Moro yatakata, Wanyeche moto gofu ya Alliance 

ILIKUSANYA zaidi ya wacheza gofu 150 kutoka vilabu vyote nchini, michuano ya mwaka huu ya Alliance iliyotamatika katika viwanja vya Gymkhana mjini Morogoro mwishoni mwa juma itabaki kuwa na historia nzuri ya ubora wa matokeo kwa msimu huu.

Kwa mujibu wa Seif Mcharo, ambaye ni nahodha wa klabu ya gofu ya Morogoro Gymkhana, uitikio wa wachezaji ulikuwa mzuri na kuwepo kwa mashindano kuliuongezea mji wa Morogoro shamra shamra za mwisho wa juma na sikukuu ya Eid.

“Kifupi mahudhurio makubwa na wachezaji kurudisha alama nzuri vilisaidia kuyang’arisha mashindano yetu na wengi wamefurahia kucheza katika uwanja wetu ambao ni wa pekee wenye rangi ya kahawia(brown course),” alisema Mcharo ambaye pia ni moja ya wachezaji waliofanya vizuri kaika mashindano ya mwaka huu.

Michuano ya mwaka huu ya Alliance ilishirikisha wachezaji wa kulipwa na wa ridhaa kutoka vilabu vya Dar es Salaam Gymkana, TPDF Lugalo,   Arusha, TPC, Kilimanjaro, Mufind Iringa na wenyeji Morogoro Gymkhana.

Baada ya mtifuano wa mashimo 54  yaliyochezwa kwa siku tatu, mchezaji kutoka Kili Golf Club ya Arusha,Enosh Wanyeche ndiye  aliyeibuka shujaa wa michuano baada ya kuzamisha mpira kwenye mashimo 54 kwa jumla ya mikwaju 225.

Wanyeche alianza kampeni ya ushindi kwa kupiga mikwaju 70 siku ya kwanza  na siku iliyofuata  alicheza mikwaju 76 kabla ya kumaliza  mashimo kwa kupata mikwaju 79  iliyomfanya ashinde kwa jumla ya mikwaju 225  na kumpiga mpinzani wake wa karibu, Michael Massawe  kwa mikwaju saba.

Akimaliza nafasi ya pili, Massawe  alipata jumla ya mikwaju 232. Alinza vibaya kwa kupiga mikwaju  80 siku ya kwanza na kuiboresha kidogo siku ya pili kwa mikwaju 79, lakini alikuwa mkali sana siku ya tatu ambapo alipiga mikwaju 73 ambayo ilimsaidia sana dhidi ya wapinzani wake wa karibu.

Wachezaji watatu;Julius Mwizani, Seif Mcharo  na Isihaka Daudi walifungana katika nafasi ya tatu baada ya wote kupata jumla ya mikwaju 233. Kwa sharia ya gofu ya kuhesabu kuanzia mwisho (countback),Mwizani akamaliza wa tatu, Mcharo wa nne na Isihaka Daudi kushika nafasi ya tano. Nafasi ya sita ilishikwa na Prosper Emanuel alyepiga jumla ya mikwaju 235.

Shufaa Twalib aliyepiga mikwaju 148,  ndiye aliyetangazwa mshindi wa wanawake na kufuatiwa  na Christina Charles aliyepata mikwaju 149 huku nafasi ya tatu ikatwaliwa na Asteria Kinunda  aliyechapa mikwaju 150.

Mchezaji bora kwa ujumla (gross) kwa wanawake alikuwa ni Vicky Elias wa Dar es Salaam aliyelenga mashimo kwa mikwaju 164 na kufuatiwa na Loveness Frank  aliyepiga mikwaju 172 wakati  alimaliza wa tatu, Ayne Magombe.

Related Posts