Moshi. Rais, Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu kufuatia kifo cha aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa huo, Dk Tixon Nzunda (56) aliyefariki dunia pamoja na dereva wake, Alphonce Edson (54) jana, Juni 18, 2024 kwa ajali ya gari.
Ajali hiyo, ilitokea jana, Juni 18 saa 8:30 mchana katika eneo la Njiapanda ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) wakati wakienda kumpokea Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ambaye alikuwa akielekea mkoani Arusha kikazi.
Kufuatia taarifa iliyotolewa jana usiku, Juni 18 na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Sharifa Nyanga, Rais Samia anawapa pole ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu na Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi.
“Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ajali hiyo iliyochukua maisha ya Dk Nzunda na dereva wake imetokea majira ya saa nane mchana katika eneo la Njiapanda ya uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) Wilaya ya Hai alipokuwa kwenye ziara ya kikazi,”
“Rais Samia anawapa pole ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu, Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi,”