Mirerani. Mkazi wa Kitongoji cha Kazamoyo katika mji mdogo wa Mirerani, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, amejeruhiwa mgongoni akidaiwa kumwagiwa maji ya moto na mkewe.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Juni 19, 2024, Ouma Odauseri amesema alifanyiwa ukatili huo Juni 18, 2024 kwa kumwagiwa maji ya moto na mkewe, Flora Daniel ambaye anashikiliwa na polisi, baada ya kuyachemsha kwenye jiko la gesi.
Odauseri amesema chanzo cha mkewe kufikia hatua hiyo ni ugomvi baina yao ambao umekuwa ukitokea mara kwa mara, akidai unasababishwa na ukorofi wa mke wake.
Amesema ameishi na mke huyo kwa zaidi ya miaka 24 na wana watoto watatu, mmoja ameolewa, wa pili yupo kidato cha nne na mwingine yupo shule ya msingi.
“Siku ya tukio alikuwa ametoka kukesha kwenye disko na kurudi nyumbani nikagombana naye akachemsha maji kwenye jiko la gesi na kunimwagia lakini kwa bahati nzuri nikainama yakatua mgongoni,” amesema.
Amesema miaka ya hivi karibuni wamekuwa na ugomvi wa mara kwa mara ambapo mke wake huwa anampiga kibao na kumtukana kila wakati lakini hakuchukua hatua yoyote.
“Ni mtu ambaye amezeeka lakini anaendekeza starehe kwa kulala disko na baa na anaweza kuondoka nyumbani hata mwaka na kurudi kibabe bila kutaka kuulizwa alipokuwa,” amesema.
Amesema mwanamke huyo amekuwa anamnyanyasa lakini anashindwa kumchukulia hatua kwani kuna wakati alimpiga hadi watu wakaingilia kati, hivyo hafanyi chochote.
“Ila kwa hili la kutaka kuniua kwa kunimwagia maji ya moto, acha twende mahakamani kwenye kesi, kwani alidhamiria kunifanyia jambo baya,” amesema.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, George Katabazi amesema wanamshikilia mwanamke huyo, Flora Daniel anayedaiwa kufanya tukio hilo.
Kamanda Katabazi amesema wanatarajia kumfikisha mahakmani mwanamke huyo kwa kosa la kumjeruhi mumewe kwa kumuunguza mgongoni na maji ya moto.
Mmoja kati ya shuhuda wa tukio hilo ambaye ni jirani yao, Patricia Ibrahim amesema mwanamke huyo amefanya jambo baya lakini ugomvi wao wa mara kwa mara ndiyo umesababisha hali hiyo.
“Mwanamke amekuwa analewa na kutoa matusi kila wakati, yaani kama si mtoto kumwambia baba yake mama anataka kukuchoma na maji ya moto ameyachemsha kwenye jiko la gesi, angeungua usoni na kichwani,” amesema.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kazamoyo, Hamad Malya amesema wamechoka kusuluhisha ugomvi wa wawili hao kila wakati, hivyo suala hilo ni bora lifikishwe mahakamani.
Malya amesema zaidi ya miaka mitatu ofisi yake imekuwa ikisuluhisha tatizo hilo na mwanamke huyo amekuwa chanzo cha mgogoro huo.
“Yule mama ni mkorofi na jamaa yake huwa anamwacha tu, kwani anaweza kumkuta mumewe na kumpiga kibao bila sababu,” amesema.