ANZANIA KUOKOA MABILIONI UJENZI WA TANZANIA TWIN TOWER KENYA

 

 

 

SERIKALI ya Tanzania Juni 18 2024 imezindua rasmi ujenzi wa majengo pacha jijini Nairobi, Kenya yatakayotumika na ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini humo na kitega uchumi.

 

Ujenzi huo ambao ni uwekezaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF utajengwa katika eneo la kibiashara katikati ya jiji la Nairobi kwenye eneo ambalo Serikali ya Kenya iliipa Tanzania kwa ajili ya kujenga ofisi zake za ubalozi.

 

Akizungumza katika tukio la uzinduzi huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, amesema mradi huo ni sehemu ya mkakati mpya wa serikali kuhakikisha inatumia maeneo na majengo yake yaliyopo ughaibuni kuingiza fedha za kigeni badala ya kutumia fedha za serikali kuendesha ofisi hizo.

 

Waziri Makamba amesema mkakati wa serikali unataka kuiondoa Tanzania kutoka kutumia kiasi cha shilingi bilioni 29 kwa mwaka kulipa kodi kwenye balozi zake ughaibuni na badala yake kuingiza kiasi cha shilingi bilioni 36 kwa mwaka kama mapato ya uwekezaji kama huo wa unaofanyika Kenya.

 

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Walemavu), Deo Ndejembi, amesema mradi huo umefanyika baada ya upembuzi yakinifu wa kina uliofanywa na kubainisha faida itakayopatikana baada ya kukamilika kwa ujenzi huo.

Mgeni rasmi katika tukio hilo, Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Mhe. Musalia Mudavadi, alipongeza Serikali ya Tanzania kujenga jengo hilo akisema litakuwa mojawapo ya alama za kudumu za uhusiano wa kirafiki baina ya nchi hizo mbili.

Mudavadi ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Fedha wa Kenya, alisema serikali yao pia imejifunza kitu kuhusu namna ya kutumia fedha za taasisi kama NSSF kwa kufanya uwekezaji ili zizalishe zaidi na kuwa muda si mrefu, Kenya itafuata nyayo za Tanzania kwenye utaratibu huo.

Related Posts