TFF, Yanga kumekucha… | Mwanaspoti

YANGA wamewaambia mashabiki wao mitandaoni kwamba wameshamaliza madai kwa kuwalipa wachezaji wao wawili walioifungulia kesi Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetoa msisitizo kwamba hatua ya kufunguliwa kwa Yanga bado.

Mapema Jana, Ofisa Habari wa Yanga Ally Kamwe, akizungumza na kituo cha Azam TV, amesema tayari klabu yao imeshafanya malipo kwa kuwalipa wachezaji hao, Lazarous Kambole na beki Mamadou Doumbia,ambao walisitishiwa mikataba na klabu hiyo.

Kamwe amesema wamewasilisha kwa FIFA nyaraka za malipo hayo, ambapo Shirikisho hilo litakuwa na jukumu ya kujiridhisha juu ya malipo hayo kwa wachezaji hao.

Baada ya taarifa hiyo ya Kamwe,TFF kupitia Msemaji wake Clifford Ndimbo, amesema bado Yanga iko kwenye zuio la usajili mpaka FIFA itakapotoa taarifa.

Ndimbo amesema kwasasa Yanga bado haiwezi kufanya lolote kwenye dirisha la usajili lililofunguliwa Juni 15, kutokana na kesi hizo ambapo kama itamalizana na FIFA haraka watarudishiwa nafasi ya kusajili.

“Mpaka Sasa bado kinachoonekana wako (Yanga) zuio, kwahiyo kama wakimaliza hilo na FIFA ikijiridhisha watafunguliwa dirisha kuendelea na usajili,”amesema Ndimbo.

“FIFA pekee ndio wana nafasi ya kuifungulia timu iliyofungiwa hili hatuhusiki nalo TFF wao wakishaifingulia timu yoyote iliyozuiwa tutajulishwa na tutatoa taarifa kwa umma kama ambavyo tumefanya wakati wa kufungiwa.”

Related Posts