Dk Mpango aeleza ya kukumbukwa kwa RAS Kilimanjaro

Moshi.  Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema Serikali imepata pigo kubwa kwa kuondokewa na aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Tixon Nzunda aliyefariki dunia Juni 18, 2024 kwa ajali ya gari, huku akieleza alikuwa mtu makini katika utendaji kazi.

Nzunda (56) na dereva wake Alphonce Edson (54) walifariki dunia jana Juni 18, 2024 kwa ajali ya gari iliyotokea saa 8.30 mchana eneo la Njiapanda ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) alipokwenda kumpokea, Dk Mpango aliyekuwa akielekea mkoani Arusha kikazi.

Dk Mpango amesema alikuwa mtumishi wa umma mwadilifu, mwenye hofu ya Mungu, ambaye ameacha mfano mzuri katika utendaji kazi, akitaka watumishi wengine kuiga mfano wake.

“Alikuwa mtumishi wa umma mwadilifu, nadhani kilichobaki kwa watumishi wa umma ni kuiga uadilifu katika kuwatumikia wananchi na kila mara tutangulize hofu ya Mungu,” amesema Dk Mpango.

“Kwetu ametuachia mfano mkubwa, kila tukiwa naye katika nafasi zake mbalimbali, ninamkumbuka vizuri nikiwa Waziri wa Fedha nilikaa naye akiwa Ofisi ya Waziri Mkuu kwenye vikao vyetu vya utatu na wafanyakazi,” amesema.

“Rais yupo safarini nje ya nchi nasema poleni, lakini pia niwashukuru kwa moyo wenu tangu tukio lilipotokea mmekuwa pamoja na familia hii, ndiyo Utanzania ninaoufahamu.”

Dk Mpango amewataka viongozi kuishi vizuri na watu wawapo kazini, majirani na marafiki ili utakapoondoka duniani ukumbukwe kwa mema uliyoyatenda.

“Kilicho muhimu na sisi tujiandae kwa sababu hatujui siku yetu itafika lini, tumwombe Mungu na sisi atufundishe kuzijua saa zetu kuishi vyema kazini, na majirani na marafiki ili tutakapoondoka angalau basi tupate watu wa kutusindikiza, wakinena mema tuliyotenda kwa ajili ya familia zetu, marafiki zetu na Taifa letu,” amesema.

Alivyopokea taarifa za ajali

“Nilishtuka kidogo kwa sababu jana niliondoka nyumbani saa tisa sikuwa nimepata habari yoyote, kwenye saa 9.30 nikawa nimefika Uwanja wa Ndege Dodoma ndipo nilipoarifiwa kwamba mwenzetu ametangulia kupitia ajali pale karibu na KIA alikuwa anakuja kunipokea ni jambo gumu kweli,” amesema.

Kuhusu dereva, Dk Mpango amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu kufikisha salamu za pole kwa familia kwa niaba ya Rais na yeye mwenyewe.

“Natamani ningefika lakini majukumu ndiyo hivi, bila shaka RC atakwenda kumwakilisha Rais lakini na mimi mwenyewe katika msiba huo na kama Serikali tutafanya kila linalowezekana kuhakikisha ndugu zetu hawa waliolitumikia Taifa kwa uaminifu tunawapumzisha,” amesema.

Mwili wa Nzunda utaagwa Juni 20, 2024 mkoani Kilimanjaro na kusafirishwa kwenda Dar es Salaan na maziko yatafanyika mkoani Songwe.

Akitoa ratiba ya mazishi, Babu amesema mwili utaagwa nyumbani kwake na baadaye kusafirishwa kupelekwa Goba, Dar es Salaam na Ijumaa utapelekwa Songwe kwa maziko yatakayofanyika Jumamosi.

Amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa ndege ya Serikali kwa ajili ya kusafirisha mwili hadi Dar es Salaam.

“Mwili utaletwa nyumbani saa nne asubuhi ukitokea Hospitali ya KCMC, kutakuwa na ibada na baadaye wananchi kupata fursa ya kuaga mwili wa marehemu,” amesema.

Amesema saa 10.00 jioni mwili utasafirishwa kwenda Dar es Salaam ambako utalala nyumbani Goba.

Kuhusu dereva, amesema wamekubaliana na familia maziko yatafanyika Jumatatu Juni 24, 2024 eneo la Kahe, Wilaya ya Moshi.

“Tumeongea na familia, naye ni mkazi wa Mbeya lakini ameishi huku muda mrefu, hivyo maziko yatafanyika Jumatatu hapa Moshi, mkoani Kilimanjaro, baada ya kumzika Katibu Tawala, tutarudi kwa maziko yake,” amesema.

Related Posts