Keissy: Mizengwe uchaguzi 2020 ilining’oa, nikashtaki kwa JPM

Unamkumbuka Ally Keissy, mbunge wa zamani wa Nkasi Kaskazini (CCM)? Bila shaka utakubaliana nami kwamba Keissy ni mmoja wa wabunge machachari waliotikisa kwenye Bunge la 12 la mwaka 2015 – 2020.

Keissy alipata umaarufu kutokana na hoja zake tata zilizoibua mjadala na wakati mwingine zilibainika kwenda kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hususan hoja yake ya Muungano na kutaka Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli aongezewe muda.

Kuhusu Muungano, Keissy alikuwa na msimamo kwamba Wazanzibari wananufaika na Muungano, hivyo hawatakiwi kudai mambo mengi kwa kuwa wako wachache ukilinganisha na Tanzania Bara.

Mbunge huyo wa zamani, pia, aliwavunja watu mbavu aliposisitiza bungeni Juni 9, 2020 kwamba Rais Magufuli aongezewe muda wa kuendelea kuliongoza Taifa hili na ikibidi “alazimishwe atake asitake”.

Mwananchi limefanya mahojiano maalumu na Keissy kuhusu masuala mbalimbali, ikiwemo alivyoshindwa uchaguzi, uhusiano wake na hayati Magufuli, alivyosotea ubunge kwa miaka 20 na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete alivyomuingiza kwenye siasa.

Keissy ni mbunge pekee wa CCM aliyepoteza jimbo kwa upinzani katika uchaguzi wa mwaka 2020. Katika uchaguzi huo, alishindwa kutetea kiti chake cha Nkasi Kaskazini na kujikuta akipoteza ubunge wake kwa Aida Khenani wa Chadema.

Wengi walishangaa Keissy kushindwa kwenye uchaguzi huo katika kipindi ambacho alikuwa maarufu na wagombea wengi wa CCM kuwa na nafasi kubwa ya ushindi kutokana na mazingira ya wakati huo.

Keissy anasema alihujumiwa kwenye uchaguzi huo na baadhi ya watu waliomfanyia hujuma hiyo ni wenzake ndani ya CCM, jambo ambalo lilimsikitisha.

Anasema alianza kuona dalili za hujuma mapema tangu wakati anafanya kampeni, kwani kuna wafanyabiashara wanaCCM wenzake, walimpinga na kumsapoti mgombea wa Chadema.

“Walichanga pesa kumpa mgombea wa upinzani ili ‘aning’oe’ kwenye ubunge, hiyo ndiyo mbinu waliyoitumia, wakafanikiwa. Niliwaambia wananchi kinachoendelea, lakini hawakunisikiliza.

“Kwenye siasa huwa kuna mambo mengi, mengine ya hatari, hata hivyo niliifahamu njama hiyo kuwa ilikuwa mkakati wa makandarasi,” anasema Keissy.

Keissy anasema mkakati huo wa mahasimu wake ulifanikiwa, kwani hata waliokuwa wagombea wenzake kwenye kura za maoni hawakumuunga mkono.

“Nilimpigia simu Rais Magufuli, nikamueleza nilivyohujumiwa na wafanyabiashara makandarasi wa miradi ya maji ambao waliona naingilia maslahi yao na wengine nilikuja kugundua walikuwa na wakubwa nyuma yao,” anasema.

Mwanasiasa huyo anasema alipomueleza Magufuli, alimjibu kwamba angelifuatilia, lakini kabla hajamwambia chochote, mkuu huyo wa nchi wakati huo, akaaga dunia.

“Nilihujumiwa hadi na wanaCCM wenzangu, hakuna aliyekuja kunisaidia kampeni, nilisimama mimi kama mimi, hata wananchi waligeuka baada ya kupita kuambiwa wasinichague.

“Sikuwa na namna zaidi ya kukaa pembeni kuacha mambo yaendelee, lakini sikuona kosa langu kama mbunge kufuatilia miradi ya maendeleo jimboni kwangu,” anasema Keissy.

Keissy anasema chanzo cha kufanyiwa hujuma ni kufuatilia upigaji kwenye miradi mingi ya maji jimboni kwake akiwa mbunge.

“Kuna mradi mkubwa wa Nakarundi, mtu mmoja alitaka kuuchukua, sikukubali kuona pesa ni za Serikali halafu mradi uende kwa mtu binafsi,” anasema.

Anabainisha kwamba kuna Sh4 bilioni aliziokoa pia kwenye moja ya miradi ambao ulishuka kutoka Sh7.9 bilioni hadi Sh3.8 bilioni.

“Makandarasi wa huohuo mradi walinifuata hadi Dodoma nikiwa bungeni, wakataka kunihonga nikakataa, sikutaka hata kuonana nao.

“Kuna baadhi ya wanaCCM wenzangu wa kule Sumbawanga, Rukwa nao walinishawishi nichukue rushwa, nikawakatalia, nikasema sikuja bungeni kwa sababu ya rushwa, hiyo ilikuwa ni kipindi cha JPM,” anasimulia.

Anasema kwenye mradi wa Namanyere nako aliokoa Sh300 milioni.

“Nilimwambia JPM amfukuze mkurugenzi, nikamueleza kuhusu mradi fulani, thamani yake ni fulani, nikamwambia huyu mkurugenzi anataka kuwapa watu mara tatu ya thamani ya mradi, akachunguza na kuona ni sahihi, akamfukuza,” anabainisha.

Keissy anasema jambo hilo lilimjengea chuki na wafanyabiashara na makandarasi wa miradi mingi ya maji, ndipo wakamfanyia hujuma ili ang’oke kwenye ubunge.

Akiwa mbunge, Keissy alikuwa karibu na Rais Magufuli na kuwepo na tetesi kwamba, nje ya kazi ni marafiki. Hata hivyo, Keissy anasema hawakuwa marafiki, lakini alikuwa na uwezo wa kumpigia simu moja kwa moja na kumweleza mambo yake.

“Ni kweli, hata nilipokuwa na tatizo, nilimpigia JPM simu moja kwa moja, alipenda utendaji kazi wangu, lakini hatukuwa marafiki,” anasema.

Keissy anasema wakati anahujumiwa, Rais aliambiwa mambo mengi kumhusu yeye, mengine anadai alisingiziwa.

“Sababu zilikuwa ni hizi hizi za kuwabana kwenye miradi ya maji, lakini nikaja kugundua nyuma yao kulikuwa na wakubwa, nilimwambia yote JPM, lakini Mungu alimchukua,” anaeleza Keissy.

Licha ya Katiba kuweka ukomo wa miaka 10 kwa Rais, Keissy alikuwa miongoni mwa wabunge waliompigia debe JPM aongezewe muda wa kukaa madarakani baada ya vipindi vyake viwili vya miaka mitano mitano kumalizika kwa mujibu wa katiba.

Keissy anasema alifanya hivyo kutokana na uongozi wa Hayati Magufuli ambao anadai uliimarisha nidhamu serikalini.

“Nidhamu ilirudi, udokozi ulipungua na waliobainika aliwafukuza hadharani, hakuwa na mchezo na mtu asiye mwajibikaji.

“Hiki ndicho kilinisukuma nimsapoti JPM aongezewe muda, kama utendaji wake ulionekana, kwa nini tusiendelee naye, sema ndiyo hivyo, Mwenyezi Mungu alimchukua,” anasema mbunge huyo wa zamani.

Alivyosotea ubunge miaka 20

Miaka 20 ni umri wa mtoto kuzaliwa, kusoma elimu ya msingi hadi kuhitimu sekondari na kwenda chuo. Kwa Keissy, haikuwa tatizo, hata alipokosa ubunge katika chaguzi nne, anasema hakukata tamaa.

Akieleza harakati zake za siasa, Keissy anasema aliingia kwenye siasa akiwa kampeni meneja wa aliyekuwa mbunge wa Nkasi, Mwani Nsao.

“Wakati huo, hili jimbo halikuwa limegawanywa, Mwani aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Biashara na Viwanda wakati wa Mwalimu Nyerere (Rais wa kwanza), nilikuwa meneja kampeni wake.

“Nilipatia uzoefu huko, alipostaafu ndipo nikaingia kwa kuwa nilishapata uzoefu, niligombea nikashinda, lakini nikafanyiwa mizengwe na kuambiwa mimi sio raia, hicho ndicho kilinikwaza na kuhamia NCCR Mageuzi,” anasema.

Keissy, aliyezaliwa mwaka 1950 huko Nkasi, wakati huo nchi ikiwa ni Tanganyika, anasema baadaye alikwenda TLP, na kisha akaenda Chadema, lakini aliona upinzani Tanzania bado, hivyo akarudi CCM.

JK alivyomuingiza bungeni

Keissy anasema uchaguzi uliofuatia mwaka 2010, akiwa CCM, aligombea na kushinda kwenye kura za maoni.

“Niliambiwa tena sio raia, kama sio JK (Jakaya Kikwete, Rais wa awamu ya nne), mimi nisingekuwa mbunge.

“Nakumbuka wakati wa kutangaza matokeo, katibu CCM Mkoa wa Rukwa alisema mimi ni mshindi, lakini sifai kwa kuwa nahamahama vyama na pia siyo raia,” anasimulia mwanasiasa huyo.

Anasema Rais Kikwete akiwa mwenyekiti wa CCM, alisimama akawauliza: “Nyinyi mnamfahamu vizuri Ally?

“Alihama chama sababu ya vitimbi, mnamsumbua tu, ni raia, hapo ndipo nikapitishwa kugombea ubunge kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka 20, ndipo mwaka 2010 nikaingia bungeni kwa mara ya kwanza,” anasema Keissy.

Akumbuka sakata la Escrow

Katika miaka 10 ya ubunge wake (2010 – 2020), Keissy anasema pamoja na mambo mengi aliyoyafanya, hawezi kusahau sakata la Escrow.

“Escrow iliibua mjadala mkali, ilifika kipindi baadhi ya mawaziri wakajiuzulu, tuliitwa kwenye kamati ya uwekezaji wa mitaji ya umma (PIC), nilisimama nikamtetea Pinda (Mizengo, aliyekuwa Waziri Mkuu).

“Nilisema Pinda hakutajwa, kwa nini ajiuzulu? Mangula ndiye alikuwa mwenyekiti, hoja yangu ikakubaliwa, niliona Pinda hakuhusika kutokana na aina ya maisha yake wote tuliyaona,” anaeleza Keissy.

Licha ya kutorudi bungeni, Keissy anasema amekuwa akifuatilia mijadala inayoendelea bungeni, japo asilimia kubwa ni wabunge wa CCM, lakini wapo wanaozungumza kweli kweli, huku akimtaja mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina.

“Kuna wabunge mle ndani wanasema, mfano ni Mpina, huwa anaibua ishu, ni vema anayoyasema yakachunguzwa kama ni kweli au la.

“Pia, haya yanayoibuliwa na CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) yangetekelezwa kwa haraka, wananchi wangefarijika,” anasema.

Wakati vuguvugu la uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu likiendelea na uchaguzi mkuu mwakani, Keissy anasema mwaka 2025 atarudi na kujitosa kuwania ubunge katika jimbo lake la zamani huko Nkasi.

Anasema wengi wanamshawishi arudi kugombea 2025, hivyo anachokisubiri ni muda ufike ajitose upya kwenye kinyang’anyiro cha ubunge na anasema atagombea jimbo hilo alilofanya maendeleo akiwa mbunge wao kwa miaka 10.

“Nimeondoka na kuviacha vijiji vyote vina umeme, barabara tulipasua njia mpya na kuboresha zile za zamani, tulijenga madarasa, tuliboresha huduma ya maji na maendeleo mengine mengi yalifanyika Nkasi Kaskazini,” anasema.

Anasema bora kuwe na utaratibu wa wanachama wote kuchagua, tofauti na kuwa na wajumbe kadhaa ambao yeye anaona ni rahisi kurubuniwa kwa rushwa.

“Ninachofurahi ni kusikia kuna Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, lakini matamanio yangu ni kwa CCM, hili suala la wajumbe kwenye kura za maoni liondolewe.

“Mchakato ubadilike, wanachama wote wapige kura, hii itasaidia, kwani hata ukitaka kuhonga, huwezi kuwahonga wote,” anasema Keissy, ambaye kwa sasa anaishi Namanyere, Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, akiendelea kufanya shughuli nyingine.

Anavyouzungumzia Muungano

Keissy anasema Muungano huo umekuwa ukiibua hoja mbalimbali kuhusu muundo wake ambapo sasa kuna Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, jambo ambalo Keissy anasema kwake sio sahihi.

“Bora tuwe na Serikali moja ya Jamhuri ya Muungano, lakini hii ya Zanzibar kuwa na Rais wake, bendera yake na wabunge binafsi sioni kama ni sahihi.

“Kwa miaka 60 ya Muungano tulishajua, wapo Wazanzibari wanaishi Bara na watu wa Bara wanaishi kule, tumeoleana na tunafahamiana ipasavyo, wanasema umoja ni nguvu, miaka 60 ni mingi, embu sasa tuwe na mfumo wa Serikali moja katika Muungano wetu,” anasema.

Anasema kwake yeye Serikali moja ni bora, kama inatumika fedha moja haoni tatizo kukiwa na Serikali moja, huku akieleza kumshangaa mbunge aliyesema watumie pasipoti.

Keissy pia ameishauri Serikali ijali kwa upana wake wanyonge, akitolea mfano kwa wakulima na kusisitiza kuna haja Serikali ikanunua mazao kwao na si kuwaacha wafanyabiashara wajipangie bei waitakayo.

“Wanafanya hivi na kumuacha mkulima hafaidiki chochote na jasho lake, hii si sawa, mbona kwa mfanyakazi akilipwa mshahara hapangiwi matumizi? Lakini kwa mkulima ni tofauti, huyu mtu hukumsaidia chochote kipindi anapambana shambani, basi ili kumpa ahueni, mpe bei nzuri,” anasema.

Related Posts