MICHUANO ya Kombe la Mataifa ya Ulaya (Euro 2024) yalianza wiki iliyopita na kushuhudia michezo mikali ikipigwa na jana raundi ya pili ya hatua ya makundi ilianza.
Wenyeji wa michuano hiyo ngazi ya mataifa, Ujerumani ilicheza djhidi ya Hungary na Scotland ilicheza dhidi ya Switzerland kundi A, huku kundi B ulipigwa mchezo mmoja na Croatia ilicheza dhidi ya Albania.
Fainali hizi zimekuwa za aina yake miaka ya nyuma na moja ya mambo ya kukumbukwa ni kwa wachezaji kuwakilisha nchi tofauti kwenye michuano tofauti.
Michuano ya mwaka huu jambo hilo halijatokea tofauti na miaka ya nyuma na ilikuwa ni kawaida mchezaji kuliwakilisha taifa lingine na kuna waliochezea mataifa mawili hadi matatu tofauti.
Ilikuwa hivyo hasa kwa nchi za Ulaya na Amerika ya Kusini na chache kwa Afrika na iliwahi kujitokeza katika nchi za Afrika Mashariki kwenye mashindano ya Kombe la Gossage na yale ya Chalenji 1967.
Miongoni mwa wachezaji mashuhuri wanaotajwa kuvaa jezi za timu za taifa zaidi ya moja ni:
. Diego Costa aliyeichezea Brazil alikozaliwa na baadaye kuchukua uraia wa Hispania na kuchezea timu ya nchi hio.
. Enrique Guaita, baada ya kuchezea timu ya kwao Argentina alijiunga na Roma 1933 na baadaye Racing Club za Italia, akachukua uraia na kuvaa jezi ya Italia katika fainali za Kombe la Dunia za 1934.
Alirudi Argentina 1936 na kuchukua tena uraia wa nchi hiyo na kuichezea Argentina.
. Nacer Chadli – Ni mzaliwa wa Ubelgiji aliyeichezea nchi hiyo na baadaye kuchukua uraia wa Morocco walikotoka wazazi wake na aliichezea nchi hiyo mwaka 2010, akiwa na miaka 21.
Baadaye alirudi Ubelgiji na kuchukua tena uraia na kuchezea timu ya nchi hiyo.
. Jermaine Jones – Alizaliwa Frankfurt, Ujerumani, baba yake akiwa ofisa wa Jeshi la Marekani na alikuwa huru kuchukua uraia alioupenda.
Baada ya kuichezea Ujerumani mwaka 2008 alikwenda Marekani na kuichezea timu ya taifa ya nchi hiyo.
. Raimundo Orsi – Huyu ni mzaliwa wa Argentina na aliwahi kuwemo katika kikosi cha taifa cha nchi hiyo katika michezo kadha ya kimataifa.
Hata hivyo, baadaye aliamua kuchukua uraia wa Italia na kuichezea nchi hiyo katika fainali za Kombe la Dunia za 1930 na 1934.
. Josef Bican alikuwemo katika kikosi cha Ujerumani cha miaka ya 1930 na kuhamia Czechoslovakia 1939 alikochukua uraia na kuichezea timu ya nchi hiyo.
. Thiago Motta – Huyu ni mzaliwa wa Brazil aliyeng’ara alipokuwa na klabu za Barcelona, Atletico Madrid, Genoa, Inter Milan na PSG kuanzia mwisho wa miaka ya 1990 hadi 2012.
Kwanza alikuwa na kikosi cha Brazil, lakini baadaye alipochukua uraia wa Italia alichezea taifa hilo.
. Darko Pancev – Alizaliwa Yugoslavia na alikuwa mfungaji bora wa Ulaya 1991.
Baada ya kuichezea Yugoslavia kwa miaka michache alikwenda Ujerumani, akabadili uraia akiwa na Bayern Munich na kuwemo katika kikosi cha taifa cha nchi hiyo.
. Juan Alberto Schiaffino – Alisifika kama mchezaji nyota wa Uruguay iliyoshinda Kombe la Dunia 1953.
Aliondoka Uruguay mwaka 1954, akiwa na miaka 23 na kwenda Italia kujiunga na AC Milan na alichukua uraia na kuichezea timu ya nchi hio.
. Ferenc Puskas- Siyo rahisi kuzungumzia soka nchini Hungary bila ya kumtaja Puskas.
Kutokana na hali ya kisiasa Hungary alikwenda ughaibuni. Puskas alikwenda Hispania, akachukua uraia wa nchi hiyo na kujiunga na Real Madrid na kuichezea Hispania kwa miaka michache kabla ya kustaafu.
. Alfredo Di Stefano – Huyu anahesabika kama kiumbe wa aina yake katika historia ya soka kwa kucheza kama mshambuliaji, kiungo, mlinzi na hata kipa.
Mara nyingi, Di Stefano aliyezaliwa Argentina, alipokuwa mshambuliaji aliamua kuwa kipa timu yake ilipopigiwa penalti na ilikuwa sio rahisi kumfunga na alikuwa mfungaji mzuri wa penalti.
Di Stefano alipotofautiana tu na kocha, alihama nchi na kila alipokwenda alichukua uraia.
Alizichezea Argentina, Colombia na Hispania na zote alizifungia mabao. Aliifunga Argentina mabao sita, Colombia saba na Hispania 23. Alikuwa mchezaji bora wa Ulaya mara mbili.
. Luis Monti – Aliziwakilisha nchi mbili katika michezo ya fainali wa Kombe la Dunia, Argentina alipozaliwa na baadaye Italia alikohamia miaka ya 1930.
Visa kama nilivyovieleza vya wachezaji kubadili uraia na kuwa katika vikosi vya taifa vya zaidi ya nchi moja vilikuwepo Afrika ya Mashariki miaka ya nyuma.
Tofauti ni nchi za Afrika ya Mashariki zilikuwa makoloni ya Uingereza na hivyo ilikuwa kawaida wachezaji kuhamia nchi nyengine, lakini hii ilikuwa zaidi kwa wachezaji wa Kenya na Uganda.
Kila mashindano ya Kombe la Gossage yalipokaribia miaka ya 1950 na mwanzoni mwa miaka ya 1960 ilikuwa tabu kutabiri baadhi ya wachezaji wangechezea Kenya au Uganda.
Miongoni mwa wachezaji mashuhuri ninaowakumbuka wakati wa utoto wangu katika miaka ya 1950 kutoeleweka wangechezea Kenya au Uganda katika mashindano hayo walizichezea klabu za Uganda.
Miongoni mwao ni Edward Kalibala (Engineer), Stephen Mariadua, Gilbert Sseruage na kipa John Argard.
Hata pandikizi la jitu aliyekuwa mlinzi maarufu wa Uganda, Francis Jogoo baadaye alikwenda kwao Kenya na kuichezea timu ya taifa ya nchi hiyo.
Tanganyika nayo ilipata wachezaji wachache kutoka nchi jirani. Miongoni mwao ni William Nahason Ongweya (alijulikana zaidi kwa jina la Nason).
Huyu ni mzaliwa wa Kisumu, Kenya na alikuja Mwanza akiwa karani wa kazi, akiwa na shirika la Afika Mashariki la Reli na Bandari. Alichezea timu ya Tanganyika mwaka 1950.
Mchezaji huyu aliyekuwa na chenga za maudhi aliisaidia Tanganyika kuifunga Kenya 3-2 na kubeba Kombe la Gossage katika mashindano yaliyofanyika Zanzibar mwaka 1951.
Katika mchezo ule wa fainali magavana wote watatu wa Uingereza, Sir Edward Twinning (Tanganyika), Sir Andrew Cohen (Uganda)} na Si Evelyn Baring (Kenya) na mfalme Seyyid Khalifa wa Zanzubar walivutiwa sana na mchezo wake.
Nyimbo nyngi zilitungwa kumsifu Nahashonna iliotia fora ni ile aliyoimba mpia gitaa maarufuwa zama zile W.W.Witts (Owiti) wa Kenya ambayo ilihadithia namna ambavyo mchezaji huyu alivyotambaa na mpira hadi golini.
Baada ya kustaafu akiwa na Shirika la Reli Nahashon na baada ya kustaafu mwanzoni mwa miaka ya 1960 akiwa na Shirika la Reli
aliendelea kuishi Tanganyika.
Nilikutana naye Mwanza mwishoni mwa miaka ya 1970 akiwa kipofu na hali mbaya ya maisha na kusikitika ulimwengu wa soka haukumsaidia na hakuna aliyejali mchango wake kwa timu ya Tanganyika. Alifariki dunia mwanzoni mwa miaka ya 1980 na maiti yake kupelekwa Kisumu kwa mazishi.