Ramaphosa aapishwa kuanza muhula wa pili Afrika Kusini – DW – 19.06.2024

Halfa ya taifa ya kumwapisha Ramaphosa imefanyika kwenye mji mkuu wa serikali ya nchi hiyo Pretoria na kuhudhuriwa na viongozi wa mataifa kadhaa ya Afrika.

Kiapo cha urais kiliongozwa na Jaji Mkuu wa Afrika Kusini Raymond Zondo mbele ya majengo ya Ikulu ya nchi hiyo. Mfalme Mswati III wa Ufalme wa Eswatini, Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, Bola Tinubu wa Nigeria na Emerson Mnangagwa wa Zimbabwe ni miongoni  viongozi na wageni mashuhuri waliohudhuria hafla ya kuapishwa Ramaphosa.

Baada ya kula kiapo Ramaphosa alipigiwa mizinga 21 ya heshima na kulikuwa vilevile na onesho la ndege za kivita zilizoruka kupita juu ya majengo ya Ikulu.

Wanamuziki wa Afrika Kusini na vikundi vya ngoma za asili navyo viliwatumbizwa maelfu ya watu waliohudhuria halfa hiyo.

Ahadi za mageuzi zawatawala hotuba ya kwanza ya Ramaphosa baada ya kiapo 

Ramaphosa anaanza muhula wa pili akiwa amedhoofika kisiasa baada ya kulazimika kuungana na vyama vingine kuunda serikali baada ya chama chake kupoteza wingi mkubwa wa viti bungeni.

Gwaride la heshima wakati wa halfa ya kuapishwa Rais Cyril Ramaphosa mjini Pretoria
Gwaride la heshima wakati wa halfa ya kuapishwa Rais Cyril Ramaphosa mjini Pretoria.Picha: Phill Magakoe/EPA

Hiyo inakuwa ni mara ya kwanza kwa ANC kushindwa kuunda chenyewe serikali kufuatia matokeo mabaya iliyoyapata katika uchaguzi uliofanyika mwezi uliopita.

Katika hotuba yake kwa taifa baada ya kula kiapo, Rais Ramaphosa ameahidi kwamba serikali yake ya umoja wa kitaifa itafanya kazi ya kuboresha hali za maisha ya watu wa Afrika Kusini.

Amesema kupitia uchaguzi uliopita umma wa nchi hiyo umetuma ujumbe wa kuwataka wanasiasa waache mchezo wa kutupiana mpira wa lawama na badala yake watimize wajibu wao.

“Kwa kutambua kwamba hakuna chama kinachoweza kutawala au kutunga sheria chenyewe, vyama vyetu vimekubaliana kufanya kazi kwa ushirika, kuunganisha vipaji vyetu kwa maslahi ya nchi na maendeleo ya watu wake. Kwa pamoja, vimekubaliana kuunda serikali ya umoja wa kitaifa kusukuma mbele ajenda ya mabadiliko ya msingi na ya kudumu. Kuundwa serikali hiyo ya umoja ni wasaa wenye manufaa makubwa. Ni mwanzo wa enzi mpya,” amesema kiongozi huyo. 

Kazi ya kuunda serikali inaanza chini ya kiwingu cha upinzani wa Zuma na Malema

Mmoja wa raia wa Afrika Kusini waliohudhuria halfa ya kuapishwa Rais Cyril Ramaphosa
Mmoja wa raia wa Afrika Kusini waliohudhuria halfa ya kuapishwa Rais Cyril Ramaphosa. Picha: Jerome Delay/AP/picture alliance

Kumekuwa na maoni mseto nchini Afrika Kusini kuhusu serikali mpya itakayoundwa ambayo inadhihirisha kutetereka kwa chama cha ANC kilichopigania kukomeshwa utawala wa wazungu wachache na sera ya ubaguzi wa rangi hadi mwanzoni mwa miaka 1990.

Ama kuhusu matarajio ya raia wa nchi hiyo, mmoja ya waliohudhuria halfa ya kuapishwa Ramaphosa amesema:

“Shauku yangu kubwa ni moja tu: ni kuona rais anakuwa mwaminifu. Uaminifu, hakuna la ziada, Wanasiasa kuweni waaminifu. Msicheze na maisha ya raia wa Afrika Kusini kwa sababu siku zinazokuja, hawataweza kustahamili.”

Baada ya kiapo Ramaphosa anatarajiwa kutangaza baraza jipya la mawaziri litakalokijumuisha chama cha pili kwa ukubwa nchi hiyo cha Democratic Alliance na vingine vidogo vilivyojiunga na ANC kuunda serikali.

Ingawa ametumia hotuba yake kutoa matumaini ya kushughulikia matatizo ya umma wa Afrika Kusini kuna wasiwasi mivutano na tofauti za kisera baina ya vyama washirika inaweza kuzitia ganzi juhudi hizo.

Kuna tofauti kubwa za kimatazama baina ya ANC na chama cha DA mathalani katika kushughulikia tatizo la ukosefu umeme linaloikabili nchi hiyo au hata mgawanyo wa rasilimali za taifa katika nchi ambayo pengo baina ya mabwenyenye na makabwela na kubwa kupindukia.

Na kuna kizingiti kingine, nacho ni upinzani kutoka vyama viwili vikubwa kile kinachoongozwa na rais wa zamani Jacob Zuma cha uMkhonto weSizwe na kingine cha Economic Freedom Fighters kinachoongozwa na mwanasiasa machachari Julius Malema.

Vyote viwili vimekataa kujiunga ndani ya serikali ya umoja wa kitaifa na vimeapa kuitia jakamoyo serikali ya Ramaphosa ndani na nje ya bunge.

Related Posts