinda michuano hiyo japo ushindi huu wa kuungaunga unatilia mashaka uwezo wao wa hatimaye kuchukua ubingwa.
Soma pia: Mbappe avunjika pua katika ushindi wa Ufaransa dhidi ya Austria
Yote tisa, kumi ni ushindi unaoweka hai matumaini ya nahodha Cristiano Ronaldo kushinda taji lake la pili akiwa na timu yake ya taifa baada ya kulinyakua mnamo mwaka 2016 baada ya kuifunga Ufaransa 1-0 katika mechi ya fainali.
Ureno sasa itavutana mashati na Uturuki mnamo siku ya Jumamosi katika mechi yao ya pili itakayotifua vumbi katika dimba la Signal Iduna Park mjini Dortmund huku Jamhuri ya Czech ikiwa na miadi na Georgia mjini Hamburg.
Kwengineko, kinda wa Real Madrid Arda Guler alionyesha makali yake baada ya kufunga bao maridadi na kuisaidia timu yake ya taifa ya Uturuki kupata ushindi wa 3-1 dhidi ya Georgia, inayoshiriki michuano hiyo ya Ulaya kwa mara ya kwanza katika historia yao.
Soma pia: Waziri wa Uchumi wa Ujerumani asema Michuano ya Euro 2024 ni zawadi kwao
Guler mwenye umri wa miaka 19 na aliyebandikwa jina la utani la “Messi wa Uturuki” ameingia kwenye rekodi kwa kuwa mchezaji wa tatu mwenye umri mdogo zaidi kufunga bao kwenye mechi yake ya kwanza ya michuano ya EURO.
Guler anafuata nyayo za Ferenc Bene wa Ufaransa aliyepachika bao dhidi ya Uhispania mnamo mwaka 1964 na Cristiano Ronaldo aliyefunga bao dhidi ya Ugiriki mnamo mwaka 2004.
Kocha wa Georgia Willy Sagnol ameonesha kuridishwa na wachezaji wake licha ya kampeni yao kuanza kwa kipigo. hicho