Mahakama kumaliza ubishi nyaraka ya malipo ya mkopo wa Sh26 bilioni Equity

Dar es Salaam. Hatima ya uhalali wa nyaraka iliyopingwa katika kesi ya kibiashara iliyofunguliwa na kampuni ya Continental Reliable Clearing (T) Limited (CRC) dhidi ya Benki za Equity Tanzania na Equity Kenya, itajulikana leo, Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara itakapotoa uamuzi wa pingamizi hilo.

Kampuni hiyo ilifungua kesi hiyo baada ya Benki ya Equity Kenya kupitia wakala wake, Equity Tanzania kuiandikia barua ikiipa siku 21 kurejesha mkopo ambao zilikuwa zimeipatia kwa nyakati tofauti kuanzia mwaka 2013, zaidi ya Dola za Marekani 10.13 milioni (sawa na zaidi ya Sh26 bilioni).

Katika kesi hiyo ya kibiashara namba 16 ya mwaka 2023 inayosikikizwa na Jaji Dk Agatho Ubena, CRC inadai kuwa ilisharejesha mkopo wote na hivyo haina deni kwa benki hizo.

Jana, kampuni hiyo kupitia shahidi wake wa pili, Alexander Johns akiongozwa na wakili wa kampuni hiyo, Frank Mwalongo, iliiomba mahakama hiyo ipokee nyaraka hiyo ambayo ilidaiwa kuwa ni jedwali la malipo ya mkopo wote ambao kampuni hiyo ilipewa na benki hizo.

Hata hivyo mawakili wa benki hizo, Emmanuel Kagali anayeiwakilisha Equity Tanzania na Mpaya Kamala, anayeiwakilisha Equity Kenya walipinga nyaraka hiyo kupokewa wakidai kuwa haijakidhi matakwa ya kisheria.

Pingamizi hilo lililoibua mvutano mkali wa hoja za kisheria baina ya mawakili wa benki hizo waliobainisha zile walizoziita kasoro za kisheria za zinazoifanya nyaraka hiyo isistahili kupokewa na Wakili wa CRC, Mwalongo, akipinga hoja za mawakili hao na kujitetea nyaraka hiyo kuwa inastahili kupokewa.

Mahakama hiyo baada ya kusilikiza hoja za pande zote iliahirisha kesi hiyo mpaka leo Juni 19, 2024 kwa ajili ya uamuzi wa ama kupokea au kuikataa nyaraka hiyo.

Kesi hii ni miongoni mwa kesi kadhaa zilizofunguliwa na kampuni mbalimbali zikipinga kudaiwa na benki hizo na zile zilizofunguliwa na benki hizo dhidi ya kampuni kadhaa zikizidai kampuni mbambali fedha ambazo zikizikopesha mabilioni ya fedha.

Jinsi mawakili walivyochuana

Katika pingamizi hilo, wakili Kagali alidai kuwa nyaraka hiyo ilipaswa iambatanishwe kwenye hati ya madai wakati hati hiyo ilipowasilishwa mahakamani, lakini haikuambatanishwa katika hati hiyo na kinyume cha masharti ya Amri ya 7, Kanuni ya 14(1) ya Kanuni za Mashauri ya Madai (CPC).

Pia alidai kuwa nyaraka hiyo haikuwa imetajwa katika orodha ya viambatanisho vya hati ya madai kinyume cha amri ya 13 (1), (2) ya CPC, wala haikuelezwa katika hati ya madai.

Aliongeza kuwa maneno yaliyomo kwenye nyaraka hiyo yalipaswa kuwemo kwenye hati ya madai lakini kinyume chaka hayamo na kwamba hivyo kuipokea ni kufanya marekebisho ya hati ya madai kwa mlango wa nyuma, hivyo kuwanyima wadaiwa fursa na haki ya kujibu taarifa zilizomo.

Vilevile Wakili Kagali alidai kuwa taarifa zozote zinazoingizwa katika vitabu vya benki zinapaswa kuthibitishwa na afisa wa benki au mbia kama Sheria ya Ushahidi inavyoelekeza.

Alidai kwamba shahidi aliyeomba nyaraka hiyo ipokewe hana mamlaka kwa kuwa hana sifa hizo na kwamba pia uhalisia wake unatia mashaka, kwani haina saini, mhuri wala hakuna kiapo cha mdaiwa yeyote kuthibitisha kuwa imetolewa naye.

“Hivyo haiwezi kuamika katika kuthibitisha marejesho ya mkopo,” alidai wakili Kagali.

Kwa upande wake wakili Kamala naye aliunga mkono hoja za wakili Kagali na kuongeza kuwa nyaraka hiyo ilipaswa kuambatanishwa na hati ya madai iliyofanyiwa marekebisho, iliyowasilishwa mahakamani Juni 26, 2023; lakini iliandaliwa Septemba 8, 2023 baada ya kukamilisha ubadilishanaji wa nyaraka za kesi.

Alidai kuwa ni jambo la hatari kutengeneza ushahidi mpya baada ya kukamilika kwa hatua ya ubadilishanaji nyaraka za kesi.

Alidai kuwa mdai (CRC) alikuwa na fursa ya kueleza sababu kwa nini nyaraka hiyo haikuambatanishwa kwenye hati ya madai, kuorodheshwa katika orodha ya viambatanisho wala kutajwa katika hati ya madai na kupewa ridhaa ya mahakama lakini hakufanya hivyo.

Akijibu hoja hizo, wakili wa CRC, Mwalongo alikiri kuwa kweli nyaraka hiyo haikuambatanishwa katika hati ya madai, lakini akadai kuwa inawasilishwa kama nyaraka za nyongeza chini ya amri ya 13 kanuni ya 1 (1) na (2) ya CPC.

Alidai kuwa kanuni amri na kanuni hiyo inaruhusu nyaraka ambazo hazikuwasilishwa mahakamani sambamba na hati ya madai kutolewa siku ya kwanza ya usikilizwaji wa kesi.

 “Amri hii inawahusu wadaawa wote (pande zote husika katika kesi) yaani mdai na mdaiwa. Mdai ametumia haki hiyo kuwasilisha nyaraka za nyongeza”, alidai wakili Mwalongo.

Wakili Mwalongo alidai kuwa amri ya 13 kanuni ya 1 (1), (2) inapaswa kusomwa pamoja na kwa upatanisho na amri ya 7 kanuni ya 14 (1).

Vilevile alidai kuwa hati ya madai imelezea wazi marejesho ya mkopo huo na kwamba jedwali hilo ni orodha ya malipo yote yaliyofanywa na mdai (CRC).

Alidai kuwa katika ushahidi wake shahidi huyo alieleza kuwa alikusanya taarifa hizo za malipo kutoka katika kalenda mpaka na kwamba shahidi alichagua kuandaa nyaraka hiyo bila kuiambatanisha na hati ya madai.

Wakili Mwalongo alidai kuwa baada ya nyaraka hiyo kuwasilishwa mahakamani Septemba 12, 2023 na wadaiwa kupatiwa nakala Septemba 13, 2023, walikuwa na muda wa kutosha wa miezi tisa kuisoma na kisha kuitumia kumhoji shahidi maswali ya dodoso.

Alidai kuwa nyaraka hiyo ni halisi kwa kuwa mwandaaji amebainishwa, na kwamba nakala halisi imesainiwa, imegongwa mhuri na inaonesha tarehe na kiwango cha malipo.

Pia, alidai kuwa hapakuwa na haja ya kuwepo kiapo cha mdaiwa kuithibitisha na kwamba wakili wa mdaiwa alijielekeza vibaya kudhani kuwa imeandaliwa na wadaiwa, huku akidai kuwa hakuna ushahidi mpya uliotengenezwa.

Wakili Mwalongo alidai kuwa shahidi huyo kuandaa nyaraka hiyo kuna irahisishia kazi mahakama na hata wadaiwa wenyewe na akaiomba mahakama hiyo itupilie mbali pingamizi hilo.

Hata hivyo mawakili Kagali na Kamala walizipinga baadhi ya hoja za Mwalongo, wakidai kuwa amri ya 13 kanuni ya 1 (1), (2) hazipaswi kusomwa kwa pamoja kwani kila moja ina jukumu tofauti.

Wakili Kagali alibainisha kuwa amri ya 13 inazungumzia nyaraka za nyongeza ambazo zinaweza kusaidia hati ya madai katika ulali wa uwezekano na si nyaraka muhimu kama hiyo.

Alisisitiza kuwa nyaraka hiyo ni nyaraka muhimu kwa kuwa ndio msingi wa kesi ya mdai ilipaswa kuambatanishwa na hati ya madai.

Alihitimisha kuwa taarifa za kuthibitisha kutolewa na kurejeshwa kwa mkopo huo kunapaswa zitolewe kwenye taarifa za kibenki na si kwingineko kokote.

Kwa upande wake wakili Kamala naye alisisitiza kuwa amri ya 13, kanuni 1 (1), (2) na amri ya 7 kila moja ina jukumu tofauti na nyingine na kwamba hakuna inayopuuza nyingine.

Alidai kuwa muda wa kutosha kuisoma nyaraka hiyo na kuitumia katika maswali ya dodoso, alidai kuwa maswali ya dodoso na kujibu taarifa za nyaraka hiyo ni mambo mawili tofauti.

Related Posts