Hili la Msajili wa Hazina Zanzibar lifanywe na taasisi nyingine

Ofisi ya Msajili wa Hazina ya Zanzibar ambayo mwendo wake wakati inaanzishwa miaka miwili iliyopita ulikuwa wa konokono, sasa inakwenda kwa kasi na kutoa matumaini ya kupunguza ufisadi, matumizi mabaya ya fedha, mali za umma na madaraka ya baadhi ya maofisa wa mashirika na taasisi za umma.

Ofisi hii, wiki iliyopita imefungua milango na madirisha kwa vyombo vya habari kuelewa kazi inayofanywa, maendeleo, mafanikio na changamoto inazokabiliana nazo.
Hii ni tofauti na taasisi nyingi za umma za Zanzibar ambazo zimejijengea usiri na kuona waandishi wa habari wanaotaka taarifa au ufafanuzi juu ya masuala mbalimbali kuwa wakorofi na hawana haki hiyo.
Viongozi hawa wapo mstari wa mbele kuzungumzia umuhimu wa utawala bora, ukweli na uwazi na hasa juu ya mambo yanayowahusu walipakodi wa Zanzibar, lakini vitendo vyao vinatofautiana na kauli zao.
Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi aliwataka wakuu wa mashirika na taasisi za umma kuwa karibu na vyombo vya habari, lakini mwongozo ule unaonekana kupewa kisogo na wengi wao na wanapofanya mikutano huchagua wale watakaokuwa tayari kugeuzwa magolikipa na kazi yao kuwa kupokea tu.
Hawa ni wale waandishi, hasa wa vyombo vya serikali kwa kuhofia kupoteza ajira endapo watauliza masuala nyeti, wanabaki kuitikia hewala bwana au hewala bibi kwa kila wanachoambiwa hata wakijua wanadanganywa.
Katika kikao maalumu na waandishi wa habari, Msajili wa Hazina, Waheed Sanya na maofisa waandamizi wa ofisi yake, walifanya kikao cha karibu saa tatu cha kutoa taarifa na mijadala.
Msajili na wasaidizi wake waliwasilisha mada fupi zilizotoa maelezo ya muundo, mpango kazi, kinachoendelea na kilichopo mezani kukamilishwa.
Kilichonifurahisha ni kwa Msajili na wasaidizi wake kuchukua kama saa moja kutoa maelezo na kwa saa mbili wakapokea maswali na ushauri kwa njia ya kirafiki na maelewano.
Kikao hiki kilitoa nafasi nzuri kwa waandishi wa habari kuelewa kwa kina kazi za ofisi hii na kinachoendelea.
Katika maelezo ya Msajili na majadiliano yaliyofuatia, ilionekana wazi namna ofisi hii ilivyojipanga kupambana na ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka, fedha na mali ya umma.
Kwa mfano, ofisi hii ya Msajili imeanza kuitekeleza sheria ya kuhakikisha wanaochaguliwa kuwa wajumbe wa bodi za taasisi za umma ni watu wanaomudu kazi wanayopewa kwa kuwa na elimu na uzoefu wa kutosha na nidhamu.
Hivi sasa Ofisi ya Msajili inachuja waliopendekezwa na kupeleka majina ya wanaofaa kuteuliwa.
Hii itaondoa mwanya kwa waziri kuchagua wanafamilia, marafiki au watu ambao wana uelewa na uwezo wa kumudu kazi ya kusaidia kuliongoza shirika.
Eneo jingine ambalo alisema limeshughulikiwa ni namna ya kuuza mali za serikali. Kuanzia sasa kutakuwa na uwazi kwa kinachotaka kupigwa mnada kutangazwa mapema ili kuziba pengo la kuwepo upendeleo.
Hata hivyo, Ofisi ya Msajili itatoa kipaumbele kwa wafanyakazi wa shirika wanaotaka kununua kinachouzwa kwa mnada.
Hivi sasa, kanuni na taratibu za kuiendesha kazi hii kwa ufanisi zipo katika hatua za mwisho za kukamilika.
Ofisi ya Msajili wa Hazina ya Zanzibar pia imetia saini hati ya maelewano na Ofisi ya Msajili ya Bara na hivi sasa taasisi hizi zimeanza kushirikiana katika nyanja mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ukaguzi wa shughuli za baadhi ya mashirika.
Hatua ya Ofisi ya Msajili wa Hazina kuweka shughuli zake wazi na ujasiri wa kukutana na kuwapa waandishi wa habari nafasi ya kutosha kuuliza maswali, kupata ufafanuzi na hata kupokea ushauri, inafaa kuigwa na mashirika mengine ya umma Visiwani hapa.
Hii kwanza itasaidia kuelewa baadhi ya mambo yaliyojificha na kuelewa jamii inaionaje na kufahamu malalamiko yaliopo nje ya ofisi.
Ni vizuri kwa taasisi zilizojigubika chandarua kwa dhana kuwa viongozi wake watakuwa hawaonekani pale wanapotumia vibaya madaraka au matumizi ya fedha na mali za serikali kubadilika.
Kufikiria kazi kubwa ya waandishi wa habari ni fitna, ni kosa na vizuri wakaelewa wanachokifanya ni wajibu wao wa kuwa daraja zuri la mawasiliano kati ya serikali na taasisi zake na umma.
Ni kwa kuwepo mawasiliano mazuri na kufanya kazi pamoja kama washirika wa maendeleo, ndiyo taasisi hizi zinaweza kufikia malengo ya kuanzishwa kwake.
 

Related Posts