USHINDI wa bao 1-0 iliyopata JKU mbele la waliokuwa watetezi wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), KMKM imewafanya vinara hao wa ligi hiyo kulishikilia taji kwa mkono mmoja na hii ni baada ya Zimamoto kulazimishwa sare ya 1-1 na Mlandege mechi zilizopigwa jana mjini Unguja.
JKU iliyotemeshwa taji la michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) kutokana na kufanya fujo katika pambano la fainali dhidi ya Chipukizi ya Pemba, ilipata ushindi huo muhimu kwenye Uwanja wa Mao A na kuifanya ifikishe pointi 65 na sasa inahitaji pointi moja tu kutangaza ubingwa.
Sare ya Zimamoto iliyopata kwenye Uwanja w Mao B, imeitibulia timu hiyo iliyokuwa ikiifukizia JKU, kwani ili itwae ubingwa huo katika mechi za kufungia msimu zitakazopigwa wikiendi hii ni lazima yenyewe ishinde na JKU ifungwe na kubebwa na uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.
JKU imefunga mabao 44 na kufungwa 22 wakati Zimamoto yenye pointi 62 imefunga mabao 51 na kufungwa 21 ikiwa na wastani mzuri unaoweza kuinyang’anya JKU tonge mdomoni katika mechi za wikiendi iwapo itaibuka na ushindi mbele ya New City, huku JKU ipoteze kwa maafande wenzake wa Kipanga.
Katika mechi ya juzi bao pekee la JKU liliwekwa kimiani na Saleh Masoud Abdulla dakika ya 33 na kuikamili KMKM iliyokuwa ikishikilia taji hilo kwa misimu mitatu mfululizo msimu huu kutoka kapa kwani iling’olewa mapema kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho.
KMKM sasa imesaliwa na pointi 54 ikisaliwa na mechi moja ya kufungia msimu dhidi ya Mlandege.
Katika mechi nyingi zilizochezwa pia jana jioni, Zimamoto na Mlandege zilishindwa kutambiana kwa kutoka sare ya 1-1, huku Maluindi na New City zikitoka suluhu kwenye Uwanja wa Amaan B.
Zimamoto iliyokuwa ikisaka ushindi ili kuzidi kuibana JKU ili shtukizwa kwa kwenda mapumziko ikiwa nyuma kwa bao 1-0 lililowekwa na Bakar Nassor Bakari dakika ya 45 kabla ya kuzinduka dakika za lala salama ilipowasawazisha kupitia Ibrahim Hamad ‘Hilika’.
Hilika aliyerejea katika Ligi hiyo akitokea kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars alifunga bao dakika ya 85 likiwa ni la 16 kwake akipunguza pengo la mabao na kinara Suleiman Mwalim Abdallah wa KVZ mwenye mabao 20.
Sare hiyo kwa Mlandege imeifanya ifikishe pointi 37 ikisaliwa nafasi ya tisa, huku sare ta Malindi na New City zimezifanya timu hizo pia kusalia nafasi zilizokuwapo, licha ya kuongeza pointi moja kila moja.
Malindi ipo nafasi ya 10 ikiwa na pointi 36, huku New City 34.
Katika mechi nyingine za kukamilisha raundi ya 29 ya ligi hiyo, Chipukizi na Jamhuri zilizotoka sae ya 1-1 kwenye Uwanja wa FFU Finya, kisiwani Pemba, huku Kipanga na Mafunzo zikitunishiana misuli ka kufunga mabao 3-3 kwenye Uwanja wa Mao, mjini Unguja.
Mwinyi Hassan aliitanguliza Mafunzo kwa bao la dakika ya 45 na kudumu hadi wakati wa mapumziko.
Kipindi cha pili Kipanga ilikuja na kasi na kuchomoa bao hilo dakika 51 lililofungwa a Mansour Kombo kisha kuongeza jingine la pili dakika 54 lililofungwa na Amour Mohammed, hata hivyo Mafunzo ilizinduka na kufunga bao la pili la kusawazisha kupitia Rashid Abdallah dakika ya 63 kabla ya James Msuva kuongeza la tatu dakika ya 68.
Bao hilo la mdogo wa nyota wa kimataifa ya Tanzania anayecheza Saudia, Simon Msuva lilidumu kwa dakika mbili tu, kwani William Patrick aliisawazishia Kipanga bao dakika ya 70 na kufanya matokeo hayo kudumu hadi ilipolia filimbi ya mwisho kuashiriki kumalizika kwa pambana hilo.