Geita. Mahakama Kuu Kanda ya Geita imemhukumu kunyongwa hadi kufa, Anold Shemas baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumuua kwa kukusudia mtoto wake, Anna Shemas mwenye umri wa mwezi mmoja kutokana na mtoto huyo kutofanana naye.
Kesi hiyo ya jinai namba 53 ya mwaka 2022, Shemasi alikuwa akikabiliwa na kesi ya mauaji, akidaiwa kuua kwa makusudi mtoto wake, Anna Shemas, Oktoba 19, 2021 katika Kijiji cha Kakumbi kilichopo Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita kinyume na kifungu 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu, sura ya 16, kama kilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Akitoa hukumu hiyo Juni 19, 2024, Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Kelvin Mhina amesema upande wa mashtaka umethibitisha pasi na shaka kuwa mshtakiwa alimuua Anna Shemas kwa kukusudia kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha kanuni ya adhabu, sura ya 16.
Akisoma hukumu hiyo kwa dakika 55, Jaji Mhina ameeleza kuwa Mahakama baada ya kuangalia ushahidi wa pande zote mbili, mambo ya msingi ya kuthibitishwa ni kuwa kweli mtoto alifariki, kifo kilikuwa sio cha kawaida na kama kweli mshtakiwa alihusika.
Jaji Mhina amesema hakuna ushahidi wa macho unaothibitisha mshtakiwa kuhusika lakini ushahidi wa kimazingira na ukiri wa mshtakiwa unadhihirisha Anna Shemas ni marehemu.
Kwa mujibu wa ushahidi wa shahidi wa tatu na wa tano unaonyesha mshtakiwa alimchukua mtoto na hakurudi naye huku ushahidi wa shahidi wa sita ambaye ni dereva bodaboda ukionyesha alimbeba mtuhumiwa akiwa na mtoto kwenda Lugito lakini hakurudi naye.
Pia, ushahidi wa shahidi wa tatu na wa tano unaonyesha mshtakiwa ndiye alikuwa mtu wa mwisho kuonekana na mtoto (marehemu) akiahidi kumpeleka hospitali kwa kuwa alikuwa akiumwa.
Ameeleza kwamba kwa mujibu wa maelezo ya onyo ya mshtakiwa ambayo yanathibitishwa pia na shahidi wa tatu, tano na sita unaonyesha mwili wa marehemu uliopatikana eneo la Lugito, ni wa marehemu Anna Shemas.
Amesema kwa mujibu wa uchunguzi wa daktari unathibitisha kuwa Anna Shemas hakufa kifo cha kawaida kwa kuwa alinyongwa na kusababisha kukosa hewa na mwili uliokutwa kwenye maji haukuwa na maji tumboni, hivyo kuthibitisha kifo chake hakikuwa cha kawaida.
“Ushahidi wa shahidi wa 3, 5, 6 na 1 unamuunganisha mshtakiwa na mazingira yanaonyesha kwamba hakuna mtu mwingine aliyemchukua marehemu na kumtupa eneo la Lugito, yeye ndiye alikuwa mtu wa mwisho kuonekana na marehemu na kwa ushahidi huo mshtakiwa ndiye amesababisha kifo cha marehemu,” ameeleza jaji.
Ameeleza kuwa pamoja na kuwa hakuna ushahidi wa macho, ukiri wa mshatakiwa na ushahidi wa shahidi wa 1, 3, 5 na 6 unaunga mkono maelezo ya onyo ya mshtakiwa ambaye alikiri kumuua marehemu.
Wakili wa upande wa mashtaka, Scolastica Teffe akizungumza baada ya mshtakiwa kutiwa hatiani, amedai upande wa mashtaka hauna kumbukumbu ya makosa mengine aliyofanya mshtakiwa lakini akaiomba mahakama kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine.
Wakili upande wa utetezi, Elizabeth Msechu ameiomba Mahakama kumuonea huruma mteja wake na kumpunguzia adhabu kwa kuwa anategemewa kama kaka mkubwa kwenye familia aliyokuwa akiwalea wazazi wake lakini pia ni nguvu kazi ya Taifa.
Akitoa hukumu hiyo, Jaji Mhina amesema kwa mujibu wa sheria za Tanzania, kosa la mauaji likithibitishwa kwa mujibu wa kifungu cha 197 cha Sheria ya Makosa ya Jinai, adhabu ni hukumu ya kifo, hivyo mshtakiwa atanyongwa hadi kufa.