Moshi. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amefika nyumbani kwa aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro (RAS), Tixon Nzunda (56) kutoa salamu za pole.
Mbowe akiwa ameambatana na viongozi wa chama hicho Mkoa wa Kilimanjaro, alifika nyumbani hapo jioni ya leo Jumatano Juni 19, 2024.
Nzunda na dereva wake, Alphonce Edson (54) walifariki dunia jana Jumanne, kwa ajali ya gari iliyotokea eneo la Njiapanda ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) wakati wakienda kumpokea Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ambaye alikuwa anaenda Arusha kikazi.
Mbowe baada ya kufika nyumbani hapo, amesalimiana na viongozi wa Serikali waliokuwepo kisha kusaini kitabu cha maombolezo kabla ya kuingia ndani kutoa pole kwa mjane wa Nzunda, wafiwa wengine na kisha kuondoka.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana usiku na Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Simon Maigwa, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari aina ya Scania, aliyeshindwa kulimudu gari lake na kwenda kugonga gari la RAS na kusababisha vifo hivyo.
Mwili Nzunda utasafirishwa kwa ndege ya Serikali kutoka Kilimanjaro kwenda nyumbani kwake, Goba, Dar es Salaam kwa kesho Alhamisi.
Kisha utasafirishwa Ijumaa ya wiki hii kwenda kijijini kwao, Mkoa wa Songwe kwa mazishi yanayotarajia kufanyika Jumamosi Juni 22, 2024.