Kamatakamata ya ‘makahaba’ Dar yadaiwa kukiuka haki ya faragha

Dar es Salaam. Sakata la ukamataji wanawake wanaodaiwa kujihusisha na biashara ya ukahaba, limeibua mjadala kutoka kwa wanaharakati.

Ukamataji huo pia unahusisha wanaume wanaokuwa na wanawake hao bila kujali kama wanahusika ama la.

Hata hivyo, uchunguzi wa Mwananchi umebaini licha ya ukamataji kufanyika, bado hurejea katika maeneo hayo na kuendelea na shughuli zao kama kawaida.

Kwa wiki tatu zilizopita, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hassan Bomboko aliendesha operesheni kuwakamata watuhumiwa hao katika maeneo ya Ubungo Riverside na Sinza.

Hata hivyo, baadhi ya wanaharakati wamekosoa operesheni hiyo, wakisema inakiuka haki za binadamu.

Mwanaharakati wa haki za binadamu, Dk Hellen Kijo-Bisimba, akizungumza na Mwananchi alisema kinachofanyika ni kuingilia faragha za watu kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano. “Kama lengo ni kulinda maadili, hata kuingilia faragha ya watu ni kosa kisheria,” alisema.

Dk Kijo-Bisimba alisema sheria zina utata katika kudhibiti biashara ya ukahaba.

“Sheria ya Kanuni ya Adhabu inasema mtu anayetumia mapato yatokanayo na ukahaba ndiye anayefanya kosa.” Kwa nini wanaonunua madada poa wasiwe na kosa? Kama mwanamke anauza mwili, maana yake yupo mnunuzi. Unajuaje kwamba huyu anajiuza? Maana wengine ni wapita njia tu?” alisema.

Alizungumzia pia operesheni iliyowahi kufanyika ya kuvunja nyumba zinazodaiwa kuwa madanguro, akisema ulikuwa uonevu. “Walivunja nyumba za watu masikini, maana ukahaba unafanyika hadi kwenye hoteli za nyota tano. Kwa nini wabomoe nyumba badala ya kufanya tu marekebisho ya matumizi? Hata hao wanawake wanaojiuza wanatakiwa kurekebishwa tu, maana wengine wana tabia tu ya kujiuza hata kama hana shida ya hela,” alisema.

Mwanaharakati, Mary Ndaro alisema haina maana yoyote akifafanua:

“Kwanza, nguvu iliyotumika ni kubwa na haikustahili. Kwa nini watu wanapoenda kufurahia maisha wakamatwe? Kwamba sasa ukienda baa unajikuta umepanda karandinga? Mpaka uje ujitetee useme sihusiki utakuwa umeshachakazwa. Kwangu haiingii akilini.”

Mary akizungumza kupitia mitandao ya kijamii alisema anawatetea wanawake wanaotuhumiwa kujiuza kwa kuwa wana haki kama binadamu wengine.

“Itikadi ya kifeminia inayoniongoza, nikiona dada yeyote yuko kwenye changamoto huwa nasimama naye kwa sababu ya thamani ya utu, siyo juu yangu kuunga mkono biashara wanayofanya, ile ni miili yao, wana uamuzi nayo. Ninawaheshimu na kuwathamini kama binadamu. Ukitaka kumwondoa unampeleka wapi? Umempa mbadala au unamwondoa halafu ukamrushe huko unapotaka?” alihoji.

Alisema katika jamii kuna maovu mengi yanayoendelea na siyo ukahaba pekee.

“Kama ni magonjwa wale ndio wanaojilinda zaidi kwa sababu wanajua wanafanya biashara. Huyu ana mteja wake, kwa mfano mimi najiuza nyumbani kwangu, amekuja mteja nimempa huduma ameondoka, nina mteja mwingine saa nane nimempa huduma ameondoka, na mwingine saa 12.00, mimi nakuathiri nini wewe?” alihoji.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Bomboko alisema haki zote zilifuatwa katika ukamataji, ikiwemo kuwekwa huru kwa dhamana.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuendelea kuwapo ukahaba katika maeneo kadhaa, yakiwamo Riverside na Sinza, ambako operesheni ilifanyika.

Saa nne usiku eneo la Riverside, mwandishi aliwakuta wakiendelea na shughuli zao kama kawaida.

“Hapa hili haliwezi kwisha, kama huamini ngoja nikupitishe,” anasema dereva wa bodaboda aliyefuatana na mwandishi.

Katika baadhi ya barabara eneo la Riverside baadhi ya wanawake walikuwa wamekaa vijiweni nje ya nyumba, wengine wakiwa wamesimama.

“Umeona hao waliokaa, wanajiuza, usije kudhani wako nyumbani kwao,” anasema bodaboda huyo.

Hata hivyo, anasema idadi yao ni ndogo tofauti na awali. Hali kama hiyo ilionekana Sinza, baadhi ya watu waliendelea na shughuli hizo.

Maeneo yenye mwanga hafifu ndiyo yaliyotumika kwa wanawake hao kuendelea na shughuli zao. “Hii vita ni ngumu, si ya siku moja, labda wanaowanunua wote wakamatwe,” anasema Kilian Mtweve, mkazi wa Sinza, Mtaa wa Nzasa.

Anasema uwepo wa biashara hiyo iliyoota mizizi inaweka ugumu katika makuzi ya watoto, hasa wanaowahi kuamka kwenda shuleni.

“Wengine hawana staha, hawana hata muda wa kuchukua vyumba wakafanye shughuli zao, vichochoro wao ndio wanatumia, sasa wakati mwingine wakishalewa sana asubuhi mtoto hukuta vitu vya ajabu,” anasema Mtweve.

Mariam Juma, mfanyabiashara mkazi wa Sinza amesema biashara hiyo imemfanya akose usaidizi wa mtoto wake wa darasa la sita kutokana na wogo asije kushuhudia yanayofanywa.

“Duka nafunga saa tatu usiku, ikifika saa mbili wameshaanza kusimama, mtoto asijekuwa anaenda kujisaidia huko nyuma akakutana na vitu vya ajabu,” anasema.

Malalamiko kama hayo yapo pia Ubungo, ambako mmoja wa wazazi anasema jirani yake alihama baada ya mtoto kuokota kondomu iliyotumika akidhani ni puto.

“Mama yule alichanganyikiwa, alihama hajamaliza kodi, maana aliwaza akiwa kazini mangapi yanatokea nyuma hajui. Sisi tunaokaa kwenye nyumba za wazazi wetu ndiyo hatujui kitu cha kufanya,” anasema Zubeda Yassin.

“Kuna wakati ikifika saa 12.00 jioni wameshajipanga njiani, kiasi unaogopa kumtuma mtoto dukani, huwezi jua atakutana na nini, asubuhi akiamka kwenda shule unawaza kama njiani kumeshakuwa safi,” anasema.

Si hao tu, wanaokwenda kusali, wakiwamo waumini wa dini ya Kiislamu wanaeleza wanakwazwa na hali hiyo.

“Hapa Riverside ikifika saa 12.00 jioni wameshajipanga, kuna siku nikiwa naenda msikitini nilipita kwenye uchochoro nikavutwa kanzu, ilibidi safari iishie hapo maana nilitumia lugha mbaya,” anasema Abdurahman Abdul.

Baa zikitajwa kuwa vichocheo vya uwepo wa biashara hizo, wamiliki wanapinga.

Mmiliki wa baa Riverside, ambaye hakutaka kutajwa jina lake anasema biashara ya ukahaba humuathiri hata yeye kwa kuwa baadhi ya wateja hawataki kusumbuliwa, na wakibaini mmiliki anahusika huhama. “Hapa kwangu ni marufuku kukanyaga, lakini sehemu ambayo wateja wanaegesha magari wanasimama, mtu akitoka anakuta gari limezungukwa, siku nyingine harudi, tunakosa wateja kwa sababu yao,” anasema.

Akizungumza katika baa maarufu iliyoko Tabata, mmoja wa wahudumu anasema mitindo ya uvaaji husababisha ugumu kutambua nani anafanya biashara hiyo. “Labda mlinzi awe anamfahamu ndipo atamzuia, ukisema uangalie nguo asilimia kubwa mavazi yao yanafanana na wateja tunaowahudumia, si kwamba tunawalinda ila ni ngumu kuwachambua mmojammoja,” anasema.

Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Nzasa, Kata ya Sinza, Edwin Mfanga anasema kabla ya operesheni iliyofanywa na mkuu wa wilaya, jitihada kadhaa zilishafanyika kukomesha biashara hiyo. Mfanga anasema malalamiko yaliwahi kufika hadi kwa mkuu wa wilaya, hali iliyofanya moja ya baa kufungwa kwa muda.

“Baadhi ya watu walioona hawawezi kumudu hali hii walihama, pia kwa ajili ya makuzi ya watoto wao,” anasema.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Mtaa wa Kibangu, Desderi Ishengo anasema kukamatwa kwa watuhumiwa wa biashara hiyo haitoshi kuidhibiti.

“Ugumu wa zoezi hili ni watu wanaomiliki shughuli hizo, leo utakamata madada poa watatu, wanne, watano, kesho wanarudi, wanaomiliki shughuli hizo, nyumba za wageni ndio wa kushughulika nao,” anasema. Ishengo, maarufu Mzee wa usiku kama Mchana anasema hali hiyo imefanya kuwapo malalamiko mengi ofisini kwake, baadhi ya watu wakikimbia nyumba zao.

Related Posts