Vilio, simanzi vyatawala nyumbani kwa RAS Kilimanjaro

Moshi. Vilio na simanzi vimetawala nyumbani kwa aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Tixon Nzunda (56) aliyefariki kwa ajali ya gari yeye na dereva wake wakati mwili huo ulipowasili nyumbani kwake Shanty Town, Manispaa ya Moshi, mkoani humo, saa 4:50 asubuhi, ukitokea Hospitali ya KCMC ulikokuwa umehifadhiwa.

Tixon yeye na dereva wake, Alphonce Edson (54) walifariki juzi Juni 18, 2024  kwa ajali ya gari iliyotokea saa 8:30 mchana katika eneo la Njia panda ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), wakati wakienda kumpokea Makamu  wa  Rais, Dk Philip  Mpango ambaye alikuwa akielekea mkoani Arusha kikazi.

Vijana wa Msalaba mwekundu (Red cross) pamoja na vijana wa Skauti wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Tixon Nzunda ambaye alifariki kwa ajali  Juni 18.

Viongozi mbalimbali wa chama na serikali, viongozi wa dini, watumishi wa serikali mkoani humo, wabunge, wakuu wa taasisi mbalimbali za serikali na zisizo za serikali pamoja na  wananchi wamefika nyumbani hapo kushiriki ibada fupi ya kuaga mwili huo.

Hata hivyo, baada ya mwili huo kuwasili  nyumbani hapo  umeingizwa ndani kwa ajili ya ibada fupi ya kifamilia na kisha mwili huo itatolewa nje kwa ajili ya ibada maalumu na wananchi waliofika kupata fursa ya kuaga na kutoa heshima za mwisho.

Ratiba iliyotolewa jana na  Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema mwili wa Tixon  baada ya kuagwa nyumbani kwake leo saa 10 alasiri mwili huo utapelekwa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro na kisha  kusafirishwa kupelekwa Goba, Dar es salaam kwa ndege ya Serikali.

Kesho  Ijumaa, Juni 21 mwili huo utapelekwa Songwe kwa mazishi ambayo yatafanyika siku ya Jumamosi, Juni 22.

Endelea kufuatilia mitandao yetu.

Related Posts