Utouh: Changamoto katika ununuzi wa umma tatizo sugu

Dar es Salaam. Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu, Ludovick Utouh amesema bado kuna changamoto katika ununuzi wa umma zinazotakiwa kupatiwa ufumbuzi wa kudumu ili kuleta maendeleo endelevu.

Kutokana na changamoto hizo, Utouh ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Uwajibikaji wa Umma (Wajibu), amesema wameandaa mkutano wa siku mbili utakaofanyika Agosti 6 na 7, 2024 jijini Arusha ili kuwaleta wadau wa ndani na nje ya nchi, kujadili changamoto na kutafuta suluhisho katika ununuzi wa umma.

Mkutano huo ambao ni mfululizo wa mikutano ya kimataifa ya uwajibikaji (ITAC), utakuwa na kaulimbiu ya ‘Kuchochea Mifumo bora ya ununuzi wa umma kwa maendeleo endelevu Afrika’, ikilenga kujadili umuhimu wa mifumo ya ununuzi yenye uwazi na uwajibikaji.

Akiuzungumza na waandishi wa habari leo Juni 19, 2024 Dar es Salaam, Utouh amesema baada ya mkutano wa mwaka jana, washiriki walipendekeza kwa wingi ununuzi wa umma ujadiliwe.

“Tulipochamba maoni ya washiriki tuliona kwamba ununuzi wa umma umejadiliwa zaidi. Hata ukisoma ripoti ya CAG na ripoti za PPRA (Mamlaka ya Ununuzi wa Umma) na ripoti za Wajibu kuhusu sheria za rushwa, utaona suala la ununuzi liko juu sana,” amesema.

Amesema kuonyesha kuwepo kwa changamoto hizo, Serikali imekuwa ikibadilisha mifumo ya ununuzi.

“Awali tulikuwa na mfumo wa ununuzi unaoitwa TANePS (Tanzanian National e-Procurement System) lakini haukuleta mafanikio, ndipo ikaleta mfumo mwingine unaoitwa NeST (National e-Procurement System of Tanzania) ambao umeanza mwaka jana.

“Zote hizo ni hatua za Serikali kuitafuta njia za kutatua matatizo yaliyokithiri ya ununuzi,” amesema.

Amesema kwa kuwa mkutano huo ni wa kimataifa wamewashirikisha wadau ikiwamo PPRA, Wizara ya Fedha na taasisi za kimataifa kutaka mjadala zaidi katika suala la ununuzi wa umma.  

Awali akielezea mada zitakazowasilishwa kwenye mkutano huo, Meneja wa programu wa Wajibu, Moses Kimaro amesema kutakuwa na mada tano ambazo ni pamoja na Matumizi ya mbinu za kisasa kwenye ununuzi wa umma ili kuzuia rushwa, Uwazi unaoendeshwa na teknolojia: Kuhuisha michakato ya ununuzi kiuelektroniki.

“Kutakuwa na mada ya mchango wa ubia kati ya sekta binafsi kwenye kuimarisha ufanisi na uwajaibikaji katika mchakato wa ununuzi, Maarifa juu ya viwango vya mabadiliko ya kimataifa kwenye ununuzi wa umma na Nafasi ya wadau wasio wa Serikali katika kuimarisha usimamizi kwenye michakato na taratibu za ununuzi wa umma,” amesema.

Related Posts