Miili sita ya wahamiaji yaopolewa baharini

Roma, Italia. Walinzi wa pwani ya Italia wamesema wameopoa miili sita baada ya boti ya wahamiaji kuzama wiki hii kwenye pwani ya Kusini ya Bahari ya Mediterania, huku zaidi ya watu 60 wakiripotiwa kutoweka wengi wao wakiwa ni watoto.

Shirika la Habari la AFP limesema watu 12 wameokolewa baada ya mashua hiyo kuzama karibu maili 120 kutoka pwani ya Calabria, usiku wa Jumapili na inadaiwa mmoja wao alikufa baada ya kuteremka.

Hivyo, walinzi wa pwani wamesema leo Jumatano Juni 19, 2024 wameendelea kupekua eneo karibu na mashua iliyozama, ambayo bado inaonekana, baharini na angani.

“Kufuatia upekuzi uliofanywa hadi sasa, miili ya watu sita zimepatikana”.

Taarifa zaidi za shirika hilio zimesema kati ya miili hiyo sita iliyopatikana ni wanaume wanne na wanawake wawili.

Vilevile, Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) limekuwa likiwasaidia manusura, ambao waliripoti kuwa watu 66 walitoweka baada ya ajali hiyo ya meli, ni pamoja na watoto 26, baadhi yao wakiwa na umri wa miezi michache.

Takriban wahamiaji 3,155 wamekufa au kutoweka katika Bahari ya Mediterania mwaka jana, kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa na 1,000 wamekufa mwaka huu.

Mediterania ya Kati, eneo kati ya pwani ya Afrika Kaskazini na Italia na Malta, ndiyo njia mbaya zaidi inayojulikana ya uhamiaji duniani, ikichukua asilimia 80 ya vifo na kutoweka kwa watu wengi.

Related Posts