Vyanzo vya mapato bajeti ya SMZ vyakosolewa

Unguja. Mwakilishi wa Mtambwe, Dk Mohamed Ali Suleiman amesema bajeti ya Serikali imekosa vyanzo vipya vya mapato, badala yake imeongeza kodi, hivyo kuitaka kuangalia upya jambo hilo.

Amesema hayo alipochangia mpango wa maendeleo na bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/25 katika mkutano wa 15 wa Baraza la Wawakilishi, Chukwani Zanzibar Juni 19, 2024.

“Ukiangalia bajeti hii hakuna jipya, maeneo ni yaleyale badala yake Serikali imechukua vyanzo vilevile vya zamani imeongeza kodi, kwa kweli inasikitisha zaidi hakuna ubunifu wa kuandaa vyanzo vipya, badala yake itaendelea kuumiza wananchi wa hali ya chini na kuwa tegemezi,” amesema Dk Suleiman.

Pia, ametoa mfano wa mapendekezo ya Serikali kuongeza tozo katika kilo moja ya nyama na samaki wanaotoka nje ya nchi kutoka Sh100 hadi Sh300 akisema imelenga kuwaumiza wananchi wa hali ya chini.

“Hii ni tozo kubwa sana, wananchi wengi wa Zanzibar wanategemea vitoweo hivi, leo hii ukiongeza kodi kubwa kiasi hiki unataka kumkoamoa mwananchi na wala siyo kumsaidia mnyonge,” amesema Dk Suleiman.

Amesema baada ya kupitisha kiwango hicho, kilo moja ya kuku itauzwa zaidi ya Sh10,000 tofauti na Sh6,000 za awali.

Dk Suleiman amesema licha ya Serikali kusema inataka kulinda soko la ndani, bado Zanzibar haijawa na biashara ya kuku wanaoweza kutosheleza mahitaji bali wanataka kuwaumiza wananchi, hivyo wangeanza kuweka mikakati inayosaidia soko lijitosheleze.

Amesema eneo hilo linaajiri vijana wengi wanaouza samaki na chipsi kuku, hivyo kiwango kuongezeka kinakwenda kuharibu ajira za vijana na kutengeneza kundi litakalokosa ajira na kuanza kuhangaika.

Amezungumzia kupandisha kodi kwenye vinywaji, akisema wamesahau sehemu kubwa ya kutafuta kodi katika michezo ya kubeti.

Mwakilishi huyo amesema licha ya kudai tamaduni Zanzibar haziruhusu, lakini wapo watu wanaondesha kinyemela michezo hiyo, hivyo ni vyema Serikali ikaangalia utaratibu mpya wa kuirasimisha michezo hiyo na ikusanye kodi kubwa.

“Hata vinywaji, hii mivinyo utamaduni hauturuhusu lakini tunaingiza, kwa hiyo imefika wakati sasa hata hii michezo ya kubeti iruhusiwe Serikali ikusanye kodi, kuna mapato mengi yanapotea kwa sababu hata kama haturuhusu kuna watu wanafanya biashara hiyo hapa Zanzibar kinyemela,” amesema.

Kuhusu kodi za miundombinu ambazo Serikali imependekeza kutoza kwa dola badala ya shilingi, amesema atasikitika iwapo baraza litaruhusu jambo hilo kwa kuwa ni kuvunja sheria za nchi makusudi.

Dk Suleiman  amesema kutoza kodi kwa dola ni kuendelea kuishusha thamani fedha ya Tanzania wakati ni suala linalopigiwa kelele kuhakikisha fedha hiyo inapandishwa thamani.

Amesema hata Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kifungu cha 26 inaelekeza huduma zote nchini kutolewa kwa fedha za Kitanzania lakini waziri kwa makusudi anataka kuvunja sheria hiyo.

Amesema bado kuna kodi kubwa inapotea katika sekta ya utalii, akieleza takwimu za watalii wanaoingia haziendani na makusanyo halisi katika sekta hiyo.

“Mfano tunasema watalii 600,000 wameingia na kiwango cha makusanyo Sh18 bilioni, hizi takwimu hazina uhalisia kwa hiyo tunatakiwa kuziba mianya ya wizi. Bado kuna wizi mkubwa katika sekta hiyo,” amesema Dk Suleiman.

Ameshauri kuweka mifumo mizuri na kuondokana na mifumo ya zamani, akisema kodi ya kulala mgeni isilipwe kwenye hoteli badala yake mtalii ailipe pale anaposhuka kwenye ndege au bandarini kuepusha mapato kupotea.

Mwakilishi wa Kikwajuni, Nassor Ahmed Jazila amesema lazima Serikali iendelee kutoa kipaumbele kwa uwekezaji ili ikusanye kodi kubwa husuani katika visiwa vidogo.

Amesema utawala bora, uwajibikaji na kudumisha amani na utulivu, ni chanzo cha kukua kwa uchumi wa Zanzibar, hivyo hakuna budi kuendeleza mambo hayo.

“Serikali imefanya kazi kubwa katika sekta hii ya kujenga viwanja vya ndege na kuboresha masuala ya umeme na maji kufikia malengo tuliyokusudia,” amesema.

Fatma Ramadhan Mandomba, mwakilishi wa viti maalumu amesema ipo haja kwa Serikali kuangalia misamaha ya kodi wanayotoa kama ina tija au la, isije kuwa inapoteza kodi nyingi kwa misamaha ambayo haina manufaa kwa Taifa.

Ameshauri wawekezaji wanapokuja kuwekeza katika visiwa hivyo waje na vyanzo vyao vya umeme jambo litakalopunguza msongamano wa mahitaji ya nishati hiyo.

Kuhusu mikopo ya asilimia 10 amesema haijawanufaisha wanawake, hivyo Serikali iangalie namna ya kuliweka vyema jambo hilo.

Mwakilishi Aza Januar Joseph amezungumzia kilimo akisema kinatakiwa kupewa kipaumbele kwa kuwa hakijakidhi mahitaji ya chakula licha ya kuweka miundombinu mingi ila haijaleta tija.

“Kuna tani za kwenye vitabu kwamba tunapata bidhaa lakini tukienda sokoni hakuna kitu tunapata, sioni mchele wa Zanzibar unauzwa katika masoko yetu na vitu vingine vinalimwa lakini hatuvioni Zanzibar,” amesema Aza.

Amesema kwenye masoko yanayojengwa kuwe na eneo maalumu la bidhaa hizo ili wananchi wazipate kwa urahisi.

“Mkulima akilima akapata sana anapata magunia matano, hayatoshelezi. Hizi taarifa za kwenye vitabu zionekane hata kwenye masoko mitaani, tusisubiri kwenye sherehe za nane nane kuonyesha tu,” amesema.

Amesema ni vyema kuangalia mfumo unaotozwa kodi kwenye hoteli kwa kuwa bado mapato yanapotea zaidi.

Mwakilishi wa Paje, Dk Soud Nahoda amesema Serikali imejitahidi kuboresha huduma kwa kujenga shule na hospitali, hivyo kuwapunguzia wananchi kusafiri umbali mrefu kupata huduma hizo.

Related Posts