Wafungwa, mahabusu walioko magerezani kusajiliwa Nida

Dodoma. Serikali itaanza kusajili vitambulisho vya Taifa kwa wafungwa na mahabusu walioko magerezani katika mwaka 2025/26.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo amesema hayo leo Juni 19, 2024 wakati wakijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Asia Halamga.

Asia amehoji Serikali ina mpango gani kuwapa vitambulisho vya Taifa wafungwa pamoja na mahabusu.

Akijibu swali hilo, Sillo amesema utaratibu wa kusajili na kutambua watu waliopo katika makundi maalumu wakiwemo wafungwa na mahabusu ni kupitia maombi maalumu kutoka kwa wakuu wa gereza katika wilaya husika.

Amesema uratibu wa usajili wa makundi hayo unafanywa na Mamlaka ya Vitambusho vya Taifa (Nida), kupitia wakuu wa Magereza na maofisa usajili wa wilaya husika.

Amesema kwa kuwa baadhi ya wafungwa na mahabusu wamekwishakusajiliwa walipokuwa uraiani kabla ya vifungo vyao, Nida ipo tayari kufanya usajili na utambuzi kwa watu wote waliokidhi vigezo kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza.

Amehoji ni lini zoezi la utambuzi wa wafungwa litaanza kwa kuwa wafungwa waliokaa muda mrefu magerezani wanapotoka wanapata adha ya kupata huduma.

Akijibu swali hilo, Sillo amesema ni kweli haki ya msingi ya kila raia kupata kitambulisho na Serikali iko tayari kuwasajili wafungwa na mahabusu walioko magerezani.

“Kuhusu lini utaanza mheshimiwa mwenyekiti usajili huo utaanza mwaka 2025/26,” amesema.

Katika maswali ya yongeza, Mbunge wa Arumeru Magharibi, (CCM), Noah Lembris amehoji ni lini Serikali itawapa vitambulisho wakazi wa jimbo lake ambao wamepewa namba za utambulishi (NIN) kwa muda mrefu na hawaelewi hatima yao.

Akijibu swali hilo, Sillo amesema kuanzia Oktoba mwaka 2023 wametengeneza vitambulisho vya kutosha na kuagiza Msajili wa NIDA katika Wilaya ya Arumeru ahakikishe anapeleka vitambulisho vyote vya wananchi waliosajiliwa.

Related Posts