Septemba 11, 2023, yalifanyika maadhimisho ya miaka 50 ya kuondolewa madarakani na kuuawa kwa aliyekuwa Rais wa kidemokrasia wa Chile, Salvador Allende. Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA), lilikiri kuhusika na mipango hadi utekelezaji wa mapinduzi hayo.
Septemba 11, 1973, wanajeshi waasi wa Chile, walioongozwa na Jenerali Augusto Pinochet, waliizingira Ikulu ya Chile, iliyopo Santiago, walimpindua na kumuua Allende. Huo ukawa mwanzo wa utawala wa kidikteta. Chini ya utawala Pinochet, Chile ikawa dola ya kipolisi, yaani police state.
Allende alikuwa mjamaa. Na alihakikisha uchumi wa nchi unamilikiwa na Serikali. Hata hivyo, aliruhusu vyama vya siasa kuwa huru. Alipata wakati mgumu kupitisha miswada na mipango mingi ya Serikali ndani ya Bunge, maana alikuwa na wabunge wachache. Allende aliacha Bunge liwe huru.
Ushujaa wa Allende unaweza kugawanywa katika maeneo mawili; demokrasia na usawa. Kwamba chini ya mfumo wa Ujamaa, aliweka mazingira ya watu wote kuwa sawa mbele ya mkate wa taifa. Wanafunzi wa hali zote walisoma bila ubaguzi. Watu walikuwa huru kutoa maoni na kumkosoa.
Mwaka mmoja wa uongozi wake, mambo yalikuwa safi kwa Allende, uchumi ulienda vizuri. Hali za maisha zilikuwa bora. Baada ya Marekani kuiwekea vikwazo Chile kwa sababu ya sera zake za Ujamaa, mambo yalibadilika. Mfumuko wa bei ulipaa hadi kufikia asilimia 140. Hali ya ukuaji wa uchumi ilikuwa hasi.
Baada ya Pinochet kuingia madarakani, miaka saba ya mwanzo uchumi uliimarika na kukua kwa asilimia 10 kutoka hasi. Mfumuko wa bei ulidhibitiwa mpaka asilimia 0. Pamoja na hivyo, Pinochet alilinyamazisha bunge, alitaka yeye pekee ndiye awe msemaji na mwamuzi.
Pinochet pia alifuta shughuli za kisiasa. Vyama vya siasa vikawa taasisi haramu. Watu 40,018 walifungwa kisiasa. Makisio ya Serikali ni kwamba watu 3,095 waliuawa na 1,200 walipotezwa, na alama zao hazijawahi kupatikana.
Chini ya mfumo wa uliberali, matabaka ya vipato yalirejea Chile. Matokeo yake watoto wa maskini walishindwa kumudu gharama za masomo, hasa elimu ya juu, wakati Allende aliweka mteremko katika elimu. Pinochet aliondoka madarakani mwaka 1990 lakini alibaki Amiri Jeshi Mkuu mpaka mwaka 1998. Alifariki dunia mwaka 2006 baada ya kukutana na misukosuko mingi, ikiwemo kufungwa, kuwekwa kizuizini na kadhalika kwa sababu ya makosa aliyofanya akiwa madarakani.
Mwaka 2013 wakati wa maadhimisho ya miaka 40 ya kifo cha Allende, ilioneshwa kuwa kiongozi huyo licha ya kukaa muda mfupi madarakani na kusemwa kwamba aliharibu uchumi, lakini ndiye anapendwa zaidi na Wachile. Pinochet aliyeinua uchumi, kuua mfumuko wa bei na kupandisha Pato la Taifa, Wachile hawataki kumsikia.
Kizazi kipya cha Chile kinamtukuza Allende kwa sababu alikuwa mwanademokrasia na kinambagaza Pinochet kwa udikteta wake. Ni kwa mantiki hiyo, mhariri wa jarida la siasa la The Clinic, Chile, Patricio Fernandez, aliandika makala akisema: “Hiki kizazi kinakumbusha kuwa kuna mambo ni muhimu sana kuliko uchumi.”
Maneno ya Fernandez kuwa kuna mambo muhimu mno kuliko uchumi, ndiyo ambayo nimekusudia kuyatumia kujenga hoja kwenye makala haya. Hadithi ya Allende na Pinochet, shabaha ilikuwa kuitafuta hiyo nukuu ya Fernandez kuwa nchi ina mambo ambayo ni muhimu kuliko uchumi.
Uhuru na demokrasia ni masuala muhimu kabla ya uchumi. Watu huru ndiyo hujenga uchumi mzuri. Maana huwa huru kuhoji, kukosoa, kusahihisha na kujenga uchumi na maendeleo yao. Hivyo, uhuru wa watu na demokrasia, ni mambo yenye kupaswa kutangulia katika taifa kuliko hata uchumi.
Chile wanaishi katika kovu la dola ya kipolisi walilopitia miaka 17 chini ya Pinochet. Gharama ya maumivu na muda walioupoteza chini ya nyakati ngumu za nchi pasipo demokrasia wala uhuru wa watu, hakuna ambaye anaweza kuwafidia leo au angalau kuwapa tathmini halisi ya hasara ya jumla waliyopata.
Yapo mambo muhimu kwenye nchi kuliko uchumi. Ujenzi wa watu kifikra na kuunda taifa la viongozi wenye misingi, hilo ni jambo ambalo linapaswa kupewa kipaumbele, maana ni muhimu kuliko uchumi. Harakati zozote za kujenga uchumi kwenye nchi ambayo haina watu bora ambao wanaweza kuwa viongozi, hilo ni janga.
Uchumi mzuri kwenye nchi isiyo na watu wenye maono mazuri kuhusu nchi, leo na kesho, ni sawa na kujenga ghorofa ndefu bila msingi imara. Inabomoka na kuporomoka wakati wowote, bila kusubiri vimbunga Fred na Hidaya. Taifa lenye watu walioundwa katika misingi bora, ndio ambao siyo tu wanaweza kuipa nchi maendeleo makubwa ya kiuchumi haraka, bali pia kuulinda uchumi wenyewe.
Kuchagua au kuteua viongozi wenye kujua nini maana ya uongozi, ni jambo lenye maana kubwa na muhimu kuliko kukimbilia kujenga uchumi. Huwezi kuwa na wabunge pamoja na mawaziri wanaimba kila uchwao nyimbo za kumsifu na kumtukuza rais, halafu utarajie matokeo makubwa. Nchi inahitaji wabunge imara na mawaziri wanaojua dhima wanayobeba ili hata rais akifanya makosa wamwambie, wamsahihishe.
Mataifa mengi ambayo yameweza kuwa na uchumi unaopanda bila kutetereka kwa miongo mingi, chanzo chake ni aina ya viongozi. Jinsi wanavyotazama mambo, wanavyoyasimamia na wanavyoyatetea. Taifa haliwezi kupiga hatua kwa kuwa na viongozi ambao inapofika awamu yao, hutafuta sifa binafsi badala ya kuitumikia nchi kwa faida ya miongo na karne kadhaa baadaye.
Ona Tanzania leo, maneno ya viongozi kumsifu Rais Samia Suluhu Hassan, hayatofautiani na makundi ya wananchi ambao wanaamini kuingia kwenye kitabu kizuri cha mkuu wa nchi ni kumsifu na kumpamba. Wanaona kufanya kazi bila kupayuka tenzi za kusifu na kupongeza hadi pasipostahili pongezi, hakutatosha kulinda kibarua.
Haya yanasababishwa na dhana kuwa kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa kiongozi ni kuula. Si utumishi wa umma tena. Ndiyo sababu ni lazima kumsifu na kumtukuza ambaye akiamua vinginevyo na ulaji unatoweka. Taifa kuwa na viongozi wenye kutambua wao ni watumishi wa umma na siyo wafanyakazi wa rais, hilo ni muhimu kuliko uchumi.
Ujenzi wa maadili kwa wananchi ni muhimu kuliko uchumi. Taifa lenye watu wasio na maadili, hukaribisha viongozi wasio waadilifu. Nchi yenye mmomonyoko mkubwa wa maadili, hutengeneza dola ya kifisadi. Mafisadi ni kikwazo kikubwa cha maendeleo na kesho njema ya nchi.